NAJA KAMA MWIVI KESHENI

Siku za Mwisho No Comments

NAJA KAMA MWIVI KESHENI

Maandiko yanatufundisha kuwa Bwana YESU atakuja kama “Mwivi”..

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake)”

1Wathesalonike 5:1-3 Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

[2]Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

[3]Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

Mathayo 24:43-44 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

[44]Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

2 Petro 3:10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

Ndugu hayo maandiko yatoshe kukuaminisha kuwa Bwana anakuja kama Mwivi (mwizi)..

Na kama tunavyojua mwizi lengo lake ni kuiba vile vya thamani na si kingine!. Hivyo Bwana Yesu anakuja duniani kuiba vile vilivyo vya thamani na kuviacha vile visivyo vya thamani..

Kama vile mwizi ajavyo usiku, haji kuiba vitu vibaya bali vile vizuri vyenye thamani, ndivyo Bwana Yesu atakavyokuja kuiba watu wake (wale walio watakatifu na wenye thamani machoni pake) na kwenda nao mbinguni.

Kufumba na kufumbua, dunia itashaa tu watu fulani wametoweka katika mazingira ya kutatanisha!. siku hiyo hata shetani haijui.. ghafla atashangaa tu watu baadhi hawapo!

Luka 17:34 “Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

35 Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

36 Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa”

Je! Hiyo sio tabia ya mwizi??.. hebu jiulize unakaa na mwanao ndani, mmelala asubuhi unakuta hayupo na milango imefungwa kwa ndani vile vile, umekaa na mume wako ghafla unashagaa katoweka..upo kazini na mtu Fulani ambaye unamjua ni mtu anayejishughulisha sana na masuala ya wokovu, ghafla unashangaa hayupo!!!

Ndugu, Bwana Yesu kujifananisha na mwizi sio kwamba anakubaliana na wizi, Bali anataka tufahamu jinsi itakavyokuwa siku hiyo ya kuja kwake.

Kama tunavyofahamu wakati wa usiku kabla hatujalala, huwa ni lazima tufunge milango yetu yote, kwa makufuli na makomeo, na hii sio kwasababu tunapenda kujifungia tu hapana! bali ni kujiweka katika hali ya usalama dhidi ya WEZI usiku, Kwasababu hatujui ni wakati gani wataingia na kuleta madhara. Hii ni desturi kwa kila mtu,hakuna mtu asiyefahamu kuwa anapaswa kufunga milango yake wakati wa usiku.

Lakini pamoja na hayo kufunga mlango tu na kwenda kulala haitoshi, kwasababu mwizi anajua kabisa akienda atakutana na changamoto ya milango kufungwa hivyo atakuwa amekwisha jipanga kwa njia mbadala ili kuhakikisha kuwa zoezi lake la kuiba linafanikiwa kikamilifu, hivyo ni dhahiri kuwa atakuwa na vifaa husika vya kuvunjia nyumba.

Kwahiyo ili mwenye nyumba aweze kunusuru mali zake au roho yake sio tu KUBANA MILANGO yake bali anapaswa pia AKESHE, Kwasababu mwizi hawezi kuharibu kama mwenye nyumba yupo macho. Hivyo dawa pekee ya kudhibiti wizi usiku ni kubana milango pamoja na KUKESHA.

Ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Bwana Yesu Kristo,akifananisha kuja kwake na kama ujio wa mwizi wakati wa usiku alisema …

Mathayo 24:40-44″ Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;

41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni neno hili; KAMA MWENYE NYUMBA ANGALIIJUA ILE ZAMU MWIVI ATAKAYOKUJA, ANGALIKESHA, wala asingaliiacha nyumba yake KUVUNJWA. “

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa damu yuaja.

Tukisoma pia katika Marko 13:32 Bwana Yesu alisema maneno haya:

Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

33 Angalieni, KESHENI, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, KWAMBA NI JIONI, AU KWAMBA NI USIKU WA MANANE,au AWIKAPO JIMBI, au ASUBUHI;

36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, KESHENI. “

Kumbuka hapo Bwana Yesu hakusema “fungeni milango” bali alisema “kesheni” kwasababu inajulikana ni wajibu wa kila mtu kufunga milango yake, na kufunga milango ina maana kujiona umeokoka lakini maisha yako hayaendani na ukristo,umebatizwa na unaenda kanisani lakini umelala katika roho(vuguvugu), nje milango imefungwa lakini ndani umelala kwasababu hiyo basi mwizi atakapokuja hautajua lolote. Mkristo aliyeridhika na dhehebu lake au mapokeo yake lakini hazingatii mambo ya muhimu yanayohusiana na wokovu wake na maisha yake ya umilele ni sawa na mtu aliyejifungia na kulala usingizi.

Dunia sasa hivi ipo katika GIZA NENE SANA ikiashiria kwamba huu ni wakati wa USIKU na ndio wakati uliokaribia wa BWANA kurudi tena, kuongezeka kwa maovu ulimwenguni kama vile anasa,ulevi,uasherati uliokithiri hususani katika ulimwengu huu wa sasa wa utandawazi,mauaji,uchawi,rushwa,dhuluma, kupenda ulimwengu zaidi ya Mungu,n.k. vinawafanya watu wazidi KULALA usingizi wa mauti, na jinsi giza linavyozidi kuongezeka ndivyo wakristo nao wanavyozidi kushawishika kulala.

Sasa katikati ya kilele hichi cha maovu hapo ndipo Kristo atakaporudi, alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu watu walikuwa wakila na kunywa(ikiashiria kufanya anasa),walikuwa wakipanda na kujenga, hata siku ile ikawajilia kama ghafla, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu.

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) “.

MAANA YA KUKESHA NI NINI?

Kukesha kunakozungumziwa ni KUKESHA KATIKA ROHO, kutokulala katika roho, kudumu katika utakatifu kuishi kwa kuzisoma nyakati na kuyaelewa majira tunayoishi, kuishi kwa kukaa mbali na uasherati, ulevi, anasa, mavazi yasiyompendeza Mungu, matusi, rushwa, na mambo yote mabaya na kudumu katika kujifunza Neno la Mungu kila wakati. Hiyo ndio maana ya kukesha. Siku zinakuja hizi ni za hatari sana, huu ni wakati wa kukesha kweli kweli.

Maneno ya Mungu yaliyofunga kitabu cha biblia ni maneno ya Bwana Yesu na maneno hayo aliyoyasema ni haya..

Ufunuo 22:20 “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.

21 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.”

Maran atha (Na uje Bwana Yesu).

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *