LAKINI HAKUJUA YA KUWA BWANA AMEMWACHA.

Biblia kwa kina No Comments

LAKINI HAKUJUA YA KUWA BWANA AMEMWACHA.

Jina la Mwokozi YESU libarikiwe. Karibu tujifunze biblia.

Kama ni msomaji wa biblia utakuwa unafahamu ile habari ya Samsoni na Delila, leo kuna jambo nataka tujifunze katika hiyo habari.

Tukisoma hiyo habari..tunaona baada ya Delila kumsumbua Samsoni kila siku ili atake kujua siri za nguvu zake, hatimaye Samsoni alikuja kumwambia siri yake.. Kwamba nguvu zake zipo katika nywele na hivyo nywele zake zikikatwa ndipo wataweza kumkamata. Hivyo Delila baada ya kujua hilo..hakuchelewa, kwa haraka aliwaita wale Wafilisti na kuwaeleza hiyo siri, Samsoni alipolala usingizi, alinyolewa zile nywele zake na alipoamshwa na kuambiwa Wafilisti wamekuja.. yeye alidhani itakuwa kama siku zote, hakujua kuwa Bwana amemwaacha, alidhani anaweza akaamka na zile nguvu zake na kuwatawanya Wafilisti. Kumbe Bwana alimuacha siku nyingi..kilichobakia ni kukamatwa na kutobolewa macho na kwenda kusagishwa ngano huko gerezani. Hebu tusome kwa ufupi kuna jambo nataka tujifunze hapo.

Waamuzi 16:18 “Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.

[19]Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.

[20]Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. AKAAMKA KATIKA USINGIZI WAKE, AKASEMA, NITAKWENDA NJE KAMA SIKU NYINGINE, NA KUJINYOSHA. LAKINI HAKUJUA YA KUWA BWANA AMEMWACHA.

[21]Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”

Nataka tutafakari huo mastari wa 20 anaposema ”LAKINI HAKUJUA YA KUWA BWANA AMEMWACHA.” Hapo ndipo kiini cha somo letu lipo.

Unaweza ukawa unafanya kazi ya Mungu huku ukidhani Bwana yupo pamoja na wewe.. kumbe Bwana amekuacha siku nyingi pasipo wewe kujua, Vilevile unaweza ukaitwa mkristo na unahudhuria kanisani kila mara, unafanya matendo mema lakini Bwana akawa hayupo na wewe, huku wewe ukidhani Bwana yupo pamoja na wewe kwa vile unapoona ishara na miujiza anayokutendea, au kwa vile unapotumia jina lake na mapepo yakakutii, wagonjwa wakapona..n.k

Ndugu uliyeokoka, angalia sana jinsi unavyoenenda katika wokovu wako, Bwana alisema..

Mathayo 7:21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

[22] WENGI wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.

Wakristo wengi katika hizi siku za mwisho wanaachwa na Bwana pasipo wao kujua, wanapumbazwa na karama walizonazo pasipo kujua kuwa karama za Mungu hazina majuto (Warumi 11:29).

Unaweza ukawa mtumishi na ukafanya miujiza mingi kwa jina la Bwana lakini Bwana hayupo nawe, unaweza ukawa ni mchungaji, nabii, Mtume n.k lakini pamoja na jitihada zako zote.. Bwana anaweza akakuacha bila wewe kujua, haijalishi unahuduma kubwa kiasi gani, au unawaombea watu na wakapona matatizo yao..kama hufanyi mapenzi ya Mungu… fahamu kuwa Bwana hakujui, huwenda mwanzoni alikuwa anakujua lakini alishakuacha siku nyingi. Samsoni alikuwa ni mwamuzi wa taifa lote la Israeli, lakini alipoenda kinyume na mapenzi ya Mungu.. Mungu alimuacha pasipo yeye kujua..na mwisho wake akabaki kuwa kipofu baada ya kutobolewa macho na adui.

Sasa mapenzi ya Mungu ni nini? Biblia imetoa jibu katika..

1 Wathesalonike 4:3 Kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, KUTAKASWA KWENU, MWEPUKANE NA UASHERATI;

[4]kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;

[5]si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu..

Umeona mapenzi ya Mungu haswa, ni kuishi maisha ya utakaso/utakatifu ili tuepukane na uasherati; kwani uasherati ni jambo linalomchafua mtu na kumtenga na Mungu kabisa.. Bwana alisema watu walio kwenye ndoa wanaweza wakatengwa na mambo mawili tu, ”kifo” na “uasherati” (Soma Mathayo 5:32). Na katika roho sisi tulio wakristo wa kweli ni bibi arusi wa Kristo (Tumefunga ndoa na Kristo).

Dhambi ya uasherati ndio dhambi iliyomtenga Mungu na Mwanadamu tangu Edeni, Wana wa Israeli wakiwa jangwani walipigwa kwa pigo kuu kwa dhambi ya uasherati pale walipozini na wanawake wa kiMoabu (Hesabu 25), Samsoni aliachwa na Bwana kwasababu ya uasherati, na halikadhalika katika siku hizi ambayo kila mtu anafahamu kuwa ni siku za mwisho, wakristo wengi wanaachwa na wataachwa kwasababu ya dhambi ya uasherati. Na kibaya zaidi mtu anapoachwa hajui kuwa ameachwa.. kwasababu ufahamu wake umechukuliwa na huo uasherati. Biblia ndivyo inavyosema kuwa..

Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.”(Hosea 4:11)

Na uasherati sio tu kufanya lile tendo, bali hata kuabudu miungu ni uasherati, kuwa na Bwana mwingine zaidi ya Bwana YESU ni uasherati. Huyo Bwana sio lazima awe mtu, bali hata mali ni Bwana..ndivyo biblia inavyosema.

Mathayo 6:24 Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. HAMWEZI KUMTUMIKIA MUNGU NA MALI.

Umeona hapo, hiyo mali inafananishwa na libwana, na hutuwezi kuwatumikia mabwana wawili. Hii ikiwa na maana kuwa na mali sio vibaya.. lakini unapoigeuza kuwa bwana wako..Kwa kuitumikia kiasi kwamba huna muda na Mungu, muda wote unawaza tu hiyo mali, hata ukipoteza unaweza ukazimia, moyo wako wote umetekwa na hiyo mali, usiku na mchana unaihangaikia, siku saba kwa week hupumziki. Basi fahamu kuwa unafanya uasherati na Bwana ni lazima akuache.

Na wakristo wengi katika siku hizi za kumalizia, wanaachwa kwasababu ya huu uzinzi wa kiroho. Mkristo wa kweli anaweza asifanye ule uasherati wa kimwili, lakini wengi wanafanya uasherati wa kiroho pasipo wao kujua na wengi wanaachwa ama wataachwa kwa ajili hiyo.

Bwana anasema..

1 Wakorintho 6:12 Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote.

Kutafuta na kuwa na mali/fedha ni halali, lakini kuweka hivyo kwenye moyo wako inakuwa haifai, kwani inakuwa sio mali tena, sio fedha tena..bali ni mungu. Na huo ndio uasherati wa kiroho.

Halikadhalika na vitu vingine ni halali, lakini sio vyote vinafaa, kuwa na Elimu hata degree zote ni jambo nzuri, lakini kumbuka kuwa hiyo elimu yako inaweza kugeuka na kuwa bwana wako..na hapo ndipo wakristo wengi tunapokosea. Pale ambapo tunakuwa na kiburi kwasababu ya Elimu, au kwasababu ya hadhi fulani, hapo hiyo Elimu haifai tena, huko ni kufanya uasherati.

Halikadhalika kuwa na umbo zuri, sura nzuri ni jambo la kumtukuza Bwana, lakini sasa tunapogeuza uzuri wetu na sura zetu kwa kuongezea uzuri zaidi ya huo tuliopewa, kwasababu tu ya kutafuta utukufu kwa wanadamu ambao sio wao walituumba, hapo tunafanya machukizo makubwa sana pasipo sisi kujua.

Na wengi wanaachwa na wataachwa kwasababu hii.

Bwana alipotuumba, alituumba tukiwa wakamilifu na tena tukiwa wazuri sana machoni pake, lakini sisi tumeona kuwa Mungu aliyetuumba kwa namna ya ajabu, alikosea kutuumba, Mungu alikuumba ukiwa mweusi na akakuona kuwa we ni mzuri na unapendeza machoni pake, lakini wewe leo hii unataka kuwa mweupe uonekane na wanadamu, Kwa hiyo unachukua vitu bandia unabadilisha rangi ya ngozi yako, unachukua rangi unapachika mdomoni uwe na mdomo mwekundu, unachukua rangi unapaka kwenye kucha ili uwe na kucha nyeusi, unachukua vyuma na madhabahu unatoboa masikio yako na pua unaweka, nywele ambazo Bwana alikuumbia..unaona hazifai, unachukua zile bandia unaweka. Na sababu ya kufanya hayo yote ni kwasababu unatafuta utukufu kwa wanadamu..Kwa uasherati huo, kwanini Bwana asikuache??

Isaya 29:16 Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?

Kama Mkristo tafuta kujua na kufanya mapenzi ya Mungu ambayo ni kuishi maisha ya utakatifu wa mwili, nafsi na roho, ili siku ile usije ukawa miongoni mwa wale watakaotupwa nje, na kuambiwa ondokeni kwangu ninyi mliowafanyaji wa udhalimu, japokuwa walifanya miujiza mingi na kutoa mapepo kwa jina la Bwana.

Kaa mbali na uasherati wote..wa kimwili na kiroho. Kwakuwa wengi wanaachwa ama wataachwa kwasababu ya uasherati..wengi leo hii walikuwa ni wachungaji na wainjilisti wa kweli… lakini leo hii wanasagishwa ngano kwenye gereza la ibilisi, wameaachwa siku nyingi pasipo wao kujua kwasababu ya uasherati.

Bwana atupe macho ya kuona na masikio ya kusikia.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *