
LANGO LI WAZI
Mtunzi wa tenzi namba 121 aliimba kwa ufunuo wa Roho, akisema..
1. Liko lango moja wazi, Ni lango la mbinguni; Na wote waingiao Watapata nafasi.
Lango ndiye Yesu Bwana Wote waingie kwake, Lango! Lango La Mbinguni ni wazi.
2. Yesu ndiye lango hili, Hata sasa ni wazi, Kwa wakubwa na wadogo, Tajiri na maskini.
3. Hili ni lango la raha, Ni lango la rehema; Kila mtu apitaye Hana majonzi tena.
4. Tukipita lango hili Tutatua mizigo, Tuliochukua kwanza, Tutavikwa uzima.
5. Hima ndugu tuingie Lango halijafungwa, Likifungwa mara moja Halitafunguliwa.
Hakika YESU KRISTO ndiye lango la mbinguni kila mtu aingiaye kwake ataokoka, yeye mwenyewe alisema..
Yohana 10:1,9 Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi.
[9] MIMI NDIMI MLANGO; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.
Hili lango, mpaka sasa bado lipo wazi, lakini muda sio mrefu litaenda kufungwa.
Swali ni je! umeingia kupitia lango hili?
Kumbuka, kadri siku zinavyoenda mbele ndiyo ile siku inakaribia ya kufungwa kwa lango hili. Hivyo kama bado hujaingia ni heri leo uamue kuingia kabla hujachelewa.
Ezekieli 44:1 “Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa.
2 BWANA AKANIAMBIA, LANGO HILI LITAFUNGWA, HALITAFUNGULIWA, WALA MTU AWAYE YOTE HATAINGIA KWA LANGO HILI, kwa maana Bwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa”.
Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango,…..”.
Ndugu yangu, hizi ni nyakati mbaya sana tunazoishi, leo utaudharau wokovu wa Yesu Kristo, lakini alishatabiri kuwa kuna siku ataufunga mlango huu, na siku hiyo utakapofungwa ndipo watu watakapogundua kuwa walikuwa wanapuuzia kitu cha msingi sana, cha uzima wa roho zao.. Ndipo watakapoanza kubisha wafunguliwe, kumbe hawakujua kuwa lango hilo likishafungwa mara moja, halitafunguliwa tena daima. Kitakachofuata baada ya hapo ni matujo makubwa sana ambayo hayajawahi kutokea duniani kote.
Hivyo wokovu sio wa kukwepwa, injili si ya kudharauliwa wala kupuuziwa kabisa, huu si wakati wa kumwangalia jirani, au ndugu, au mzazi, katika suala lako la wokovu, Ni wakati wa kumkimbilia Kristo na kumwangalia yeye tu, kwasababu muda uliobakia ni mchache, nani ajuaye lango hilo litafungwa leo usiku, au kesho asubuhi. Jiulize Unyakuo ukipita leo halafu ukabaki, na injili zote hizo ulizosikia, na mafundisho yote hayo uliyofundishwa na kujifunza, utaenda kujibu nini mbele ya kiti cha hukumu.
Usikubali kusongwa na jambo lolote, huu mlango umeshakuwa finyu sana. Kuiingia sio mrahisi tena kama tunavyodhani, hivyo ni wakati wa kufanya maamuzi magumu, wa kukubali kujitwika msalaba na kumfuata Yesu, na uwe tayari kwenda kubatizwa na kupokea Mtakatifu.
Bwana akubariki sana.
Ikiwa bado hujabatizwa, na utapenda kupata huduma hiyo ya ubatizo, au kumpa Kristo maisha yako, basi wasiliana nasi inbox au kwa namba zilizopo chini hapo.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.