TUNAHITAJI KUSAIDIANA

Uncategorized No Comments

TUNAHITAJI KUSAIDIANA

Nakusalimu katika jina kuu la Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Katika ukristo kusaidiana sisi kwa sisi ni jambo la muhimu sana na ni moja ya silaha ya kumshinda adui.

Hebu tuitafakari habari hii kwa pamoja kisha tujifunze somo.

1 Mambo ya Nyakati 19:8 “Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.

[9]Wakatoka wana wa Amoni, wakapanga vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwandani.

[10]Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami.

[11]Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni.

[12]Akasema, Wakiwa Washami ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe.

[13]Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake.

[14]Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake.

[15]Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu”.

Yoabu alipoona maadui ni wengi na nguvu yake ni ndogo alimwambia ndugu yake kilichobaki ni KUSAIDIANA TU, maadui wakiwa hodari kwngu utanisaidia, na wakiwa hodari kwako nitakusaidia. Na ndivyo walivyoshinda.

12] “Akasema, Wakiwa Washami ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe”.

Nini tunajifunza hapo.

Biblia inasema..

Mhubiri 4:9-12 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.

[10]Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!

[11]Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?

[12]Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; WALA KAMBA YA NYUZI TATU HAIKATIKI UPESI.

Kusaidiana ni jambo la muhimu sana katika safari ya imani. Kila mmoja wetu anahitaji kusaidiwa na yeye kusaidia wenzake. Huo ndio umoja ambao Bwana alituombea kwa Baba tuwenayo.

Yohana 17:20 “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.

[21]Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma”.

Na mahali pa muhimu sana kusaidiana mbali tu na kushauriana, kutiana moyo ni KUOMBEANA pia.

Ndugu yako anaweza akazidiwa na kazi akakosa muda wa kutosha wa kuomba, au pengine akawa katika hali ya udhaifu wa mwili, lakini wewe unaweza ukawa na muda wa kutosha wa kuomba..ukatumia hiyo nafasi kumwombea/ kuwaombea ndugu zako katika imani, na wewe pia siku ukikosa muda wa kuomba, au ukiwa katika hali ya udhaifu ndugu zako wanakuombea, huo ndio umoja na ushindi wetu.

Hivyo uingiapo kwenye maombi, daima wakumbuke ndugu zako katika imani, ukijua kuwa nao wanakuombea, usijiombee tu mwenyewe.

Tunapoombeana kuna neema ya ziada inashuka juu yetu…(Mungu anaachilia rehema, amani, uponyaji, nguvu ya kuendelea mbele), Tunapomwomba Bwana atuhurumie sisi na kuwahurumia wengine, tunafungua wigo mpana wa Yule tunayemwombea kuponywa na kwetu sisi pia kuponywa pamoja na kufunika wingi wa dhambi..(Yakobo 5:20).

Hivyo kile kile unachotaka Mungu akutendee, muombee pia ndugu yako atendewe.

Ayubu alikuwa ni mwenye haki lakini hakuacha kuwaombea wanawe, vivyo hivyo na sisi kama Kanisa la Kristo hatuna budi kuombeana sisi kwa sisi, wakati mwingine kwa kutajana majina.

Yakobo 5:16 “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii”.

Bwana atubariki na kutusaidia.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *