SHIKA UZIMA WA MILELE ULIOITIWA

Biblia kwa kina No Comments

SHIKA UZIMA WA MILELE ULIOITIWA

Kila mmoja wetu aliyeokoka kweli kweli anapaswa kujua kitu cha kwanza Mungu alichotuitia sio mafanikio ya hapa duniani hayo ni ya ziada, lakini kikubwa ambacho tumeitiwa ni UZIMA WA MILELE.

1Timotheo 6:12 “Piga vita vile vizuri vya imani; SHIKA UZIMA ULE WA MILELE ULIOITIWA, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi”.

Sasa watu wengi hatufahamu huu uzima wa milele ni uzima gani, lakini leo tutaangalia kwa ufupi maana ya uzima wa milele ili tupate sababu ya kuushikilia kwa juhudi zote.

Uzima wa milele ni maisha yasiyokuwa na mwisho. Yaani unaishi tu, na utaendelea kuishi, hivyo hivyo kwa siku zisizokuwa na ukomo.

Ukikaa chini ukajaribu kutafakari kwa umakini hili Neno UZIMA WA MILELE, utashangaa sana, wakati mwingine utajiuliza hili jambo linawezekanaje kanaje, na ukilitafari sana utaona kama akili yako inafika sehemu inagota. Eti unaishi tu siku zote bila kuwa na kikomo, unaishi leo, miaka mia inapita bado unaendelea tu kuishi.

Miaka elfu inapita bado unaendelea kuishi, miaka milioni moja inapita bado unaendelea kuishi, miaka bilioni moja inapita bado unaendelea kuishi. Miaka trilioni moja inapita ndio bado hata maisha hayajaanza…unaendelea tu, miaka kuadrilioni moja (ambayo ni sawasawa na miaka trilioni elfu moja), inapita bado unaendelea kuishi, miaka kuintilioni moja inapita ndio bado hata hakuna dalili ya kufika mwisho, miaka seksitilioni moja, wewe bado unaendelea tu kuishi. Miaka oktilioni na nonilioni, na desilioni na anidesilioni inapita, hapo bado utaendelea tu,..miaka dodesilioni, na tradesilioni na kuatuordesilioni na kuindesilioni na seksidesilioni bado tu safari inaendelea ukiwa bado kama kijana mdogo tu, n.k. n.k. tukiziandika namba zote hapa tunaweza kujaza ukurasa mzima na bado zisitoshe…kamwe hakuna siku itakayofika na ukasema leo ni ukomo wa mimi kuwa hai, kamwe hutakaa ufe, utakuwa hai hivyo hivyo daima..huo ndio uzima wa milele.

Embu jaribu kufikiria hayo ni maisha marefu kiasi gani, leo hii tu ikipita miaka 20 au 30 unaona kama ilikuwa ni zamani sana, na tena unaiita enzi hizo, sasa hapo bado haijatapita miaka milioni moja sijui hiyo utaiitaje labda utaita kama ile ya historia zama za mawe za kwanza, pengine hata kumbukumbu zake utakuwa umezipoteza..

Jambo kama hilo ukilifikiria sana, kuna mahali hata akili yako itafika na kugota, jaribu uone,, kwasababu ni jambo ambalo tangu umezaliwa halijawahi kuwa sehemu ya maisha yako, tangu ulipokuwa mdogo mpaka unakua umekuwa ukijua kuwa siku moja maisha yako yatakwisha kwa kifo, lakini pale unaposikia kuwa hutakaa ufe tena, akili yako inaweza kushindwa kulipokea jambo hilo kwa wakati huo.Lakini ukweli ni kwamba hilo litawezekana, lakini sio kwa kila mtu anayeishi leo hii duniani, bali kwa kundi Fulani tu la watu, si watu wote wataishi milele.

Na ndio maana biblia inasema, Karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Karama ni zawadi, hivyo zawadi kubwa kuliko zote ambayo Mungu anaweza kumpa mwanadamu, si nyingine zaidi ya uzima wa milele. Yaani maisha yasiyokuwa na ukomo..Huoni kama hiyo ni zawadi iliyopitiliza?

Sasa Mungu asiyekuwa na mwisho ametuahidia zawadi hiyo kuu bure, Hata tusingepewa zawadi nyingine hiyo tu ya Uzima wa Milele ingetutosha. Ni zawadi kubwa sana isiyoelezeka.

Na kumbuka pia Mungu asiye na mipaka, miaka hiyo yote hatutakuwa tunaishi tu kama watu wasiokuwa na mwelekeo “idle”. Au unaishi tu bila maaana yoyote hapana! vinginevyo umilele utakuwa wa ku-boa.

Badala yake kila siku, kila wakati kutakuwa na matukio yake na mambo yake mazuri mapya, yaani tutayafurahia maisha kila iitawapo leo, kwasababu kila siku itakuwa na mambo yake, kutakuwa hakuna magonjwa, kutakuwa hakuna kuzeeka, kutakuwa hakuna shida, kutakuwa hakuna mahangaiko, wala kupigwa na jua hakutakuwepo, wala ulemavu hautakuwepo, wala uchungu, wala kuudhiwa, wala kuumizwa, wala kudaiwa. Siku zote tutaishi katika raha isiyo na kifani, tukiushangaa utukufu wa Mungu na kumwabudu yeye katika raha isiyoelezeka.

Mungu kashaipigia mahesabu kila siku moja ya umilele hivyo analijua tukio ambalo litatokea siku Fulani ya mwaka Fulani wa bilioni moja huko mbeleni kwamba wewe utakuwa unafanya kitu Fulani na Yule kitu fulani,..Huyo ndio YEHOVA..hatuishi kumshangaa kwa matendo yake ya ajabu.

Na ndio maana Mungu anasema katika..

Isaya 55:8 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”.

Kauli hiyo ya Mungu inatuthibitishia kuwa mipango ya Mungu aliyotuandalia sisi, hatuwezi kuidhania au kuifikiria ipasavyo hata kwa chembe ndogo sana. Kwasababu ipo mbali sana na upeo wetu wa kufikiri, na ndio maana ni jukumu letu kuhakikisha sisi sote hatuukosi huo uzima wa milele.. Kwasababu hapa ni kama tunaandaliwa tu kwa ajili ya kuishi maisha halisi, hapa duniani hatuna maisha, miaka 70 au 80 sio maisha. Bali tunaandaliwa tu kwa ajili ya kuishi kule ambako Mungu alitukusudia tuishi, tunatengenezwa tu ili tuweze kustahimili huo umilele unaokuja huko mbeleni..

Hivyo tukiwa tunayatafakari hayo kila siku tutapata nguvu ya kutokujali ni nini tunapoteza sasa tukiwa hapa duniani, kwa ajili ya maisha yetu ya umilele ya baadaye…hatutojali tunapoteza fursa ngapi za biashara kwa ajili ya kuhudhuria maombi, hatutojali tunapoteza hiki au kile kwa kwenda ibadani, kwa kujifunza Neno la Mungu…Hatutojali ni mambo mangapi ya kidunia yanatupita, sisi tunatazama maisha ya milele Mungu aliyotuandalia…

Hata mithali ya kidunia inasema, “usiache mbachao kwa msala upitao”. Ikiwa na maana tusiopoteze uzima wetu wa milele kwa vitu vya kidunia vinavyopita, ambavyo mwisho wake ni hapa tu..Itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima, kisha tupate hasara ya nafsi zetu.? Kwasababu mshahara wa dhambi ni mauti…lakini karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Lakini uzima wa milele huu kuupata ni bure, nao unakuja kwa kumwamini tu YESU KRISTO, pale unapotubu kwa kudhamiria kwa dhati kutoka moyoni mwako kwamba kuanzia leo unaacha dhambi zako zote..Unafanya maamuzi ya kuacha pombe, kuacha uasherati, kucha uvaaji mbaya, kuacha rushwa, kuacha wizi n.k. Na vitu vyote ulivyokuwa unaviona vinakufaidisha sana vya kidunia unaviacha vyote unavihesabia kama ni mavi. Kama Mtume Paulo alivyovihesabia.

Wafilipi 3.7 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.

8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama MAVI ili nipate Kristo”

Na baada ya kutubu na kuyahesabia mambo yote uliyokuwa unayafanya machafu kama MAVI. Hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamwisha katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako sawasawa na Matendo 2:38,.Kisha Bwana atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu..Hivyo Hatua hizo zote zikikamilika juu yako basi na wewe utakuwa umefanyika kuwa mwana wa Mungu na yeye mwenyewe atakupa karama hii ya uzima wa milele bure..

Kumbuka huwezi kuupata uzima huo kwa mwanadamu mwingine yoyote duniani au mbinguni, anayejiita, mtume, au nabii, au kuhani n.k. hakuna mwanadamu yoyote zaidi ya Yesu Kristo peke yake ndiye anayeweza kuachilia karama hiyo ya uzima wa milele ndani ya Mtu.

Na ndio maana yeye mwenyewe alisema.

Yohana 3:36 “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia”.

Hivyo kila mtu anayemwamini na kumpokea, anakuwa tayari na uhakika huo kuwa ndani yake uzima wa milele upo. Hata akifa leo, siku ile ya ufufuo atafufuliwa na kuungana na watakatifu wengine, na kwa pamoja wataishi milele na Mungu mbinguni milele.

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.

Shika uzima wa milele!! shika uzima wa milele!!

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *