Madhara ya kuabudu Sanamu.

Biblia kwa kina No Comments

Madhara ya kuabudu Sanamu.

Sanamu ni kitu chochote kile kinachotengenezwa chenye umbile aidha la malaika wa mbinguni, mwanadamu, mnyama, au mimea…Mwanadamu yoyote anayetengeneza kitu chochote chenye mifano ya hivyo vitu tayari kashatengeneza sanamu.

Moja ya amri 10 Mungu alizowapa wana wa Israeli, ilikuwa ni pamoja na kujiepusha na ibada za sanamu za aina yoyote..

Amri ya pili inasema hivi..

Kutoka 20:4 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 

6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”.

Hivyo mtu akikigeuza kitu chochote, kuwa mbadala wa Mungu, huko ni sawa na kuabudu sanamu, ukiweka mdoli nyumbani kwako na kwenda kumpigia magoti na kumwomba kana kwamba ni Mungu, ujue hapo unafanya ibada za sanamu..

Ukitengeneza kinyago chenye sura ya mtakatifu Fulani labda Mariamu, au Bwana Yesu akiwa pale msalabani, kisha ukakihusianisha na mambo ya ibada kwa mfano kukisujudia, au kukiabudu, au kuombea dua zako kwa kupitia hicho, tayari hiyo ni ibada za sanamu,

Ukining’iniza picha ukutani ya mtu Fulani maarufu, au mnyama , au kitu Fulani kwa lengo la kukifanya kama kipatanishi chako na Mungu, au kitu chako kinachoweza kukupa bahati Fulani, hiyo tayari ni ibada za sanamu.

Hata ukipanda mti, au Ua fulani, ukiamini kuwa linaweza kukulinda, au kueleza hatma ya maisha yako, tayari hiyo nayo ni ibada za sanamu.

Kumbukumbu 16:21 “Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako.”

Na ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu, yanayomtia wivu kiasi cha Mungu kukupatilizia maovu hata ya baba zako, uone ni jinsi gani kitendo hicho kinavyomuudhi Mungu..

Lakini mbali na kuwa ibada ya sanamu ni machukizo kwa Mungu, yapo madhara mengi ambayo watu wengi wanaoabudu sanamu hawajui, na leo ukijua kama unaabudu sanamu yoyote sidhani kama utaendelea kuabudu.

Hebu tuangalie madhara ya kuabudu sanamu.

Zaburi 115:4-8 biblia inasema..

4 “Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.

[5]Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,

[6]Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,

[7]Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.

[8]WAZIFANYAZO WATAFANANA NAZO, KILA MMOJA ANAYEZITUMAINIA.”

Hapo mstari wa mwisho anasema “wazifanyazo watafanana nazo, kila mmoja anayezitumainia” unaelewa maana yake?

Maana yake ni kuwa wanaozifanya hizo sanamu, au wanaotengeneza kwa lengo la kuabudu au hata kuzitumainia kiroho wanafanana nazo.

Sasa ni kwa namna gani watafanana nazo?

Hapo ukisoma anasema hizo sanamu zina vinywa lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazisikii harufu, mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, halafu anasema WAZIFANYAZO WATAFANANA NAZO.

Maana yake utakuwa na kinywa lakini hausemi, utakuwa na macho lakini hauoni, utakuwa na masikio lakini hausikii, utakuwa na mikono lakini hazishiki, halikadhalika utakuwa na miguu lakini hazitembei. Kwa ufupi utakuwa sanamu katika roho, huko ndiko kufanana nazo.

Utajiuliza kila unapotaka kupiga hatua ya kimaisha hausogei, kila ukishika vitu havishikiki vinapotea tu! Angalia unaabudu nini, unatumainia nini?

Utapigaje hatua ikiwa miguu yako imegandishwa katika roho, utashikaje vitu ikiwa mikono yako ni sanamu? Utaishia tu kusema unachezewa kumbe! umejigandisha mwenyewe kwa kuabudu masanamu. Biblia haisemi uongo, ni kweli anayezifanya sanamu au kuabudu na kuutumainia kwa namna yoyote ile atafananazo tu, atakuwa na miguu lakini haitembei, atakuwa na mikono lakini hazishiki.

Halikadhalika utakuwa na macho lakini hauoni mambo ya rohoni, utasoma biblia yote lakini hautaelewa, utakuwa na masikio lakini hautasikia!! Utahubiriwa vya kutosha kuwa kuvaa mavazi yasiyopasa jinsia yako ni machukizo kwa Mungu lakini hautasikia, Utahubiriwa na kuonyeshwa kabisa kwenye maandiko kuwa wanawake au wanaume wanaosuka marasta, wanaonyoa denge, wanaobadilisha maumbile yao, wanaoweka alama, au kutoboa miili yao sehemu yao ni jehanamu ya moto lakini hautasikia kwasababu tayari masikio yako yamegandishwa na kufanana na sanamu unayoiabudu.

Hayo ndiyo madhara ya kuabudu sanamu. kuna roho ambayo ipo nyuma ya hizo sanamu, ambayo mtu yoyote atakayeinamia na kusujudia, hiyo roho itaingia ndani yake na kumpofusha macho yake ya rohoni, kuziba masikio yake ya rohoni, na kumgandisha viungo vyote visifanye kazi kabisa.

Kwa nje utaonekana ni mtu mwenye akili, mwenye miguu inayotembea, mikono inayoshika, macho yanayoona na mdomo mzuri lakini kwa ndani unafanana na sanamu isiyoweza kuongea, isiyoshika, isiyotembea, n.k

Sasa huwenda wewe hauna lengo baya kufanya hivyo, huwenda lengo lako ni kutaka kumsogelea Mungu kwa ukaribu, lakini njia unayoitumia siyo njia ya kiMungu.

Njia pekee ya kumfikia Mungu ni kupitia njia ya msalaba! 

Yaani kujikana nafsi na kubeba msalaba wako na kumfuata Yesu. Ambaye yeye pekee ndiye atatufikisha kwa Mungu, kama alivyosema katika..

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.

Unaona hapo, hatumfikii Mungu kupitia mtu yoyote, au sanamu ya mtakatifu Fulani au malaika yoyote, njia ni moja tu YESU KRISTO. Na vilevile hatumwombi Wala kumwabudu Mungu kupitia kitu chochote, au mtu yoyote ni Yesu peke yake ndiye mpatanishi kati yetu na Mungu.

1 Timotheo 2:5-6 Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;

[6]ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.

Bwana Yesu ndiye aliyeteswa na kusulubiwa kwa ajili yetu, ni Yeye pekee ndiye alikubali kuchukua dhambi za ulimwengu, alifanyika sadaka kwa ajili yetu, Mungu alimbebesha dhambi za ulimwengu mzima.

Isaya 53:5-7 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

[6]Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.

[7]Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.”

Hivyo kuanzia leo ondoa hayo mawazo ya kudhani utamfikia Mungu kwa njia zako tu, au kupitia dhehebu lako, au dini yako, au kupitia mtu fulani, au hata yule aliyetumika kumleta Mkombozi Yesu duniani yaani Mariamu, hapaswi kupewa heshima au kuabudiwa maana yeye alitumika tu kama chombo, na pia ondoa picha na sanamu zote za Yesu maana kufanya hivyo ni kujigandisha maisha yako ya kimwili na kiroho.

Yesu hatumwabudu kupitia rozari, au picha zake au sanamu yake. Tunamwabudu katika Roho na kweli, Kama biblia inavyotuagiza.

Yohana 4:24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Kumwabudu Mungu katika Roho na Kweli ni kumpokea Roho Mtakatifu ambaye huyo atatufushisha kumjua Mungu kwa undani kupitia Neno lake na pia atatusaidia kuishi maisha yampendezayo Mungu yaani maisha masafi ya utakatifu.

Na Roho Mtakatifu ni ahadi kwa kila mmoja atakayemwamini Mwana wa Mungu Yesu Kristo, na kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha kabisa na vilevile kubatizwa ubatizo sahihi.

Matendo ya Mitume 2:37 ”Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

[39]Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”

Kabla ya kufikiri kubadilisha kanisa, au dini fikiria kwanza kutubu dhambi zako zote na kuacha ulimwengu, fikiria kuacha uasherati, fikiria kuacha ulevi, uvaaji mbaya, usengenyaji, uhuni, na mambo yote mabaya ndiyo uanze kutafuta kanisa la kweli linalohubiri utakatifu wa nje na ndani na kubatiza ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. (Usiendelee kuabudu sanamu)

Kumbuka waabuduo sanamu sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, Biblia inasema hivyo.

Ufunuo wa Yohana 21:8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na HAO WAABUDUO SANAMU, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *