Naomba kufahamu, je kuna ulazima wa kutoa fungu la kumi (zaka)?

Maswali ya Biblia No Comments

 

Bwana wetu Yesu Kristo Mwokozi wa ulimwengu Apewe sifa daima,

karibu katika darasa la maarifa ya kiMungu tujifunze biblia..Neno la Mungu wetu ambalo ndio mwanga wa njia zetu na taa ya miguu yetu  Zab 119:105..

Siku ya leo tutaenda kujifunza kwa ufupi kuhusu kutoa Zaka au fungu la kumi, Katika biblia Zaka ni sehemu ya kumi ya mapato ya mtu anayomtolea Mungu ni mojawapo ya aina ya Sadaka..

Kabla hatujaendelea mbele kujifunza zaidi kuhusu umuhimu wa kutoa Zaka, tupate kwanza historia kidogo ya Zaka au Fungu la 10,

Tukisoma Maandiko matakatifu tunaona Zaka kwa mara ya Kwanza ilitajwa kipindi ambacho Ibrahimu(Baba wa Imani) alikutana na Melkizedeki Kuhani Mkuu(ambaye tutakuja kumsoma habari zake mbele) baada Kutoka vitani kuwapiga maadui zake

Biblia inasema alipokutana..Ibrahimu alitoa fungu la kumi la vitu vyote..yaani ZAKA..kwahiyo mtu wa kwanza kutoa Zaka katika biblia ni Ibrahimu.. Habari hiyo tunaisoma katika kitabu..

Mwanzo 14:17 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme.

18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.

19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.

20 Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. ABRAMU AKAMPA FUNGU LA KUMI LA VITU VYOTE”.

Hapo tunaona Ibrahimu alimpa huyu Melkizedeki fungu la 10 la vitu vyote.
Sasa huyu Melkizedeki ni nani? alikuwa ni Mungu aliyekuja katika Mwili wa kibinadamu…ambaye pia alifahamika kama Kuhani Mkuu, mfano wa Yesu Kristo Mwana wa Mungu.. hana baba, wala mama, wala hana mwanzo wa siku wala mwisho wake. Kwahiyo Melkizedeki alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyemtokea Ibrahimu katika umbo la mwanadamu.

Abramu alipokuwa njiani akirudi kutoka kumsaidia Lutu ndugu yake ambaye alikuwa ameshikiliwa yeye pamoja na wanawe, njiani alikutana na huyu Melkizedeki ambaye alikuwa amebeba Divai na Mkate, akampatia Abramu na kwasababu Abramu alikuwa ni mtu aliyempenda Mungu sana, akaona si vyema kupokea tu bure hiyo Divai na huo mkate pasipo kurudisha shukurani yoyote…

Akiangalia Mungu alimshindia vita akawapiga maadui zake wote, kwahiyo akatambua kuwa haitakuwa busara endapo hatamrudishia Mungu chochote..ndipo akatoa fungu la 10 katika vitu vyake vyote pasipo kushauriwa au kuambiwa na mtu mwingine!!! Hakika huo ni moyo wa kipekee sana.

Abramu hakuambiwa na Mungu afanye hivyo…yeye mwenyewe ndani ya moyo wake aliona sababu ya kumtolea Mungu, alijihisi tu kuna kitu kinamsukuma atoe fungu la 10 katika vitu vyake..alijiona atakuwa na hatia akimwacha Mungu wake aondoke bila kuchukua chochote, hivyo kile kitu ambacho kilikuwa ndani yake ndio kilichomsukuma atoe mwenyewe pasipo kuambiwa na mtu yoyote hata Mungu mwenyewe hakumwambia..sasa hicho kitu si kingine zaidi ya Roho Mtakatifu.

Je kuna sheria yoyote Ibrahimu alifuata??

Sasa kumbuka kipindi hicho Mungu alikuwa bado hajatoa sheria yoyote, wala zile amri kumi hazikuwepo bado, Amri 10, na sheria, Mungu alikuja kutoa baadaye sana Wana wa Israeli walipotoka Misri baada ya miaka 430, Na moja ya sheria kati ya hizo ilikuwa ni pamoja na hiyo ya kutoa Zaka, Sheria hizo zilikuwa ni za lazima wala sio ombi..kama mtu hatatoa fungu la 10 atahesabiwa kuwa amekosa mbele za Mungu..na Mungu mwenyewe atamhesabu kuwa ni mwizi!. Soma Malaki 3:8-9″

Lakini sasa katika Agano jipya hatuishi tena kwa kuongozwa na sheria bali tunafanya mambo yote kwa Imani, na Imani hii sio nyingine zaidi ya ile ile aliokuanayo Ibrahimu, ile Imani ya kufanya mambo pasipo kuambiwa au kusukumwa sukumwa..

Kama Ibrahimu alivyotoa fungu la 10 la vitu vyake bila kushurutishwa na mtu.. ndivyo na sisi tunatakiwa tuwe na hiyo Imani ya kutoa bila masharti yoyote kwani Baba yetu wa Imani “Ibrahimu” alitoa pasipo masharti, wala sheria, wala torati kwamaana Torati yenyewe ilikuwa haijaja bado!. wala hakuna mtu aliyemshurutisha kutoa, hakusubiri kukumbushwa kumbushwa mara kwa mara au kuombwa, tena hakumwuuliza Mungu atoe au la! hakusikia mahubiri yoyote yanayohusiana na Zaka bali alitoa tu kwa Imani akijua anamtolea Mungu wake, aliyempigania na kumshindia vita katikati ya maadui zake, na zaidi alijua vitu vyote alivyonavyo alipewa na Mungu…

Kwa maana Mungu ni Mpaji(Yehova-YIRE) kwahiyo akatafakari jinsi Mungu alivyombariki mali zote hizo..akawaza kwanini asitoe sehemu ya kumi katika vitu hivyo ambavyo Mungu alimbarikia ili kumrudishia yeye shukuruni. Kwahiyo baada ya kutambua hilo akafanya kuwa sheria yake ya milele, akawa kila akipata ni lazima atenge fungu la 10 kwa ajili ya Mungu.

Ibrahimu(Baba wa Imani) alikutana na Melkizedeki na akampa fungu la 10 la vitu vyake vyote..hata leo bado Melkizedeki yupo na huyo si mwingine zaidi Yesu Kristo Bwana wetu, ndivyo biblia inavyoweka wazi hilo tukisoma katika…

Waebrania 6:20 “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki”.

Waebrania 7:1 “Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;

2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake mfalme wa amani;

3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.

4 Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara”.

Waebrania 5:5 Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

6 kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele kwa mfano wa Melkizedeki”.

Hapo tunaona Bwana Yesu anafananishwa na huyo Melkizedeki kuhani mkuu, maana yake ikiwa huyo Melkizedeki alistahili kupewa sehemu ya fungu la 10 na Ibrahimu.. ndivyo naye Kristo aliye Kuhani mkuu anastahili kupewa sehemu ya fungu la 10 kwasababu katika Agano jipya.. YESU KRISTO ndiye Melkizedeki wetu, na vilevile kama Ibrahimu alivyopiganiwa na huyo Melkizedeki.. ndivyo na sisi Bwana Yesu anatupigania leo,

Iwapo Ibrahimu hakusukumwa sukumwa kutoa fungu la 10, kama tu hakuna sheria yoyote iliyomshururisha kufanya hivyo, yeye mwenyewe alitoa bila kuhubiriwa na mtu yoyote, bila kupewa Ushauri na mtu mwingine au kuwekewa masharti yoyote, bali moyo wake mwenyewe ulimhimiza kufanya hivyo,..

Ndivyo na sisi leo tunatakiwa kumtolea Mungu sehemu ya fungu la 10 katika vitu vyetu bila kusomewa sheria yoyote, bila kuhubiriwa hubiriwa na kukumbushwa kumbushwa kila mara, tunatakiwa tutoe wenyewe ndani ya mioyo yetu si kama sheria bali ni wajibu wetu, Kwahiyo hatutasubiri kufuatwa na kuambiwa tutoe fungu la 10…

wewe mwenyewe unajua kama Mkristo ni wajibu wako kutoa fungu la 10 kwa Bwana wako Mfalme mkuu YESU KRISTO, hivyo usisubiri kushurutishwa kutoa Zaka ama fungu la 10, usisubiri kutangaziwa kanisani, usingojee kusikia mahubiri yanayohubiri kutoa Zaka, unapaswa kutoa mwenyewe pasipo masharti, wala kushauriwa na mtu,

Jifunze kwa Ibrahimu baba yetu mkuu, ni wajibu wa kila aliyeokoka yaani aliyempokea Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake,..ni wajibu wake kutoa Zaka kumtolea Bwana wake, tena kwa moyo wa dhati kabisa, si kwa ulazima,.. maana Mungu anatazama mioyo yetu, yeye hana shida na fedha ama mali zetu bali anataka azidi kutubariki hivyo toa kwa moyo wako wote.. usitoe tu ilimradi umetoa kwakuwa ni sheria, na pia kumbuka kutoa Zaka/fungu la 10 si kigezo cha wewe kukubaliwa na Mungu iwapo umekataa kutii maagizo yake,..

hutaki kusamehe, hutaki kuacha rushwa, kuacha usengenyaji, uongo, chuki, uasherati n.k, huku unakimbilia kutoa fungu la 10 ukijua Mungu atakupokea,..huo ni unafiki,.. Bwana Yesu mwenyewe alisema katika “Mathayo 23:23”

Inakupasa utoe fungu la 10 huku njia zako zinampendeza Mungu, unatii neno lake,..Neno la Mungu linaposema “Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume, na Mwanaume asivae mavazi ya mwanamke… katika ile kumbukumbu 22:5 hakikisha unalitii hilo neno..kwamaana hii mwanamke kuvaa suruali ni kwenda kinyume na neno la Mungu,..

na vilevile katika ile

1Timotheo2:9 Neno la Mungu linasema “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; SI KWA KUSUKA NYWELE, wala kwa DHAHABU na LULU, wala kwa nguo za thamani;

10 bali kwa matendo mema, kama iwapasasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”

Na pia katika

Walawi19:27 Neno la Mungu linasema “msinyoe denge(viduku) wala msiharibu pembe za vichwa vyenu” na maagizo mengine yote,..

je! unayatii? au wewe ni mwanamke unavaa masuruali, vimini, umesuka kila aina ya mitindo, na huku unakwenda kumtolea Mungu fungu la 10, ilikupasa kwanza ufanye kile neno la Mungu linakuagiza bila kuacha kutoa fungu la 10,

Na ukiona unapinga kutoa fungu la 10 na huku unaujua ukweli huo ni uthibitisho kuwa ROHO WA MUNGU hayupo ndani yako! Hiyo ni moja ya kiashirio kuwa bado ujampokea Roho Mtakatifu, maana mtu aliye na Roho Mtakatifu hawezi kupinga jambo kama hili,..kwani anakuwa na upendo kwa Mungu wake, hawezi kuacha kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya mali zake kama shukurani, akijua kuishi kwake ni miujiza..

kwani hata hajawahi kuambiwa alipie uhai wake, hakuna siku aliambiwa alipie ardhi anayoikanyaga, tena chakula anachokula hajui kimetokeaje tokeaje! pia akijua thamani ya Yesu Kristo aliyetoa uhai wake kwa ajili yake bila kulipia gharama yoyote..akijua hayo yote Kamwe haachi kumshukuru Mungu wake pindi anapobarikiwa kwa chochote,.. kinyume chake mtu asiye na Roho Mtakatifu hajui wala hafikirii hayo yote,..hana hata shukurani kidogo kwa Mungu anayempa pumzi yake bure, hathamini msalaba wa Yesu Kristo aliyekufa kwa ajili yake, Kwa ufupi hana upendo kabisa na Mungu..ndio huyo anayepinga kutoa fungu la 10, na utakuta anaendelea Kwenda kanisani, na Kwa kuwa hana Roho Mtakatifu..

Maisha yake yanakuwa ni ya dhambi tu, hafurahia kutii Neno la Mungu bali anafurahia dunia na tamaa zake,mtu huyu hana Roho Mtakatifu haijalishi anahudhuria kanisani siku zote, haijalishi anawasaidia maskini,…kama tu ni mtu asiyeishi Neno la Mungu asiyetaka kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya mapato yake,.ibada zake ni bure, hana Roho ambaye angeugua ndani yake na kumfanya atoe fungu la 10 bila masharti yoyote na kutii Neno la Mungu pia,

Hivyo Roho Mtakatifu ni muhimu sana.. maana pasipo yeye itakuwa ni vigumu sana mtu kumpendeza Mungu, itakuwa ni ngumu mtu kumtolea Mungu.. akisikia habari ya fungu la 10 utaumia, akisikia mahubiri yanayokemea dhambi hautafurahia, akiambiwa atoe sehemu ya fungu la 10 kwenye fedha zake ili injili ya Bwana iende mbele itakuwa ni ngumu sana kwake, sasa akiambiwa atoe maisha yake kwa ajili ya injili.. ni wazi hatakubali!. Iwapo tu kutoa fungu la 10 ni kazi kubwa…

Je atawezaje! Kuifia Imani!! mtu wa namna hii akisema ameokoka na anampenda Mungu anajidanganya mwenyewe wala kweli haimo ndani yake, maana kama tu kutoa Zaka ni ngumu.. mpaka afuatwe fuatwe, sasa atawezaje kuacha vyote na kumfuata Kristo!! atawezaje kutoa vyote alivyonavyo kumtolea Mungu kama yule mwanamke aliyetoa senti mbili na Bwana Yesu akamsifia, hebu wazia tu jambo hilo!

Kwahiyo fungu la 10 siyo kitu cha kuhitaji mjadala wa kutoa, siyo jambo la kuuliza uliza na kuhoji kuwa imeaandikwa wapi! Haitaji sheria, ni mtu mwenyewe kutoa kwa moyo wake wote kama Ibrahimu alivyotoa bila Sheria au Torati, labda kama huna kazi yoyote inayokuingizia kipato..hapo hauna lawama kwa Mungu, tofauti na hapo chochote unachokifanya na kupatia kipato..

hata kama ni kidogo toa fungu la 10 kwa Mungu wala sio sheria ila ni wajibu wako kumpa Mungu shukurani ukijua yeye ndiye anayekupa hata hicho kidogo, hata kama haufanyi kazi ila ukapewa zawadi fulani.. Mtolee Mungu fungu la 10 kwenye hiyo Zawadi, toa kabisa Kwa moyo si Kwa kushurutishwa, kwasababu Mungu wetu sio mkusanyaji wa mapato!. Anapendezwa tunapomtolea kwa moyo na kwa furaha, tukijua umuhimu wa kufanya hivyo kama vile alivyofanya Ibrahimu.

Swali la kujiuliza je! watu wasiotoa fungu la 10 wataenda Jehanum?

Ni vizuri kufahamu kitakachompeleka mtu jehanum sio jambo la kukataa kutoa fungu la 10, au matendo mengine mabaya kama uasherati, ulevi, wizi, matusi, n.k la hasha! bali kinachowapeleka watu wengi huko kuzimu ni kukosa kuwa na Roho Mtakatifu, ambapo matokeo ya kutokuwa na Roho Mtakatifu ndiyo hayo ya kutotoa Zaka, kuiba, kuzini, kufanya mambo machafu yote, Kwa ufupi hakuna jambo jema mtu asiye na Roho wa Mtakatifu atainufaisha ufalme wa Mungu,

Maana hata utoaji wake ni machukizo kwa Mungu, ni mtu mwenye vinyongo, asiyesamehe, ni kwasababu hana Roho Mtakatifu ambaye angeugua ndani yake na kumfanya achukie dhambi, achukie udunia, pia Roho Mtakatifu angeugua ndani yake pale anapoacha kumtolea Mungu, Kwahiyo hawezi kuacha kutoa fungu la 10, na mambo mengine mema kama kuwasaidia wengine na kuomba,

Kuna watu ambao wanajifariji kwa kusema maneno haya..kwamba utamsikia mtu akisema mimi ni mkamilifu kwa kila kitu isipokuwa ni fungu la 10 tu sitoi!.

Ukisikia hivyo.. ujue mtu huyo amedanganywa na uongo wa shetani, kwani ni vigumu mtu mkamilifu mwenye Roho Mtakatifu awe mkamilifu kwa mambo yote halafu fungu la 10 anashindwa kutoa.. jambo kama hilo halipo kabisa, iwapo mtu anaamua mwenyewe kutotoa fungu la 10 na huku ameshafahamu ukweli, basi mtu huyu akisema ni mkamilifu katika mambo mengine ni muongo, maana ni lazima kuna mambo mengine tu maovu anayafanya, ni sawasawa tu mtu aseme mimi ni Mtakatifu kwa mambo yote ila ni kusema tu uongo ndio nimeshindwa kuacha! au ni uasherati tu, au ni usengenyaji tu ndio ninao. hapo hakuna utakatifu..ni kujifariji tu kwa uongo!.

Kuwepo kwa dhambi Moja ni ishara ya kuwepo kwa dhambi zingine, ukimwona mtu anavaa mavazi yasiyo na heshima,(vimini, suruali kwa mwanamke, nguo za kubana,) ujue hawezi kukwepa kuwa na dhambi zingine kama uasherati, na kama ni muasherati pia atakuwa ni mwongo, asiyesamehe, mwenyewe vinyongo, wivu, tamaa mbaya, n.k hata kama hatazionesha moja Kwa moja kwa nje ila ndani ya moyo wake kumejaa visasi,chuki, tamaa, na kila aina uchafu, hivyo kwa kuitimisha kutokutoa fungu la 10 ni ishara ya kutokuwa na Roho Mtakatifu na

Neno la Mungu linasema katika

“Warumi 8:9” wote wasio na Roho hao sio wa Mungu, na iwapo sio Mungu amewakataa basi sehemu yao ni katika lile ziwa la moto.

Na tunampokea Roho Mtakatifu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi na ulimwengu na tamaa zake!. Kisha kubatizwa Kwa maji mengi na Kwa JINA LA BWANA YESU (Matendo 2:38)

Bwana atusaidie!

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *