
Ni nini Mungu anachokiangalia kwanza tunapomtolea sadaka.
Watu wengi tunamtolea Mungu aidha kwa njia ya fungu la kumi au kwa njia nyingine yoyote ile tunayoijua ..lakini mara nyingi hatuoni faida ya kutoa na mwisho wa siku tunaishia kuona kuwa Mungu hajibu au anajibu tu watu fulani.
Ukweli ni kwamba Mungu huwa anajibu mapema sana bila upendeleo, ikiwa tumemtolea kwa moyo na sio kwa mazoea au kulazimishwa.
Sadaka huwa inanena mbele za Mungu (inazungumza). Na kadri tunavyozidi kutoa kwa kupenda ndivyo sauti ya sadaka yako inazidi kuwa kubwa masikioni mwa Mungu, hivyo ni lazima tu Mungu akujibu, anaweza asikujibu siku hiyo hiyo, lakini atakujibu tu.
Lakini majibu ya Mungu yanaweza kuwa tofauti na matarajio yetu, na hapa ndipo watu wengi wanapopishana na baraka za Mungu.
Mungu anapoangalia sadaka zako na mahitaji uliyoambatanisha nayo, kwa sababu yeye ni upendo na anatupenda, huwa cha kwanza ambacho anaipa kipaumbele, kwanza ni kuhusu hali zetu za kiroho, kwasababu roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu, na tena mwili utakufa lakini roho itaishi milele.. hivyo haitatufaidia kitu tukipata vyote vya mwilini halafu tukapata hasara ya roho zetu.
Kwahiyo kama upo nje ya wokovu (hujampokea Yesu), na unamtolea Mungu kwa moyo wa upendo, fahamu kuwa huwenda Mungu alishakujibu kwa kukuletea watumishi wake waliokuja kukuhuburia uokoke, au leo anakujibu kupitia njia hii. Kwasababu kweli Mungu atakutimizia mahitaji yako yote ya mwilini kama ulivyoomba, lakini anataka kwanza umpokee Yesu yaani uokoke.
Ndicho alichokifanya kwa Kornelio na nyumba yake na hata sasa hajabadilika, ni yeye yule jana na leo na hata milele. Hebu tusome hii habari kwa umakini (soma habari yote usiruke-ruke)
Matendo ya Mitume 10:1 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,
[2]mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, NAYE ALIKUWA AKIWAPA WATU SADAKA NYINGI, NA KUMWOMBA MUNGU DAIMA.
[3]Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!
[4]Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, SALA ZAKO NA SADAKA ZAKO ZIMEFIKA JUU NA KUWA UKUMBUSHO MBELE ZA MUNGU.
[5]Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.
[6]Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.
[7]Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima;
[8]na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.
[9]Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;
[10]akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia,
[11]akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi;
[12]ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani.
[13]Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.
[14]Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi.
[15]Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.
[16]Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.
[17]Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango,
[18]wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
[19]Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta.
[20]Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.
[21]Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani?
[22]Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako.
[23]Akawakaribisha wawe wageni wake.
Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.
[24]Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake.
[25]Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia.
[26]Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.
[27]Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika.
[28]Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.
[29]Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?
[30]Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing’arazo,
[31]akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.
[32]Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.
[33]Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.
[34]Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;
[35]bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.
[44]Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.
[45]Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
[46]Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,
[47]Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?
[48]Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”.

Huyu Kornelio alikuwa akitoa sadaka nyingi, na sadaka zake zilikuwa zinanena mbele za Mungu kumkukumbusha Mungu atazame na ajibu maombi yake. Lakini hapa tunaona malaika wa Mungu akimjia na majibu kutoka kwa Mungu na kumwambia..
“..sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
[5] SASA BASI, PELEKA WATU YAFA, UKAMWITE SIMONI, AITWAYE PETRO.
[6]Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, ATAKUAMBIA YAKUPASAYO KUTENDA”.
Unaona hapo, pengine huyu Kornelio alipotokewa na malaika alijua labda zile sala zake za kuomba kupandishwa cheo, Mungu amejibu, pengine alijua malaika wa Mungu alimletea habari ya kuinuliwa kiuchumi, lakini malaika wa Bwana alimwambia “atume watu Yafa kumuita Petro mtumishi wa Mungu, aje kumhubiria habari za Yesu Kristo, atubu na kumpokea halafu mambo mengine yafuate.” Hiyo ndiyo ilikuwa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu.”
Na hata sasa, anachokiangalia Mungu kwanza tunapomtolea sadaka zetu, si kutupa majumba na maghorofa au kutuhudumia mahitaji yetu ya mwilini bali ni kutuponya kwanza roho zetu, yaani kutupa wokovu ambao unapatikana kupitia mwanae mpendwa Yesu.
