SILAHA MADHUBUTI ANAYOITUMIA SHETANI KUWAANGUSHA WAKRISTO.
Kama wewe ni mkristo halisi, yaani namaanisha umeokoka kweli kweli kwa kutubu dhambi zote na kuacha ulimwengu kwa ufupi umezaliwa mara ya pili, Fahamu kuwa unayo maadui wengi wanakuwinda usiku na mchana, na maadui hao sio wanadamu wenzako, bali ni shetani na jeshi lake. Usidhani kuwa shetani anafurahia wewe kuwepo kwenye wokovu, hawezi kuwa na furaha kamwe, kwani anajua unao uzima wa milele na yeye alikwisha kuhukumiwa kuangamizwa kwenye lile ziwa la moto..hiyo ndiyo hukumu yake na sasa anajua hana lolote tena kwa Mungu, hawezi tena kutubu hana hiyo nafasi.. hivyo anachokifanya ni kuelekeza vita vyake kwa wanadamu ili awavute upande wake wakaangamie nao huko.
Ufunuo wa Yohana 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.
[13]Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.
[17]Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.
Sasa, ni Vizuri kufahamu kuwa shetani hapigani na watu walio nje ya Yesu..yaani ambao hawajaokoka, hao tayari anawamiliki. Vita kubwa ipo kwa wakristo ambao ndio kanisa, ndiyo yule mwanamke.
Na silaha kubwa anayoitumia shetani kuwanasa wakristo sio nyingine zaidi ya DHAMBI! bila hiyo hawezi kuwapata kamwe, haijalishi atakukuja na jeshi la mapepo yote wabaya hawezi kuwapata.
Ndio maana kila siku tunapaswa kujitakasa na kujitenga na dhambi yoyote ile, shetani hatumshindi kwa kufunga tu na kuomba, au kwa kwenda kanisani, au kwa kutoa fungu la kumi, hatumshindi kwa kuingia kwenye maombi ya vita! huko kote ni kujiimarisha kiroho, lakini shetani tunamshinda kabisa kabisa kwa kukaa mbali na dhambi, kukaa mbali na ulimwengu. Hiyo ndiyo silaha ya kumshinda kwani na yeye anatumia hiyo hiyo kutushinda.
Ufunuo wa Yohana 12:11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.
Jiulize hapo kwanini haijasema wakamshinda kwa mafuta ya upako, au kwa kanisa zuri, au kwa maombi ya vita.. Bali kwa damu ya Mwana kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Halafu anasema ambao HAWAKUPENDA MAISHA YAO HATA KUFA.
Maana yake walijikana nafsi kweli kweli, walikubali kuacha fashions na mitindo ya kiulimwengu, na kuitwa washamba kwa ajili ya Kristo, hao ndio walioshinda.
Lakini, wewe Dada unategemea vipi kumshinda shetani na huku hujakubali kujikana nafsi, bado unaupenda ulimwengu, unavaa mavazi na mapambo ya kiulimwengu, ulimwenguni huko wanawake wameharibiwa wanavaa vitu vya ajabu, wanatembea uchi, wamebadili mionekano yao kuanzia kichwani mpaka kwenye kucha, na wewe unafuatisha namna yao…na huku unasema umeokoka, na unaenda kanisani, shetani utamshindaje hapo?
Kumbuka shetani ni muongo na baba wa huo, utadhani umeokoka kweli, unaimba kwaya, unanena kwa lugha, unawaombea wagonjwa na wanapona, kumbe shetani ameshakudanganya uendelee kubaki katika uvugu uvugu, uupende ulimwengu kidogo na kanisani kidogo, na mwisho wako utajikuta upo kuzimu pasipo kutarajia…itakuwa ni majuto makubwa sana.
Hivyo ikiwa kweli umeamua kumfuata Yesu na kuwa mwanafunzi wake, basi fahamu kuwa shetani anakuwinda kila siku na silaha yake anayoitumia ni hiyo hiyo ambayo na sisi hatuna budi kumshindia kwa kutoruhusu dhambi yoyote maishani mwetu, kila siku tunapaswa kujikana nafsi na kukaa mbali na mitindo na fashions za kidunia.
Kama ni mwanamke unakaa mbali na mavazi ya kiulimwengu kama vimini, suruali yoyote iwe pana au ndefu, magauni ya kubana, na ya mipasuko, na mgongo wazi, kifua wazi hayo ni mavazi ya kishetani, na mapambo aina zote iwe ni hereni ndogo, rangi za kucha, mekaups, lipustiks, wigi, na misuko aina zote, na namna zote za kidunia unakaa nazo mbali maana huko ndiko kumshinda shetani.
Kumbuka vitu hivyo mavazi na mapambo yanawapeleka wanawake wengi kuzimu na ndiyo silaha anayoitumia shetani kwa sasa. Hizo vitu ni najisi na machukizo kwa Mungu, biblia imeweka wazi kuwa wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujistiri na sio kwa kujipamba kwa nje yaani kutumia hivyo vitu Soma 1Timotheo 2:9 na 1Petro 3:3.
Na halikadhalika imeweka wazi kuwa mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume yaani suruali Soma kumb 22:5. Sasa jiulize hata kama biblia haijasema hivyo kuwa mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume, je kweli suruali ni vazi la kumstiri Mwanamke? kama tu sio kumkosea Mungu, na ndicho shetani anachotafuta, ndio maana suruali sasa hivi imekuwa fashion, wanakuambia kuna suruali za wanawake? Jiulize kwanini isiwepo gauni za wanaume? ni uongo mtupu! Hata maumbile yako yako yenyewe inakataa.
Kama mkristo kaa mbali na dhambi, kaa mbali na udunia.
Kaka/Dada kaa mbali na fashions, kaa mbali na ulimwengu. Shetani yupo kazini ananguruma kama simba angurumavyo atafute binti aliyeokoka, Kijana aliyeokoka, mama/baba aliyeokoka ammeze.
Zaidi ya yote jifunze kutumia silaha zingine tulizopewa katika Waefeso 6:12, usipunguze maombi, usipunguze,mifungo, usipunguze mikesha, usipunguze kusoma biblia, usipunguze kushuhudia/unjilisti na mambo mengine kama hayo.
Kumbuka ufalme wa Mungu unatekwa na wenye nguvu ndio wanaouteka, wale ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.
Na utakatifu unatafutwa tena kwa bidii (Waebrania 12:14).
Tunaishi ukiongoni mwa nyakati, Yesu yupo mlangoni.
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.