MWENYE HEKIMA ASIJISIFU KWASABABU YA HEKIMA YAKE.

Uncategorized No Comments

MWENYE HEKIMA ASIJISIFU KWASABABU YA HEKIMA YAKE.

Je! Unajisifia nini ndani ya moyo wako?

Jina la Bwana Yesu libarikiwe ndugu yangu..Karibu tuyatafakari kwa pamoja maneno ya uzima,

Maneno ya Mungu yanasema..

.. Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake;

[24]bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA,” (Yeremia 9:23-24)

Leo hii unaweza ukajisifu kwasababu ya nguvu ulizonazo, au kwasababu ya cheo, elimu, umaarufu, utajiri, uhodari, uzuri, karama, kipaji, au chochote kile ambacho kinakupa kujiona ni wa tofauti na watu wengine, lakini ni vizuri leo kufahamu kuwa ukiwa na kila kitu halafu ukakosa kumjua Mungu wa kweli, kujisifu kwako ni bure. Maana yake unajidanganya nafsi yako tu, mbele za Mungu we sio kitu kabisa.

Na kumbuka kumfahamu Mungu sio kujua kuwa Mungu yupo maana hakuna asilolijua hilo hata viumbe wengine wanajua, lakini BWANA anasema yeye ajisifuye na ajisifu kwasababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua mimi ni Bwana, NITENDAYE WEMA, na HUKUMU, na HAKI. Huko ndiko kumfahamu Mungu.

Swali ni lile lile, je unajisifu kwasababu ipi? Ni kwasababu ya kumfahamu Mungu wa kweli au kwasababu ya mambo mengine?

Huwenda kwa nje unamsifia Mungu na kuonyesha kumpenda lakini ndani unajisifu kwasababu ya mke wako mzuri, au mume wako, au cheo chako, au mali ulizonazo, au uhodari ulionao…kuwa na vitu hivyo sio vibaya lakini hatupaswi kujisifia au kujisifu kwasababu ya vitu hivyo, tunapaswa kujisifu kwasababu hii tu, kumjua Mungu wa kweli basi.

Kwasababu haitatufaidia kitu tukisifiwa au tukijisifu kwasababu ya vitu hivyo halafu tukaenda kupotea milele.

Itakufaidia nini leo hii ukisifiwa kwa umaarufu, ukuu, au we mwenyewe itakufaidia nini ukijisifu kwasababu ya mali ulizonazo, au cheo ulichonacho, uzuri wa mwili na huku roho yako ipo hatarini.

Naamani jemedari wa jeshi la Shamu alikuwa mtu mkubwa, mwenye kuheshimiwa, na alikuwa hodari wa vita, lakini alikuwa mwenye ukoma.

2Wafalme 5:1 Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; LAKINI ALIKUWA MWENYE UKOMA.

Zingatia hilo neno “lakini alikuwa mwenye ukoma”. Maana yake pamoja na kuwa na cheo kikubwa, pamoja na kuwa na heshima kubwa, pamoja na kuwa mtu hodari wa vita LAKINI ALIKUWA SIO KITU kwasababu alikuwa na ukoma. Hivyo vitu vyote alivyokuwanavyo havikumfaidia kitu, wala havikuweza kumuondolea huo ugonjwa wake haijalishi alikuwa na fedha kiasi gani.

Ukoma enzi za biblia ni ugonjwa uliojulikana kama pigo kuu kutoka kwa Mungu, kutokana na dhambi ambazo mtu alizozitenda.

Mtu aliyegundulika kuwa ana ukoma ilikuwa anatengwa na jamii nzima ya Israeli. Anapelekwa mahali ambapo wakoma wenzake walipo, mbali kidogo na makazi ya kawaida ya watu na haruhusiwi kuja kujichanganya na watu wengine asije akawaambukiza wale wasio na ugonjwa huo. Hata familia yake mwenyewe hakuruhusiwa kuisogelea, aliendelea kukaa huko huko, mbali kwa kipindi chote ambacho Mungu atamponya, na kama ikitokea hata ponywa basi maisha yake yote atakuwa ametengwa. Walawi 13.

Unaweza ukawa mtu mkubwa kama Naamani, ukawa ni mtu hodari, ukawa ni mtu wa kuheshimiwa, na ukasifiwa na ulimwengu kwa uzuri wako, uhodari wako, au ukajisifia moyoni mwako kwasababu ya maisha uliyonayo.. lakini pamoja na hayo yote, kama una ugojwa wa dhambi ndani yako, we sio kitu kabisa. Na vitu hivyo ulivyonavyo na kujisifu kwako kote ni bure na ni hasara kubwa.

Kwani vitu hivyo havitaweza kukoponya huo ugonjwa ulionao, usipotafuta kumfahamu Mungu wa kweli, utakufa na ugonjwa wako (dhambi) yako na utaenda kwenye jehanum ya moto.

Naamani alipohubiriwa injili na kujua kuwa yupo Mungu anayeponya..aliacha nchi yake, aliacha vyeo vyake, aliacha kiburi chake na kwenda kumtafuta Mungu wa Israeli.

Na baada ya kumfahamu Mungu wa kweli alikubali kuzamishwa kwenye maji na baada ya hapo alipona ugonjwa wake.. akawa mtu mpya.

2Wafalme 5:14 Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, AKAWA SAFI.

[15]Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; AKASEMA, SASA TAZAMA, NAJUA YA KWAMBA HAKUNA MUNGU DUNIANI MWOTE, ILA KATIKA ISRAELI; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.

Umeona hapo, Naamani baada kukubali kujishusha na kwenda kubatizwa kwa kuzamishwa kwenye yale maji, alitoka akiwa safi. Na akaanza kumsifia Mungu wa Israeli badala ya kusifia mambo mengine.

Hivyo na wewe ndugu unayesoma makala hii, Hebu jichunguze leo ndani yako hakuna ukoma kweli?

Ukoma ni dhambi ambayo haiwezi kutibika kwa dawa yoyote au kwa ushauri wowote isipokuwa kwa kumtafuta Mungu wa kweli na kutii maagizo yake kama alivyofanya Naamani.

Kumbuka ukisifiwa au ukijisifu kwa chochote kile na huku humjui wala humfahamu Mungu wa kweli, tayari huo ni ukoma ambayo inakutenga mbali na Mungu.. haijalishi wanadamu watakusifia kwa namna gani, au utajiona mkubwa, mwenye nguvu na wa maana sana, huko ni kujidanganya.

Mtu mkubwa, na hodari ni yule anayejisifu kwasababu ya kumfahamu Mungu kweli kweli, huyo ndiye mtu wa thamani na wa heshima mbele za Mungu. Hata kama anaonekana machoni pa wanadamu kuwa sio kitu, lakini kwa Mungu ni mtu hodari sana na mwenye utajiri mkuu kuzidi matajiri wote wa dunia.

Sasa tutamfahamuje Mungu wa kweli?

Kumfahamu Mungu wa kweli ni kumfahamu YESU KRISTO WA NAZARETHI, na kukaa ndani yake, huyo ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele, na tunapaswa kujisifu kwa kumfahamu yeye peke yake na wala sio kitu kingine.

1Yohana 5:20 Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. HUYU NDIYE MUNGU WA KWELI, NA UZIMA WA MILELE.” Haleluya.

Kwahiyo anza kujipambanua, je! upo ndani yake, na unajisifu kwa kumfahamu yeye, au unajisifia tu dhehebu lako, au Nabii wako au mchungaji wako, au mchumba wako? Unajisifu kwasababu ya nani? Au kwasababu ya nini?

Ikiwa moyo wako upo kwingineko…hebu leo ondoa huko na umpe huyu mkuu wa uzima Yesu Kristo, kwa maana yeye ndiye Mungu wa kweli.

Kubali kusarenda kwa Yesu leo kama Naamani aliposarenda kwa Elisha, kubali kutubu dhambi zako zote na kuacha njia zako mbaya za ulimwengu, kubali kuacha kiburi cha uzima na nenda kabatizwe kwa kuzamishwa katika maji mengi kama Naamani ili uoshwe huo ukoma wako/dhambi ambayo inakutenga mbali na utukufu wa Mungu. Baada ya hapo anza kuelekeza moyo wako wote kwa Kristo na ujisifu kwa kuwa ndani yake basi.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *