NITAWALEMEA NINYI KAMA GARI LILEMEAVYO LILILOJAA MIGANDA
Amosi 2:13 Tazameni, nitawalemea ninyi, Kama gari lilemeavyo lililojaa miganda.
[14]Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake;
[15]Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake;
[16]Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa Atakimbia uchi siku ile, asema BWANA.
Je! umewahi kutafakari kwa kina ile siku kuu ya Bwana inayotisha?
Kuna siku kali ya Bwana inayokuja hapo mbeleni, kulingana na unabii wa Sefania siku ile ni siku ya..
Siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu,Siku ya tarumbeta na ya kamsa, (Sefania 1:15-16)
Pia siku hiyo kuu ya Bwana inajulikana kama siku ya kuogovya, na pia ni siku ya mapatilizo
Malaki 4:5 Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na KUOGOVYA.
Katika siku hiyo..biblia inasema milima itakimbia na visiwa kuhama (Ufunuo 16:20)
Ni siku ya maombolezo makuu kwa wale watakaokuwepo katika siku hiyo, kumbuka hiyo siku ya hasira na ghadhabu ya Mungu..haitakuwa siku kama siku moja, bali ni kipindi cha kama siku 30 kulingana na biblia, ambacho ghadhabu ya Mungu itamiminwa juu ya wanadamu wote waliokataa neema ya wokovu unaopatikana sasa bure kupitia kumwamini Yesu Kristo mwokozi wa ulimwengu.
Katika siku hiyo.. wafalme wa dunia na wakuu na majemedari watakuwa wakilia kwa uchungu mwingi na kukimbilia kujificha chini ya milima na kuiambia milima itusitiri wasipate msaada.
Ufunuo wa Yohana 6:15 Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,
[16]wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.
[17]Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?
Siku hiyo ni kuu sana, hakuna shujaa wala Jemedari wa vita atakayeweza kusimama, kwani aliye na moyo mkuu miongoni mwa mashujaa, atakimbia uchi siku ile (Amosi 2:16)
Ni siku ambayo Bwana Mungu atalipisa kisasi juu ya waovu wote, Bwana alisema ni siku za mapatilizo.
Luka 21:22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.
Katika siku hizo.. wanadamu wataadimika kuliko dhahabu safi, si ajabu taifa lako likabaki watu kumi tu.
Isaya 13:9 Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.
[10]Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.
[11]Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;
[12]NITAFANYA WANADAMU KUADIMIKA KULIKO DHAHABU SAFI, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.
Tafakari hilo neno ”KULIKO” sio kama!.
Je! unatamani hiyo siku kali na ya kuogovya?Biblia inasema..
Amosi 5:18 Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwani kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru.
[19]Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.
[20]Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.
Kuna watu wanaoitamani hiyo siku kuu ya Bwana, hawa ni watu ambao kila siku wanaimba midomoni mwao wakisema siku ya Bwana, siku ya Bwana inakuja, watu hawa sio wapagani wasiomjua kabisa Mungu, ni watu wa kidini, wenye majina ya kikirsto lakini Kristo hawatambui, kwanini? Ni kwasababu hawafanyi mapenzi yake. (hawaishi utakatifu, hawaliishi Neno la Mungu), ni watu ambao mioyo yao imeshikamana na dunia, ni watu ambao wamekinai Neno la Mungu na kujiona kuwa wamehitimu,
Lakini wanahubiri kuwa Kristo amekaribia na siku ya Bwana i karibu ilihali hiyo siku yenyewe hawajafunuliwa na Roho wakajua uzito wake…Kwamba sio siku ya kusemea kwa vicheko, ndio maana wanaihubiri huku wakiangua kicheko madhabahuni na kwa kujikinai. Hawa ndio wanaoitamani hiyo siku kuu ya Bwana.
Kwani kuitamani siku ya BWANA, Ni giza, wala si nuru.
Ndugu yangu, hebu itafakari tena kwa upya hiyo siku ya Bwana, hebu kaa kwa utulivu soma biblia vizuri.. Roho Mtakatifu atasema nawe, hebu fungua Ufunuo 16.. soma kwa umakini na yatafakari hayo mapigo ya hivyo vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu.
Ufunuo wa Yohana 15:1 Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; MAANA KATIKA HAYO GADHABU YA MUNGU IMETIMIA.
Katika kalenda ya Mungu..ni unyakuo wa kanisa tu tunasubiri, na mpaka sasa dalili zote zinaonyesha kuwa unyakuo ni siku yoyote, saa yoyote na muda wowote, dalili zote za kurudi kwa Bwana kunyakua watakatifu zimekwishatimia, kwani ni dalili ipi unataka uone?
Usikubali kudanganywa na mitume wa uongo na watumishi wa ibilisi ambao kazi yao ni kukusanya magugu matita matita ili yakatupwe kwenye tanuru la moto wa milele.
Kumbuka, leo hii ukikosa unyakuo, hakuna nafasi nyingine tena ya kuokolewa, utakuwa unasubiria tu ile siku ya kuogovya ya Bwana, na katika siku hiyo fedha zako wala ukuu wako havitakusaidia. Na hata kama hiyo siku haitakukuta, fahamu pia kuzimu ipo…huko nako mateso yake hayaelezeki.
Kwahiyo usalama pekee wa roho yako ni wewe umpokee Bwana Yesu mkuu wa uzima, ili uokoke katika hayo yote.
Hebu..amua leo kutubu dhambi zako na kumaanisha kuziacha kabisa..kisha mfuate Yesu kweli kweli, (okoka kabisa kabisa), acha uvuguvugu.
Tunaishi ukiongoni mwa siku za mwisho…usiendelee tena kuwa mjinga, ni heri uonekane umerukwa na akili lakini umeiepuka hukumu ya Mungu, ni heri ukose vyote lakini usikose unyakuo.
Siku ya Bwana inakuja, Siku ya Bwana inakuja.
Malaki 4:1 Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema BWANA wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.
Yeye na aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.