NI TUMAINI GANI HILI UNALOLITUMAINIA?

Uncategorized No Comments

NI TUMAINI GANI HILI UNALOLITUMAINIA?

Jina la mwokozi wetu YESU KRISTO lisifiwe daima, Nakukaribisha ndugu mpendwa tujifunze maandiko.

Ikiwa kama mkristo fahamu kuwa kuna wakati watu wanaokuzunguka watataka kujua ni tumaini gani unalolitumainia mpaka unaishi maisha ya kujiamini namna hiyo.

Ukiletewa habari ya ugojwa mpya uliozuka hauogopi!, huna hofu na wachawi wala majini, hata hauogopi kufa! Ni tumaini gani unalolitumainia?

Ndivyo Hezekia alivyoambiwa na wale wajumbe kutoka Ashuru, baada ya Hezekia kukataa kujisalimisha kwa mfalme wa Ashuru kama walivyofanya wengine.

2Wafalme 18:17-20 Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na amiri wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.

[18]Na walipokwisha kumwita mfalme, wakatokewa na Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.

[19]Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kusema, Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, NI TUMAINI GANI HILI UNALOLITUMAINIA?

[20]Wewe wasema, lakini ni maneno yasiyo na maana, kwamba, Lipo shauri na zipo nguvu kwa vita hivi. Basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?

Kama kweli umeokoka kweli kweli, na unaishi kama mwana wa Mungu, itafika wakati wale watu wanaokuzunguka watavutiwa kujua nini hasa sababu ya wewe kuwa hivyo. Japokuwa hauna jina kubwa, hauna cheo kikubwa, unapitia kwenye dhiki na mateso na shida, ndugu na marafiki wamekutenga.. lakini bado upo na msimamo wako..Nini hasaa unakitazamia?.

Upitiapo hali kama hiyo usiogope kujibu na kuwaambia juu ya tumaini lako ambalo unalitumainia kuwa ni huyu Mkuu wa Uzima na Mkuu wa Wafalme wa dunia YESU KRISTO TUMAINI LA UTUKUFU (Wakolosai 1:27).

Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” (1Petro 3:15)

Usiogope kuwaeleza habari za TUMAINI lililo ndani yako..

Kwamba ule uzuri uliowekewa mbele yako, na ufalme ambao upo karibuni kufunuliwa na wewe ukiwa kama mfalme na kuhani, pamoja na kiongozi wako mkuu Yesu KRISTO, kama MFALME wa Wafalme, ndio sababu inayokufanya uishi kama ulivyo, ukae mbali na dhambi na matendo yote ya giza, usione kama hizo dhiki na mateso ni kitu kikubwa katika maisha yako kulinganisha na tumaini lilipo mbele yao.(1Petro 2:9)

Ndio maana umeacha kujipodoa na kujipamba kama wakina Yezebeli wasio na matumaini, ndio maana umeacha kuvaa vimini, makuptula na masuruali kama wanawake wa kidunia wasiokuwa na dira, Ndio maana umeamua kuacha vyote kwasababu ya hili TUMAINI LA UTUKUFU.

Embu jaribu kufikiria huyo mtu akisikia hivyo ataachaje kubadilika.

Hivyo ndivyo mkristo anapaswa kuishi, ili watu walio na mahangaiko, wenye hofu ya maisha na mizigo ya dhambi wakituuliza je! Mbona nyinyi mpo hivi na bado maisha yenu ni ya amani.. Nasi ndipo tuwaeleze TUMAINI lililo ndani yetu habari za YESU KRISTO…kwa upole na hofu, sio kwa kuwatisha hapana bali kwa upole na hofu biblia inatuambia hivyo. Na mwisho tutajikuta wengi wanavutiwa na TUMAINI hilo..Lililo la kweli.

Wafilipi 3:1 “Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana….”

4 Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.

5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. BWANA YU KARIBU.

6 Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.

7 Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.(Wafilipi 4:4-7)

Amen.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *