MPE MUNGU NAFASI YA KWANZA KATIKA MAISHA YAKO

Biblia kwa kina No Comments

MPE MUNGU NAFASI YA KWANZA KATIKA MAISHA YAKO

Jina kuu la Mwokozi Yesu libarikiwe.

Kama tunavyojua, Mungu wetu aliye juu mbinguni amejitambulisha kwetu kwa namna tofauti tofauti ili tuweze kumwelewa zaidi. Kwamfano anasema yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wakwanza na wamwisho. (Ufunuo 22:12)

Sasa ili tuweze kuelekea kiini cha somo letu, hebu tutazame hizi sifa kuu tatu za Mungu alivyojitambulisha kwetu.

ALFA NA OMEGA:

Tafsiri ya Alfa na Omega sio mwanzo na mwisho, kama inavyofahamika na wengi…ingekuwa ndiyo tafsiri yake hiyo, visingetenganishwa vitu vitatu hapo juu…Sasa Afla ni herufi ya kwanza kwenye alfabeti za Kingiriki..yenye alama hii (α) Na Omega ni herufi ya mwisho ya kwenye alfabeti za lugha ya kigiriki yenye alama hii (ω)…Kwenye alfabeti zetu sisi herufi ya kwanza ni (A) na ya mwisho ni (Z)….kwa kigiriki ya kwanza ndiyo hiyo alfa na ya mwisho ni omega.

Kwahiyo katika mstari huo aliposema yeye ni alfa na omega, alikuwa anajitambulisha uungu wake katika umbo la NENO. (Kumbuka hapo mwanzo kulikuwako Neno….naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa ni Mungu,…Vitu vyote vilifanyika kwa huyo wala pasipo yeye hakuna chochote kilichofanyika Yohana 1:1).

Kwahiyo akiwa katika Neno, yeye ndiye Neno la Kwanza na ndiye Neno la Mwisho, kwahiyo ili lijitambulishe lazima litumie Herufi kujitambulisha, (herufi ya kwanza na ya mwisho, alfa na Omega)…Kwanini hakutumia herufi ya A na Z?..ni kwasababu lugha zinazotumia alfabeti hizi kama vile kiingereza zilikuwa hazijazaliwa bado, na hata kama zingekuwa zimeshazaliwa bado zilikuwa ni lugha changa, kwani wakati Yohana anapewa haya maono lugha iliyokuwa kuu na uliyozungumzwa sehemu kubwa ya dunia ilikuwa ni kigiriki, hata lugha iliyotumika kuandika vitabu vingi vya agano jipya ni lugha hii, ndio maana yakatumika maneno ya kigiriki.

MWANZO NA MWISHO:

Sifa ya pili, Hapa Mungu anajitambulisha kwa umbo la MUDA….Kama alivyosema mahali Fulani yeye ni UPENDO, na sio yeye ana upendo…kadhalika hapa, anajitambulisha kuwa yeye ni MWANZO na sio yeye ana mwanzo!..halikadhalika yeye ndiye MWISHO, na sio yeye mwenye mwisho…yeye hana mwanzo na wala hana mwisho, kwasababu yeye ndio mwanzo wenyewe na ndio mwisho wenyewe. Ili uelewe vizuri hebu tafakari jambo hili: umewahi kuchunguza mwanzo wa magharibi ni upi? Au mwisho wa magharibi ni upi?…au mwanzo wa mashariki ni upi na mwisho wake ni upi?..utakuja kugundua kuwa mashariki haina mwanzo wake wala mwisho wake, vivyo hivyo na magharibi haina mwanzo wala haina mwisho, kwasababu mahali ulipo tayari panaweza kuwa ni mashariki ya mbali sana kwa sehemu nyingine halikadhalika panaweza kuwa ni magharibi ya mbali sana kutoka sehemu nyingine…kwahiyo hapo ulipo tayari ni mwanzo na mwisho wa magharibi na mashariki. Kuna mstari wanaouita kitaalamu IDL huo ndio wanasema umetenganisha mashariki na magharibi lakini kiuhalisia hakuna mstari pale…Wamebuni tu, ili kuwarahisishia kutimiza matakwa yao ya kijeografia, lakini hakuna mwanzo wa mashariki wala magharibi, ingawa kuna mashariki na magharibi..

Na ndio Mungu yupo hivyo hivyo, ingawa kuna kitu kinaitwa MWANZO na Mwisho, lakini yeye hana mwanzo, wala hana mwisho……kwasababu yeye pale alipo ndio mwanzo na ndio mwisho….Na kama vile tunavyozidi kuelekea sana mwisho wa mashariki ndivyo tunavyojikuta tunatokea mwanzo wa mashariki hiyo hiyo…kadhalika na Mungu…tunapodhani tunamjua sana na hivyo tumefika karibia na mwisho wa kumjua yeye…kumbe ndio tupo mwanzo wa kumjua yeye….Na pale tunapodhani yupo mbali sana na sisi kumbe ndio yupo karibu sana na sisi, na pale tudhaniapo kuwa tumemkaribia sana, kumbe bado sana tumfikie..Kwasababu yeye ndio mwanzo na ndio mwisho, akili zake hazichunguziki, wala hakuna mtu anayeweza kumwelezea asilimia mia na kusema sasa nimemjua Mungu.

Isaya 40:28 “Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele,Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zakehazichunguziki.”

WA KWANZA NA WA MWISHO:

Sifa ya tatu na ya mwisho, Hapa Mungu anajifunua na kujitambulisha katika umbo la mtu…Lile Neno lililojitambulisha kwa herufi alfa na Omega, sasa linavaa mwili na kujitambulisha kama Mtu, na kusema Yeye ni wa Kwanza na wa Mwisho.

Hapa anaelezea Uungu wake kabla ya vitu vyote..Yeye alikuwepo kabla ya kiumbe chochote kile…kabla ya Malaika na kitu kingine chochote…ndiye wa Kwanza, akaitoa sehemu ya roho yake akatuumba sisi wanadamu na malaika…Na hivyo sisi wote tumetoka kwake…Na mwisho wa siku tutarudi kwake..kwasababu yote yametoka kwake..

Sasa baada ya kufahamu ukuu wa Mungu wetu kwa sifa hizo, anasema anayepaswa kuabudiwa pekee yake ni yeye, anayepaswa kupewa nafasi ya kwanza ni yeye, anayepaswa kuhofiwa na kuheshimiwa zaidi ni yeye, anayepaswa kutangulizwa kwanza ni yeye ndiyo mambo mengine yafuate.

Mathayo 4:10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, UMWABUDU YEYE PEKE YAKE.

Lakini leo hii lipo kundi kubwa la watu wanaosema wameokoka na wanampenda Mungu, lakini ukienda ndani zaidi kuwachunguza, utafahamu kuwa wanachokisema hakiendani na ukweli wenyewe, kwa nje wanasema wanampenda Mungu lakini ndani yao kabisa wanamwabudu mungu mwingine. Na ndicho Kristo alichokisema pale katika..

Mathayo 15:8-9 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.

[9]Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.

Hivyo kama mkristo unayesema umeokoa na unampenda Mungu, angalia ni nini unakipa nafasi ya kwanza katika maisha yako. (Yaani katika moyo wako)

Yamkini ni mke wako au mume wako, au huwenda ni watoto, wazazi, marafiki, au ni elimu, kazi, n.k chochote kile ambacho kinachukua nafasi ya kwanza katika moyo wako kiasi kwamba ndio kinakupa furaha zaidi ya Yesu, ndio unakitegemea zaidi ya Yesu.. fahamu kuwa hicho kitu ndio mungu wako na huwezi ukamwabudu Mungu wa mbingu na nchi na wakati huo unatumikia miungu mingine. Anayepaswa kuabudiwa pekee yake ni Yesu Kristo, Ndiye Mungu Mkuu. (Tito 2:13), ndiye Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wakwanza na wamwisho.

Ukiona huwezi kujizuia kula masaa 24 kwa wiki..ili umwabudu Mungu katika kuomba, basi fahamu kuwa tumbo lako ndio mungu wako. (Soma Wafilipi 3:19), vilevile ukiona muda unaotoa kufanya shughuli zako ni kubwa kuliko muda unayotoa kwa Mungu, jiangalie sana. Mungu hataki kuwa wa pili, anataka awe wa kwanza kwa kila jambo kwasababu ndivyo alivyo.. yeye ni wakwanza siku zote.

Kwahiyo, angalia sana ni nini kinatawala moyo wako muda wowote. Ni nini unakidhamini Zaidi katika maisha yako?

Ni nini unachokiwaza wakati wowote?

Je! ni nani unamhofu na kumheshimu kuliko Mungu? Huwenda ni boss wako kiasi kwamba akikuambia uache ibada au uache utakatifu unaacha, au huwenda ni wazazi, au ni watoto wako unawaheshimu kiasi kwamba huwezi kuwaadhibu pale wanapoonyesha tabia mbaya. Eli aliwaheshimu watoto wake kuliko Mungu, akaacha kuwaadhibu pale walipokuwa wakifanya mambo yasiyompendeza Mungu ndani ya Hekalu la Mungu.

1 Samweli 2:27 “Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, BWANA asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao?

[28]Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa mbari ya baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto?

[29]Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; UKAWAHESHIMU WANAO KULIKO MIMI, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema?

[30]Kwa sababu hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa BWANA asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu.”

Umeona hapo, mwanao anaonyesha tabia kama hiyo halafu umwadhibu,.unawadekeza dekeza tu, hutaki waumie kwasababu ndio umewaweka kwenye moyo wako kuliko Mungu aliyekupa. Halafu unasema umeokoka na unampenda Mungu. (Huo ni unafiki na Mungu hataki unafiki)

Hebu leo ondoa hiyo nafasi ya watoto, mchumba, mke, mama, baba, bosi, shule, n.k ambayo umeweka yakwanza, toa na muweke Mungu kwenye hiyo nafasi na hao watu wengine na vitu vingine viwe na nafasi ya pili au ya tatu.

Marko 12:28 “…akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?

[29]Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;

[30]nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

Ikiwa bado hujaokoka, mpe Yesu maisha yako leo kwa kutoa moyo wako huko ulikoweka na dhamiria kuacha dhambi zote kabisa, kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na jina la Yesu Kristo. (Matendo 2:38). Kumbuka tunaishi ukingoni mwa siku za mwisho na wewe mwenyewe haujui mwisho wako ni lini! Hivyo saa ya wokovu ni sasa na wakati uliokubalika ni sasa.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *