Ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu.

Uncategorized No Comments

Ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu.

Mathayo 26:20 “Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara.

[21]Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.

[22]Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana?

[23]Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.

[24]Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; LAKINI OLE WAKE MTU YULE AMBAYE AMSALITI MWANA WA ADAMU! INGEKUWA HERI KWAKE MTU YULE KAMA ASINGALIZALIWA.

[25]Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.”

Usaliti, ni jambo  baya sana, usaliti sio kumkataa mtu aliyekaribu nawe, kwa hofu au shinikizo Fulani  aidha kwa hofu ya kuaibishwa, au kudharauliwa, au kuuliwa au kutengwa, au kuchekwa n.k. huku moyoni mwako unampenda mtu huyo..hapana! huko ni kumkana huyo mtu. Ndicho alichokifanya Petro kwa Bwana “alimkana Bwana na sio kumsaliti”

Petro alimkana Bwana, kutokana na shinikizo la hofu ya yeye kukamatwa na kwenda kupigwa kama Bwana..Lakini hapo nyuma utaona, alidhubutu kumuhakikisha kabisa Bwana kwamba hata wenzake wote wajapomkana, yeye hatofanya hivyo (Mathayo 26:33-35)

Utaona tena hata baadaya ya kutubu kwake baadaye, alipokutana na Bwana kule baharini bado alimuhakikisha mara tatu kuwa anampenda yeye..(Yohana 21:15-17). Kuonyesha kuwa ni shinikizo ndio lililompeleka kufanya vile, lakini moyo wake bado upo kwa Yesu.

Lakini kusaliti ni jambo baya zaidi kwasababu linahusisha, kumkataa mtu Fulani aliye karibu nawe kwa hiari yako mwenyewe, pasipo shinikizo lolote, kwa maslahi yako binafsi, ni kitendo cha moyo-baridi kabisa.

Yuda tangu mwanzo alikuwa hampendi Bwana, japokuwa yeye alipendwa sana, mahali pengine mpaka Yesu akawa anampa siri zake za ndani japokuwa alikuwa mwizi, biblia inasema hivyo katika Zaburi 41:9

9 Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.

Lakini kinyume chake akarudisha mabaya badala ya mema. Utaona yeye mwenyewe kwa hiari yake akawafuata wakuu wa makuhani bila shinikizo lolote, akawaambia mtanipa nini, nikiwapa Kristo!. Wakamuahidia Pesa. (Mathayo 26.14-16)

Usaliti unafanana na mtu ambaye yupo tayari kumuua au kumletea madhara mzazi wake, kwa faida zake mwenyewe, pengine mali, au cheo, au heshima. Bila kujali kuwa yeye ndiye aliyemnyonyesha, aliyemtunza tangu akiwa tumboni, ndiye aliyemsomesha na kumvisha n.k.

Leo hii wapo watu wanaomsaliti Bwana..Ndio hawa manabii na makristo wa uongo. Ambao wanajua kabisa waliokolewa kwa thamani, walitolewa chini matopeni, lakini wanapokuzwa kidogo, wanaanza kumgeuza Kristo kuwa biashara yao. Wanaacha utumishi walioitiwa, wanatumia fursa ya Kristo, kuyashibisha matumbo yao tu… Hawa ndio wakina Yuda.

Wafilipi 3:18 “Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;

19 mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani”.

Ndugu, ikiwa umekwisha okolewa na Bwana, na tayari umeonja uzuri wake (umepokea Roho Mtakatifu), halafu ukarudi nyuma, ukaacha kuhubiri Injili ya kweli ukageukia injili nyingine, ukaacha wokovu kwasababu tu ya tamaa za ulimwengu huu, ukaanza kuvaa kama watu wa ulimwengu, ukaanza kujipodoa kama watu wa dunia hii, Bwana anatuonya leo kuwa mtu yule amsalitiye mwana wa Adamu ni heri hata asingalizaliwa. (Maana yake mapigo yake katika lile ziwa la moto itakuwa sio ya kawaida)!.

Umeshaokoka halafu unasema ngoja “nikazini tu mara moja” kwa matarajio kwamba utatubu tu! na hakutakuwa na madhara yoyote!.. Nataka nikuambie hata Yuda, alisema hivyo hivyo, alijua bado anazo siku nyingi sana za kuendelea kuwa mtume wa Bwana Yesu, hakujua ile siku ndio ilikuwa siku ya mwisho ya utume wake! Na lile busu ndio lilikuwa busu lake la mwisho!, milele hatamwona Bwana!.. mwisho wake ulikuwa ni MAUTI (Kujinyonga)..

Leo hii unapomsaliti Bwana na kwenda kufanya uasherati, au kujiuza mwili wako, au kuiba au kutapeli, au kufanya anasa, au kuua, au kujilipiza kisasi, ukiwa na mategemeo kuwa utatubu tu! Na utarudiana na Bwana kama kawaida!!..nataka nikuambie “KUWA MAKINI SANA!!”.. Huo uzinzi unaopanga kwenda kuufanya pengine ndio unaweza kuwa mwisho wa mahusiano yako wewe na Bwana!, pengine ndio njia panda yako ya kuzimu!.. Laiti! Yuda angelijua masaa machache mbele ni nini kitakwenda kutukia, asingelimbusu Bwana!, laiti Samsoni angejua masaa machache mbele hatakaa amwone tena mama yake na Baba yake kwa macho yake, asingemfunulia siri Delila!

Kamwe usiipime nguvu ya dhambi kwa uzoefu!.. Mhubiri mmoja alisema “kamwe usimwogope shetani bali iogope dhambi” hiyo ni kweli kabisa!!.. Kwasababu maandiko hayajasema mshahara ya shetani ni mauti, bali yalisema “mshahara wa dhambi ni Mauti”

Bwana Yesu atusaidie, kila siku tuweze kujitenga na dhambi.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *