NA MWANAMKE YULE ALIKUWA AMEPABWA KWA DHAHABU.

Mwanamke No Comments

NA MWANAMKE YULE ALIKUWA AMEPABWA KWA DHAHABU.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Leo tutaangalia asili ya wanawake kujipamba ilitoka wapi na lengo la kujipamba ni lipi?

Katika nyakati hizi za mwisho wanawake wamezidi kupamba miili yao na hata kubadilisha kabisa mionekano yao Mungu aliyowaumbia.

Lakini wengi wao hawafahamu asili ya mapambo hayo yametoka wapi? Wanachokifahamu tu, ni kuwa wanafanya hivyo ili wapendeze zaidi, waonekane wanaenda na wakati, lakini hawajui chanzo cha matatizo yao mengi ni kutokana na hayo mapambo!! Hawajui kuwa chanzo cha mikosi, vifungo, ndoto mbaya n.k ni hayo mapambo waliyoweka kwenye miili yao!!

Lakini leo naamini baada ya kuujua ukweli huu, utaenda kufunguliwa, na wewe mwenyewe kama mwanamke wa kikiristo utaacha hayo mapambo kabisa bila kulazimishwa.

Biblia inatuonyesha asili ya mapambo imetoka kwa mwanamke huyu anayeitwa YEZEBELI. Hebu tuangalie huyu mwanamke ni nani, Na kwanini alikuwa anajipamba?

Yezebeli, alikuwa ni Binti wa Mfalme wa Wasidoni aliyeitwa Ethbaali (1 Wafalme 16:31). Sidoni ilikuwa ni nchi iliyokuwepo Kaskazini mwa Taifa la Israeli, kwasasa nchi hiyo ni nchi ya LEBANONI.

Desturi za Wasidoni zilikuwa ni kuabudu miungu, waliabudu mungu wao maarufu aliyeitwa BAALI.

Mfalme wa Israeli aliyeitwa Ahabu alimwoa Binti huyo wa kifalme na kumleta katika Taifa la Israeli na kuwa Malkia. Na hivyo kuingiza ibada za miungu migeni ndani ya Taifa la Mungu.

Yezebeli licha tu ya kulichafua Taifa la Israeli kwa kumshawishi sana Mumewe Ahabu, alikuwa pia ni mchawi (2 Wafalme 9:22). Aliwaua manabii wengi wa kweli wa Mungu, na aliikosesha Israeli kwa sehemu kubwa sana. Mahali pengine Inamtaja Yezebeli kuwa ni Nabii wa Uongo. (Ufunuo 2:20)

Lakini huyu mwanamke katika biblia nzima, ndiye mwanamke aliyeonekana kujipamba. Sio kwamba wengine hawakuwepo! hapana, walikuwepo wengi tu, kwani desturi ya makahaba ilikuwa ni lazima wajipambe ili wavutie wateja wao, na Yezebeli naye alikuwa miongoni mwa MAKAHABA. Lakini kwanini ametajwa katika biblia, kwasababu ndiye chanzo cha watu wa Mungu kufanya ukahaba (kujipamba).

Kwahiyo YEZEBELI alikuwa anajipamba kwa lengo la kuvutia ukahaba, tunasoma Yezebeli alipomwona YEHU anakuja, kwa tabia yake ya uzinzi, anaanza kujipaka uwanja machoni, na kupamba kichwa ili amlaghai YEHU apate kulala naye!. Na wala hata hakuwa na uchungu kwa kifo cha mwanae ambaye alikuwa amekufa, yeye anawaza uzinzi tu.

2Wafalme 9:30 “Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; AKATIA UWANJA MACHONI MWAKE, AKAPAMBA KICHWA CHAKE, akachungulia dirishani”

Na hata sasa, hii roho ya Yezebeli (kujipamba) bado ipo, na katika siku hizi za mwisho inafanya kazi sana, na lengo ni lile lile kuwafanya watu wa Mungu wazini.

Huoni hata watu leo wanaenda misibani wamejipodoa… mahali pa kwenda kutafakari mwisho wa safari ya mtu ulimwenguni, wengine wanaenda wamejipodoa kwa lengo la kuvutia ukahaba kama alivyofanya Yezebeli, katika msiba wa mwanae..

Roho hii imeingia mpaka makanisani, utaona wanawake na mabinti sehemu za ibada wanaingia kwa mionekano kama ya YEZEBELI, bila aibu wala hofu!..viungo vyao vipo wazi, nguo walizovaa ni za nusu tupu, nyuso zimejaa rangi, na vichwa vimepambwa kama Yezebeli, na hawaambiwi chochote, na wala wenyewe hawasikii chochote ndani yao kikiwahukumu… pasipo kujua kuwa hiyo ni roho ya YEZEBELI, inaishi na kutenda kazi, kama ilivyokuwa enzi za mfalme Ahabu.

Dada, Mama acha kupamba uso!!!, ndani na nje ya kanisa, hiyo ni roho ya YEZEBELI, ya Ukahaba…usidanganywe na shetani kwa kukuambia kuwa ni urembo tu.. ni urembo tu!!.. hakuna urembo ndani ya sare ya kikahaba.. Utavaaje sare ya askari na ukasema ni urembo tu!!..

Muachie Yezebeli mapambo yake yote maana yeye ndiye MAMA WA MAKAHABA MACHUKIZO YA NCHI.

Ufunuo wa Yohana 17:3 “Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

[4] NA MWANAMKE YULE ALIKUWA AMEVIKWA NGUO YA RANGI YA ZAMBARAU, NA NYEKUNDU, AMEPABWA KWA DHAHABU, NA KITO CHA THAMANI, NA LULU, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.

[5]Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.

[6]Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu.”

Biblia inasema mapambo ya wanawake wa kikiristo wanao ukiri uchaji wa Mungu ni utu wa moyoni usioonekana na sio kujipamba kwa mapambo hayo ya makahaba.

1Petro 3:1 Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;

[2]wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.

[3] KUJIPAMBA KWENU, KUSIWE KUJIPAMBA KWA NJE, YAANI, KUSUKA NYWELE; NA KUJITIA DHAHABU, NA KUVALIA MAVAZI;

[4]bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

[5]Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.

Jivue roho ya UYEZEBELI.. Mvae BWANA YESU (Warumi 13:14). Hizi ni siku za Mwisho na Bwana YESU anarudi.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *