Nini maana ya Mhubiri 11:3b
Mhubiri 11:3 Mawingu yakiwa yamejaa mvua, Yataimimina juu ya nchi; NA MTI UKIANGUKA KUELEKEA KUSINI, AU KASKAZINI, PAANGUKAPO ULE MTI, PAPO HAPO UTALALA.
Swali nini maana ya maneno haya, mti ukianguka kuelekea kusini au kaskazini Paangukapo ule mti papo hapo utalala?
Kwanza kabla hatujapata maana ya maneno hayo, hebu kwanza tuone mti unawakilisha nini kibiblia.
Danieli 4:19 Ndipo Danieli, aliyeitwa jina lake Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akajibu akasema, Ee Belteshaza, ndoto ile isikufadhaishe wala tafsiri yake. Belteshaza akajibu, akasema, Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako.
[20]ULE MTI uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote;
[21]ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa kondeni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake;
[22] NI WEWE, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia.
Umeona tafsiri ya mti kibiblia, ooh kumbe mti unawakilisha mtu!
Ndiyo mti unawakilisha mtu, na ndio maana Bwana Yesu anajulikana kama shina la Daudi au shina la Yese, maana yake Daudi ni mti na Bwana ni shina lililochipuka baada ya ule mti kukatwa.
Isaya 11:1-3 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.
[2]Na roho ya BWANA atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA;
[3]na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake”;
Ufunuo wa Yohana 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. MIMI NDIMI NILIYE SHINA na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi”.
Sasa baada ya kuona maana ya mti kuwa inawakilisha mtu, biblia inasema..
Mhubiri 3″….Na mti ukianguka kuelekea kusini au Kaskasini Paangukapo ule mti papo hapo utalala.”
Maana yake nini?
Maana yake ni hii, mtu akianguka, iwapo ameangukia kusini au Kaskasini, huko huko alikoangukia ndiko utalala daima.
Kama tunavyojua kwa kawaida mti huwa ukianguka aidha kwa kukatwa au kung’olewa, ukianguka hauamki tena wenyewe, ni sawa na mtu akifa, haamki tena, biashara yake itakuwa imeisha.
Kwahiyo biblia inavyosema mti ukianguka hauamki tena, unamaanisha mtu akifa haamki tena, na iwapo ameangukia uzimani ni huko huko milele, Kadhalika kama ameangukia mautini ni huko huko atalalia milele.
Hii ikiwa na maana kuwa baada ya kufa hakuna mageuzi tena, hali uliyoondokanayo ndiyo itakupa picha kuwa wewe umeangukia wapi, kusini au Kaskasini, peponi au jehanum. Na kama vile mti ukianguka kuelekea kusini au Kaskasini, Paangukapo ule mti papo hapo utalala, ndivyo itakavyokuwa pia kwako na kwangu pia.
Kumbuka ipo mauti ya kiroho, ambayo hiyo inakuja baada ya mtu kusikia injili sana na kukataa kutii na kugeuka, huwa neema inaondolewa kwa huyo mtu, na huko ndiko kufa kiroho, unakuwa unaishi lakini umekufa kwa habari ya kuokoka, hata ukihubiriwa injili kwa namna gani huwezi tena kuokoka..maana wokovu ni neema na hiyo neema imeondoka juu yako,
Kama ulikuwa mlevi, au muasherati, au msengenyaji, ukianguka, ukifa katika hiyo hali..moja kwa moja habari yako itakuwa imeishia hapo .. huwezi tena kugeuka.. utaendelea kubaki hivyo hivyo mlevi, mwizi, mtukanaji, mzinzi mpaka siku unashuka shimoni (kuzimu).
Neema huwa haipo siku zote, inakuja na kuondoka, na kila mtu kapewa muda wake wa kuzaa matunda (yaani kutubu na kutii injili), hebu tusome huu mfano ..utaelewa vizuri,
Luka 13:6 Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; AKAENDA AKITAFUTA MATUNDA JUU YAKE, ASIPATE.
[7]Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, TAZAMA, MIAKA MITATU hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?
[8]Akajibu akamwambia, Bwana, UUACHE MWAKA HUU nao, hata niupalilie, niutilie samadi;
[9]nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.
Umeelewa hapo, huyo mti ulipewa miaka mitatu ya kuzaa matunda halafu haukuzaa, lakini kwa huruma akaongezewa mwaka mmoja tena ili asikatwe.
Yamkini wewe leo hii pengine ni zaidi ya miaka mitatu umekuwa ukisikia injili inayohubiriwa kwako kila siku kupitia makala hizi, au huko barababarani, masokoni, kanisani, n.k lakini bado huzai matunda yapasayo toba.
Ndugu, fahamu kuwa upo hatarini sana kukatwa, yawezekana upo kwenye muda wa nyongeza ambayo pengine ni mwezi mmoja, au mwaka umepewa ili utubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha kabisa.
Kumbuka ukikatwa, hautakuwa tena nafasi ya kutubu, wala kugeuka..maandiko yanasema baada ya kufa ni hukumu (waebrania 9:27)
Hivyo, huu ni wakati wako sasa wa kumgeukia Bwana Yesu kwa moyo wako wote pasipo kusita sita.. kwamaana..
“..shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. (Mathayo 3:10)
Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi.
Kumbuka hata kama unaendaga kanisani na una nafasi ndani ya kanisa..haimanishi ndio umempa Yesu maisha yako, we mwenyewe unafahamu kabisa kuwa bado unahitaji kutubu, hivyo ni vyema leo ukafanya toba ya kweli.
Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwake, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa..
Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..
Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.
Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Hongera kwa kuokoka.
Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.