Lakini wengi wetu huwa tunapishana na hayo majibu kutoka kwa Mungu, na tunabaki kunung’unika na kulalamika kuwa Mungu hajibu maombi, haangalii sadaka zetu, na kumbe zile sadaka tunazozitoa huwa zinakwenda kunena na kumkukumbusha Mungu juu ya mahitaji yetu, lakini sasa Mungu akituangalia anaona kuna kitu tumepungukiwa ambacho ni zaidi ya mahitaji tunayoyataka, na kitu hicho ni wokovu.
Tunaweza tukajidanganya kuwa tumeokoka, lakini Mungu akiangalia anaona uchungu ndani yetu, anaona wivu, hasira, majivuno, kiburi, tamaa mbaya, uzinzi, mawazo mabaya, na mambo mengine mabaya..sasa kwa hali hiyo bado hatujaokoka, haijalishi tutakiri mara mia kuwa tumeokoka. (Hatuwezi kumdaganya Mungu).
Kwahiyo Mungu anachokifanya kwanza ni kutuletea watumishi wake wa kweli atuhubirie ili tuokoke halafu baada ya hapo ndipo ataachilia baraka zake juu yetu.
Kwahiyo leo hebu anza kujitafakari, zile sadaka ambazo umekuwa ukitoa na hauoni majibu, wala kujibiwa mahitaji zako, hebu angalia kwanza mahusiano yako na Mungu yakoje? Je! umeokoka kweli kweli?
Kumbuka Kornelio alikuwa ni mtu anayefanya matendo mengi mazuri ya kumpendeza Mungu, alikuwa anashika sheria za Mungu wa Israeli..lakini alikuwa hajamjua Yesu wala kumpokea. Unaweza ukawa ni mtu wa kidini, ukawa na dhehebu kubwa au dogo, ukafanya matendo mema ya kumpendeza Mungu na wanadamu lakini kama hauna Roho Mtakatifu bado hujaokoka. Hivyo yale matendo yako mema na sadaka zako na sala zako zote zinalia mbele za Mungu ili Mungu akupe neema ya wokovu na sio ukuinue kiuchumi au akuponye mwili halafu mwisho ukaangamie motoni.
Na hakuna njia nyingine ya kupokea wokovu isipokuwa ni kusikia injili ya kweli na kutubu dhambi, hivyo yule mtumishi aliyekuja kwako akuhubirie habari za wokovu.. fahamu kuwa ni matokeo ya sadaka zako.
Unaposikia mahali popote aidha mtandaoni au mitaani, au masokoni, au barabarani injili inayokuchoma moyo wako na kukuhuzunisha fahamu kuwa ni majibu ya Mungu baada ya sadaka zako kufika na kuwa ukumbusho mbele zake.
Huwenda ulikuwa unaomba Mungu kwa muda mrefu akuponye afya yako na umekuwa ukitoa sadaka nyingi lakini leo kumbuka yale mahubiri uliyowahi kusikia yakihubiri kuwa “chanzo cha mambo yote ni dhambi,” Chanzo cha magonjwa ni dhambi, chanzo cha kifo ni dhambi n.k… huwenda siku uliposikia mafundisho hayo ambayo yalikuchoma moyo wako, uliposikia kwamba unapaswa utubu kwa kumaanisha kuacha dhambi kabisa, ukabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo upate ondoleo la dhambi zako, na umwishie Mungu katika maisha ya utakatifu, na kwamba ukifanya hivyo hakutakuwa na jambo lolote au mlima wowote utakaosimama mbele yako, ulipuuzia, hukutaka kuchukua hatua… lakini leo Bwana amekujia tena kwa njia hii, nataka nikuambie leo ukiamua kumpa Yesu maisha yako kwa kumaanisha kutubu na kuacha dhambi na ulimwengu kabisa ukaenda kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Yesu.. nataka nikuambie huo ugonjwa sugu na kila tatizo utasahau katika yake maji.
Hivyo ndugu isikie sauti ya Mungu leo inayozungumza na wewe sasahivi, unataka kwenda katika unyakuo?? Tubu! dhambi zako ukaoshwe kwa damu ya Yesu, na kuishi maisha matakatifu. Unataka kuponywa?? Acha dhambi!.. unataka kufunguliwa?? Acha uasherati!!, acha kutazama Pornography, acha ulevi, acha sigara, acha usengenyaji, acha wizi, acha rushwa, acha uvaaji mbovu kama wanawake wa kidunia,..Acha kutazama vitu visivyokuwa na faida yoyote katika maisha yako ya kiroho, tafuta ubatizo sahihi na ujazo wa Roho Mtakatifu.
Na Bwana atakubariki na kukuzidishia tele baraka zake.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.