NCHI YA GIZA KUU

Biblia kwa kina, Kuzimu No Comments

NCHI YA GIZA KUU

Shalom jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe daima.

Je! unaifahamu ile nchi ya giza kuu. Biblia inatuambia ipo nchi ya giza kuu! Hebu tuangalie ni nchi ya namna gani hii.

Ayubu 10:20-22 “Je! Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate ngaa kutuzwa moyo kidogo.

[21]Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena, Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu;

[22]NI NCHI YA GIZA KUU, KAMA GIZA LENYEWE LILIVYO; Ni nchi ya giza tupu, isiyo na matengezo ya mambo yo yote, Nchi ambayo nuru yake ni kama giza”.

Umeona hapo kuna nchi ya giza kuu, ambapo mtu akienda huko hatarudi tena. Bila shaka umeshafahamu hiyo ni nchi gani.

Ndugu Yangu fahamu kuwa kuzimu ni mahali pakubwa sana, ni nchi, ni ulimwengu mkubwa sana..huwenda ukubwa wa nchi hiyo ni zaidi ya mara 10 ya hii dunia yetu. Ndio maana biblia inataja kama “nchi”, nchi inayozungumziwa hapo sio taifa bali ni dunia.

Kuzimu ni dunia kubwa mno. Haishibi watu wala haitakaa ijae.

Mithali 27:20 “Kuzimu na Uharibifu havishibi;..”

Lakini pia hiyo nchi ina malango yake, huwenda kuna lango la wazinzi na waasherati, kuna lango la walevi, lango la wachawi, lango la watukanaji, lango la wasengenyaji n.k

Ayubu 38:17 Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu?

Kuzimu inafananishwa na GEREZA kubwa sana lenye Malango na makomeo yake..Soma (Isaya 38:10 na Ayubu 17:6) utalithibitisha hilo..Haisemi mlango au komeo tu kana kwamba ni mmoja mmoja, hapana Bali ma-lango, ma-komeo, Hii ikiwa na maana kuna kifungo, na magereza mengi tofauti tofauti kulingana na aina ya dhambi za watu. Kama ukifa leo katika dhambi basi lipo lango lako uliloandaliwa na watu wa aina yako katika gereza lenu Na huko sio kukaa tu, hapana kuna shida na mateso ya hali ya juu sana..Wote wanakaa huko wakisubiria siku ile ya hukumu wahukumiwe kisha ndio watupwe katika lile ziwa la moto. (Kumbuka ni nchi ya giza kuu).

Na gereza la juu kabisa ni lile la shetani na malaika zake, ambalo kwasasa wapo baadhi yao huko wamefungwa wakingojea kutupwa kwenye lile ziwa la moto siku ile ya mwisho itakapofika, japo wapo wengine baadhi yao duniani wakizunguka, ndio hawa wanaoiharibu dunia..

2Petro 2:4 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu”;

Halikadhalika pia kuna watu ambao wamewekewa sehemu yao katika hiyo nchi ya giza kuu, watu hawa biblia imewataja kuwa ni visima visivyo na maji.

2Petro 2:12-15,17 “Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao;

[13]Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;

[14]wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;

[15]wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;

[17]Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, AMBAO WEUSI WA GIZA NI AKIBA WALIYOWEKEWA.

Manabii wote wa uongo, wachungaji wa uongo, mitume wa uongo, waimbaji wa uongo, na wakristo wa uongo wana sehemu yao katika hiyo nchi.

Ikiwa leo unasikia injili na hutaki kutubu na kuacha uovu wako, hutaki kuacha kutazama pornography, hutaki kuacha kusikiliza miziki ya kizinzi, hutaki kuacha kujichua, hutaki kuacha kucheza magemu na kamari, hutaki kuacha kuvaa na kunyoa kihuni, wewe ni mwanamke hutaki kuacha kuvaa mavazi ya makahaba kama vimini, suruali, makaptula, na magauni ya kubana, hutaki kuacha kujipamba kwa mapambo ya akina Yezebeli, mawigi, mahereni, mekaups, lipusticks, kucha bandia n.k fahamu kuwa sehemu yako imekwisha andaliwa kule, na kila siku wengine kama wewe wanaingia humo.

Tubu sasa, mpe Yesu maisha yako ingali bado unayo nafasi. Kumbuka kule hakuna nafasi ya pili.

Waebrania 9:27 Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *