
MTAFAKARINI SANA
Waebrania 12:3 ”Maana MTAFAKARINI SANA yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”.
Nakusalimu katika Jina kuu lipitalo majina yote mbinguni na duniani, jina Bwana Yesu Krosto. Karibu tujifunze Neno la Mungu kwa kina.
Tumeambiwa “TUMTAFAKARI SANA” huyu YESU tunayemtaja kila siku.
Huyu YESU sio wa kawaida kabisa kama wengi wanavyomchukulia. Na leo tutaangalia ni kwanini tunapaswa tumtafakari “sana” huyu mkuu wa uzima.. YESU KRISTO wa Nazarethi. Tumeambiwa tumtafakari lakini pia tumjue sana.
Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”;
Kumbuka biblia inaposema tumtafakari sana au tumjue sana, inamaanisha SANA kweli kweli na sio kidogo.
Huyu YESU tunayemjua sio wa kawaida kabisa, huyu ndiye mkuu wa uzima, ndiye mkuu wa wafalme wa dunia. (Ufunuo 1:5)
Huyu ndiye ambaye torati na manabii walitabiri juu yake. Tunasoma..
Yohana 1:43 Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate.
[44]Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro.
[45]Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.
Na yeye mwenyewe anajishuhudia kwamba ndiye aliyenenwa kweli na manabii. Tunasoma..
Luka 24:25 “Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!
[26]Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?
[27]Akaanza kutoka Musa na manabii wote, AKAWAELEZA KATIKA MAANDIKO YOTE mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.
[44]Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.
Sasa unajiuliza ni wapi ameandikiwa katika Torati na katika Zaburi na manabii. Hebu tumuone katika torati..
Tunasoma Kristo alifanyika laana kwa ajili yetu tuliokuwa katika laana kutokana na dhambi.
Tunasoma katika..
Wagalatia 3:12 “Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.
[13]Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa ALIFANYWA LAANA KWA AJILI YETU; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;
Ni wapi imeandikwa hivyo, Tusome..
Kumbukumbu la Torati 21:22 “Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe ukamtundika juu ya mti;
[23]mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi wako”.
Lakini pia ule mwamba uliotoa maji kule jangwani ulimfunua Yesu Kristo.
Hesabu 20:11 Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.
1Wakorintho 10:4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na MWAMBA ULE ULIKUWA NI KRISTO.
Yule nyoka aliyeinuliwa kule jangwani na Musa (Hesabu 21:8) alimfunua Yesu Kristo, na hapa Kristo mwenyewe anatufumbua macho kwamba yule nyoka alimwakilisha yeye..
Yohana 3:14 Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;
[15]ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.
Ile mana iliyoshushwa mbinguni wana wa Israeli wakala jangwani ni ufunuo wa Yesu Kristo soma Yohana 7:48-51, yule mwana-kondoo aliyechinjwa na Ibrahimu badala ya Isaka (Mwanzo 22:13) alikuwa anamfunua Yesu Kristo aliyechinjwa kwa ajili yetu sadaka ya dhambi zetu..(Isaya 53:7).
Hayo ni machache tu katika torati, lakini ni yeye aliyeandikiwa kila kitu katika torati yote hivyo usomapo biblia kuanzia mwanzo tazamia kumuona huyu mkuu wa uzima.
Na maisha yote ya Daudi ni ufunuo wa Yesu Kristo, hebu tutazame baadhi ya Zaburi za Daudi tumuone huyu mjumbe wa Agano jipya.
Zaburi 118:22 Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
[23]Neno hili limetoka kwa BWANA, Nalo ni ajabu machoni petu.
Kama tunavyojua jiwe hili ni mkuu wa uzima Yesu Kristo mwenyewe.
Luka 20:17 “Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni?
[18]Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; na ye yote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa.
Hebu tuangalie tukio la Bwana Yesu kukamatwa na kushuhudiwa uongo.
Daudi anasema..
‘‘Ee BWANA, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;
[12]Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi.” (Zab27:12). Haya maneno yalikuja kutimia kwa huyu aliyeandikiwa..
Marko 14:55 Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione.
[56]Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana.
[57]Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,
[58]Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.
[59]Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.
Tukio la mavazi ya Bwana Yesu kugawanywa na kupigiwa kura Soma Zaburi 22:18 na Luka 23:34.
Tukio la Yuda kumsaliti Bwana Yesu soma Zaburi 41:9 linganisha na Mathayo26:20-23 na Yohana 13:18.
Maneno aliyoyasema Daudi akisema “Mungu wangu, Mungu wangu” mbona umeniacha (Zaburi 22:1) alikuwa alikuwa anamfunua maisha ya Bwana Yesu ambaye naye alikuja kusema maneno hayo pale msalabani (Mathayo 27:46).
Bwana Yesu kukataliwa na ndugu zake (Marko 3:21 & Yohana 7:5) aliandikiwa katika maisha ya Daudi (Zaburi 69:8) soma pia maneno aliyoyasema Bwana Yesu ”wivu wa wa nyumba yako utanila” (Zaburi 69:9 na Yohana 2:17)
Zaburi yote ni maisha ya Bwana Yesu, ndiye aliyeandikiwa haya.
Na manabii wote walimuona na kumtabiri yeye. Tuangalie baadhi ya manabii waliomtabiri huyu mfalme wa wafalme.
》 Nabii Samweli aliandika habari za Bwana YESU!!..
1Samweli 2:1 “Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele”.
》 Na Nabii Isaya naye aliandika habari za mkuu wa uzima YESU,
Isaya 9:6 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani”
》 Pia Nabii Mika aliandika habari za YESU..
Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele”
》 Nabii Hosea naye hakuacha kumtaja YESU..
Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”.
Linganisha na Mathayo 2:14-15.
》 Na Yeremia naye alimzungumzia YESU KRISTO.
Yeremia 31:15 “BWANA asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako”
Linganisha na Mathayo 2:18.
》Na nabii Zekaria ni hivyo hivyo..
Zekaria 9:9 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda”.
Linganisha na Mathayo 21:5.
》 Bila kumsahau Danieli naye alimwona YESU
Danieli 7:13 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye.
14 Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa”.
》 Na malaki alimwona pia..
Malaki 3:1 “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi”
》 Nabii Yona naye ni hivyo hivyo aliandika habari za YESU..Soma Mathayo 12:40.
》 Nabii Ezekieli alieleza habari zake YESU…Soma Ezekieli 36:26-27 linganisha na Yohana 15:26.
》 Nabii Amos aliandika mahubiri yake YESU…Soma Amosi 8:9 linganisha na Mathayo 24:29.
》 Nabii Yoeli naye alizigusia kazi zake..
Soma Yoeli 2:28-32
》 Ayubu naye alimwona Soma Ayubu 19:25.
Na manabii wengine wote walimwona YESU kabla ya wakati na kuandika habari zake.
Hiyo ni kuonyesha jinsi huyu mkuu wa uzima YESU KRISTO alivyo kiini cha Imani, na kiini cha mambo yote.
Je! unamchukuliaje huyu mkuu wa mbingu na nchi ? Je! Unamchukulia tu kama Yesu wa dhehebu lako? Au unamchukulia tu kama Nabii Fulani, au Mtume aliyetumwa na mwenyezi Mungu, au ni mwana wa Mungu tu basi? Nataka nikuambie huyu siye yule tunayemdhania. Huyu ni chapa ya nafsi ya Mungu kabisa.
Waebrania 1:1,3 Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,
2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
[3]Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
[4]amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.
Soma tena..
Wakolosai 1:13 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
[15]naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.
[16]Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.
[17]Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.
[18]Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.
[19]Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae;
[20]na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
Waefeso 1:17 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;
[18]macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;
[19]na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;
[20]aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;
[21]juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;
[22]akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo
[23]ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.
Ndugu, huyu Yesu sio wa kawaida kabisa… tumtafakari kwa kina sana. Tumfakari mara mbili mbili..biblia yote inamhusu Yeye. Yule si mtu wa kawaida kabisa, ni Mungu yule!!, na sio Mungu tu bali ni Mungu mwenye nguvu, Mungu mkuu, Baba wa milele. (Isaya 9:6 & Tito 2:13)
Ndiye Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho (Ufunuo 22:13).
Ukimjua huyu mkuu wa uzima namna hii, kamwe hautakuwa na hofu ya kitu chochote, hautaogopa mashetani wala mchawi yoyote, hautaishi kwa mashaka ukimwamini na kuliishi Neno lake.
Hautatikiswa na kubangaishwa na sauti yoyote inayokutishia kuwa utakufa, kwani huyu ndiye anayemiliki walio hai na wafu (Warumi14:9)
Mtafakari sana, Mtafakari sana!!. Unapomfanyia dhihaka na kulitukana Jina lake kupitia matendo yako mtafakari sana, unapoishi maisha ya uvuguuvugu na kujiita mkristo jiangalie sana unaweza ukatoweka ghafla ukajikuta kuzimu.
Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.
[25]Angalieni msimkatae yeye anenaye. Maana ikiwa hawakuokoka wale waliomkataa yeye aliyewaonya juu ya nchi, zaidi sana hatutaokoka sisi tukijiepusha na yeye atuonyaye kutoka mbinguni;
Waebrania 3:1 “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, MTAFAKARINI SANA Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, YESU,
Maran atha (Na uje Bwana Yesu)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.