MTUMISHI WANGU AITWAYE CHIPUKIZI

Biblia kwa kina No Comments

MTUMISHI WANGU AITWAYE CHIPUKIZI

Zekaria 3:8 “Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako waketio mbele yako; maana hao ni watu walio ishara; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi.”

Huyu mtumishi aitwaye chipukizi ni nani?

Huyu sio mwingine zaidi ya Mwokozi wetu YESU KRISTO, ndiye aliyetabiriwa kutokea kama chipukizi katika shina la Yese.

Isaya 11:1 Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.

2]Na roho ya BWANA atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA;

[3]na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;

[4]bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.

[5]Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.

Hilo shina linalozungumziwa hapo si lingine Zaidi ya BWANA YESU KRISTO mwenyewe…Biblia inasema litatoka shina, ikiwa na maana kuwa ni kutoka katika mti uliokatwa, nalo litazaa sana matunda… Kama ulishawahi kuona mti mkubwa uliokatiwa chini kabisa..linakuwa linabaki tu kama gogo…halafu baada ya kipindi fulani unaona kitawi kidogo cha kijani kinajitokeza ubavuni mwa lile gogo, na kama hakitakatwa na chenyewe, baada ya kipindi fulani kitakuwa kikubwa na hatimaye kuwa tena mti mkubwa kama ulivyokuwa mwanzo…

Ndicho kilichotokea baada ya uzao wa Daudi (Yese) kukatwa na kupelekwa Babeli…ni sawa na mti uliokatwa…lakini chipukizi likatoka, katika uzao huo huo wa Daudi..

Kama ukisoma kitabu cha Wafalme, baada ya Daudi kufa, akafuata mwanawe Sulemani akawa mfalme kweli kulingana na ile Ahadi lakini naye pia akafa, na ikaendelea hivyo hivyo, kwa wajukuu na vitukuu vya Daudi, mpaka mfalme wa mwisho aliyetawala Yuda aliyeitwa Sedekia, ambaye alikuwa ni kitukuu cha 20 cha Daudi, huyu ndiye mfalme wa Mwisho kutawala Yuda, baada yake yeye, ndio Watu wakapelekwa Utumwani Babeli, hiyo ndiyo siku waliokatwa na waliporudi kukawa hakuna mfalme tena katika Israeli…vitukuu vya Daudi vilivyozaliwa baada ya Sedekia Mfalme wa Mwisho kufa, wakawa ni watu tu wa kawaida, kama watu wengine…

Ndio maana Yusufu baba yake Yesu alikuwa ni mtu wa kawaida tu maskini, ingawa alikuwa ni mwana wa kifalme…(Kwa urefu fuatilia ukoo huu wa Yesu kwenye kitabu cha Mathayo 1:1-17), laiti Israeli asingeasi na kupelekwa utumwani, Yusufu baba yake Yesu angekuwa mfalme wa Yuda, na Kristo angezaliwa huko…

Mtumishi wangu aitwaye chipukizi.

Bwana Yesu, Mwana wa Daudi, mzao wa kifalme, mwenye ahadi ya kifalme juu yake, alizaliwa huko Bethlehemu, alikuwa ni mfalme aliyetoka katika shina lililokatwa ndio maana utaona alizaliwa katika zizi la ng’ombe, familia ya kimaskini, laiti Yusufu baba yake angekuwa mfalme basi naye pia angezaliwa katika familia ya kifalme..Lakini kinyume chake alizaliwa katika ufalme uliokatwa…

Lakini maandiko yanatabiri, huyo atakuja kuwa mti mkubwa na utazaa sana matunda, na ufalme wake utaenea duniani kote…kipindi alichokuja miaka 2000 iliyopita, roho ya Bwana ilikuwa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana” Kwa hekima, na maarifa aliyoyabeba alituletea sisi Wokovu…ambao mpaka sasa tunanufaika nao…., Lakini katika utawala wa miaka 1000 ijayo, ndio tutamwona vizuri kama Mfalme, aliyeketi katika kiti cha Kifalme…katika wakati huo, yeye pamoja na sisi ambao sasa tumemwamini, tutatawala naye, sisi tutakuwa wafalme na yeye atakuwa kama Mfalme wa wafalme. Haleluya!!

Wakati huo Mamlaka yote ya kifalme atakuwa nayo yeye, utakuwa sio wakati wa wokovu tena bali wakati wa utawala, sasa hivi ndio tupo wakati wa wokovu, nyakati hizo zitakuwa ni nyakati za utawala mkuu wa Yesu Kristo. Dunia yote itajawa na kumcha Bwana, kutakuwa hakuna vurugu, kutakuwa na Amani isiyo ya kawaida..simba na kondoo watakaa pamoja na hawatadhuriana, mtoto atacheza na nyoka, na hakutakuwa na madhara yoyote.

Isaya 11.6 “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe.

8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.

10 Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu”.

Ufunuo 3:20 “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

21 YEYE ASHINDAYE, NITAMPA KUKETI PAMOJA NAMI KATIKA KITI CHANGU CHA ENZI, KAMA MIMI NILIVYOSHINDA NIKAKETI PAMOJA NA BABA YANGU KATIKA KITI CHAKE CHA ENZI.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”

Na pia alisema..

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.

15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.

16 Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. MIMI NDIMI NILIYE SHINA NA MZAO WA DAUDI, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.

17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”

Swali ni je! umemwamini ipasavyo na kumpokea kweli kweli?

Kama hujampa Yesu Kristo Maisha yako, jua umechelewa sana, lakini mlango bado hujafungwa ingia kabla mlango hujafungwa..mwisho wa mambo yote umekaribia, na Kristo yupo Mlangoni kurudi, atakaporudi nyakati hii ya mwisho atakuja kama mfalme na mtawala mkuu hatakuja tena kama mwokozi.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *