LAKINI BWANA HAKUWAPA MOYO WA KUJUA.

Biblia kwa kina No Comments

LAKINI BWANA HAKUWAPA MOYO WA KUJUA.

Kumbukumbu la Torati 29:1 “Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote BWANA aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote;

[3]yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu;

[4]lakini BWANA hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi”.

Ndugu Kama hutataka kuitii sauti ya Roho Mtakatifu inayokulilia leo umgeukie Mungu, basi fahamu kuwa kuna wakati utafika hautasikia tena hiyo sauti wala hautaona tena ishara yoyote ambayo itakuaminisha kuwa Mungu anasema na wewe. Wakati huo utakuwa unadharau tu na kutukana watu wanaokuhubiria habari za wokovu, kwasababu gani?

Kwasababu ule moyo wa kutubu hautakuwanayo tena, yale masikio ya kusikia sauti ya Mungu hautakuwanayo tena, wala hautaona tena chochote!, utabakia tu kuwa kama Farao ambaye pamoja na kuwa ameona ishara nyingi na miujiza kutoka kwa Mungu.. lakini hakukubali kunyenyekea. Kwasababu Bwana hakumpa moyo wa kujua, wala masikio ya kusikia, wala macho ya kuona.

Bwana Yesu alisema maneno haya ambayo tunayasoma katika..

Yohana 6:44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho.

Ndugu, fahamu kuwa wokovu ni wa kuchaguliwa na Mungu, hatujiamurii tu wenyewe.Tunajaliwa/tunavutwa kwa nguvu za Mungu tuokoke.

Kama hatutajaliwa na Mungu, haijalishi tutahubiriwa injili mara ngapi,tutaona miujiza mingi kiasi gani, tutatokewa na Yesu mara ngapi, kamwe hatuwezi kubadilika, Farao aliona miujiza mkubwa sana kutoka kwa Musa, lakini Mungu hakumpa moyo wa kutubu.

Hivyo uisikiapo sauti ya Mungu inaugua ndani yako, usiipuzie hata kidogo, chukua hatua haraka badilika. Kubali kutubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, Upokee kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwasababu hiyo sauti haitadumu milele ndani yako. Upo wakati itanyamaza kimya. Wakati huo hata uhubiriweje hautasikia tena kuchomwa moyoni mwako.

Wakati huo dhambi inakuwa ni kitu cha kawaida sana kwako, hata ukibaka mnyama, hata ukiua, hata ukifanya ushoga, hata ukikufuru mbele za Mungu kwako ni kama jambo la kawaida tu.

Ni kwasababu gani, kwasababu ile neema imekwisha ondolewa juu yako kwasababu ulidharau na kuipuuzia kwa muda mrefu.

Ndugu, Njia za Mungu huwa ZINATISHA, na ndio maana tumeambiwa TUZITAFAKARI VEMA KAZI ZAKE,

Mhubiri 7:13 “Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?”.

Watu wengi hawapendi kusikia maneno hayo kwamba Mungu anao uwezo wa kumletea mtu nguvu ya upotevu ili apotee,. Ni kweli Mungu hawezi kumletea mtu nguvu ya upotevu kwa yeye ambaye hajaijua neema bado lakini kwake yeye aliyeisikia na kuipuuzia na kuikataa, nguvu hiyo ya upotevu inaachiliwa juu yake, na nguvu hiyo haitoki kwa shetani bali inatoka kwa Mungu mwenyewe.

Soma >>

1Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 KWA HIYO MUNGU AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, WAUAMINI UONGO;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.”

Mhubiri 7:13 “Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?”.

Tuitafakari kazi ya Mungu vema (neema ya wokovu), sio tu kuzichukulia juu juu, Tukidhani kuwa hukumu za Mungu zinachunguzika kwamba nitaokoka tu siku moja! Au Tunasema Mungu ataokoa tu!, Mungu tu ataokoa tu! Na huku tunadumu katika dhambi tukidhani kuwa neema ni kitu cha kukifanyia mzaha. Kumbuka hilo neno lenyewe NEEMA ni kitu kinachoonyesha kuwa ni jambo AMBALO HUKUSTAHILI KULIPATA NI KWA HURUMA TU UMEPEWA, lakini unaendelea kulifanyia mzaha kana kwamba ulistahili kuipata ni haki yako?.

Unadhani NGUVU HIYO YA UPOTEVU itakapokujia juu yako ikiwa hautubu leo, na kusimama imara katika Kristo siku ile ya hukumu utasema Mungu ni MDHALIMU alikuletea mabaya kwa makusudi?.

Ndugu Itafakari vema kazi ya Mungu ili ujue leo hii unasimamia wapi!?

Mungu alishamaliza mambo yote kabla hata ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, majina ya watakaookolewa Mungu alishayaandika katika kitabu cha uzima kabla ya misingi ya ulimwengu kuwekwa biblia inasema hivyo

Ufunuo 17.8 “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. NA HAO WAKAAO JUU YA NCHI,WASIOANDIKWA MAJINA YAO KATIKA KITABU CHA UZIMA TANGU KUWEKWA MISINGI YA ULIMWENGU, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako”.

Embu tafakari kwa makini habari hii utajifunza jambo.

Warumi 9:11 “(kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye),

12 aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo.

13 Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.

14 Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha!

15 Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye.

16 Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.

17 Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.

18 Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.

19 Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?

20 La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu?Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?

21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?

22 Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;

23 tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;”

Je! Wewe ni chombo cha ghadhabu kilichowekwa tayari kwa uharibifu, au ni kile chombo cha rehema?. Jua tu ikiwa unaukwepa msalaba, ikiwa unaukwepa wokovu, ikiwa unaikwepa toba, ile nguvu ya upotevu mfano wa ile iliyokuwa juu farao ambayo HATA AONE MIUJIZA MIKUBWA KIASI GANI HAWEZI KUTUBU, NDIYO ITAKAYOKUJA JUU YAKO KAMA UTAENDELEA KUUPINGA WOKOVU NDANI YA MOYO WAKO.

Leo hii umeshaisikia injili mara ngapi, umehubiriwa uache uzinzi mara ngapi ewe kijana ewe binti,? umehubiriwa utubu dhambi zako mara ngapi? lakini umekuwa wa kwanza kufanya mizaha? umehubiriwa uache ulevi mara ngapi? unavuta sigara, unaangalia pornoghaphy, unafanya mustarbation, binti unasagana, umekuwa shoga kijana, unaenda kwa waganga, unajifurahisha katika anasa na miziki ya kidunia, mwanamke unavaa suruali, vimini, unapaka rangi kucha, kijana unanyoa mitindo isiyofaa na kusuka nywele ,na tatoo kwenye mwili wako, wanawake usengenyaji na umbea, mtukanaji, unajichanganya na watu waovu kwa jinsi isivyopasa, unachati nao mambo maovu, huku ukijua kabisa watu wanaoyafanya hayo wataishia katika jehanum ya moto, JE! UNADHANI NEEMA YA MUNGU ITAENDELEA KUDUMU JUU YAKO MILELE?. Mungu hadhihakiwi apandacho mtu ndicho atakachokivuna. Tutawezaje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?.

Kwahiyo ndugu maneno hayo hayakuogopeshi?? TUBU! yamkini hii sauti ya upole inayokuambia kila siku utubu bado inaendelea KULIA NDANI YAKO! ..itii na ugeuke maana upo katika HATARI, Maana hiyo sauti haitadumu milele ndani yako. Na ikishaondoka hakutakuwa na njia ya kurudi tena. YAANI MOYO WA KUTUBU hautakuwepo tena ndani yako utafanana na hao watu unaowaona huko ulimwenguni watendao matendo ya giza si kana kwamba hawasikii au hawakusikia injili hapana lakini hawana tena mioyo ya kutubu, na hawatakaa wasikie tena na kubadilika, ndugu usifanane nao. Mtii Mungu tubu dhambi zako muda umeenda sana kuliko unavyofikiria.Yesu yupo mlangoni kurudi.

Ufunuo 22:10 “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia. MWENYE KUDHULUMU NA AZIDI KUDHULUMU; na MWENYE UCHAFU AZIDI KUWA MCHAFU; na MWENYE HAKI AZIDI KUFANYA HAKI; na MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA.Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. “

Kumbuka kutubu ni KUGEUKA( au KUACHA DHAMBI) na sio sala ya toba tu. Maana yake unaumua kuacha dhambi zote na namna zote za ulimwengu huu kabisa kabisa.

Hivyo ukiwa umedhamiria kufanya hivyo moyoni mwako kwadhati kabisa na kutaka kumwishia Kristo kuanzia sasa na kuendelea. Unachopaswa kufanya ni kwenda kutafuta mahali ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kimaandiko, yaani ubatizo wa kuzamishwa, katika maji mengi na jina linalotumika liwe ni JINA LA YESU KRISTO na si linginelo. Ili upate ondoleo la dhambi zako, Kulingana na matendo2:38,na Bwana mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu kuanzia huo wakati na kuendelea kukusaidia kuukulia wokovu na kuishinda dhambi.

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *