TUPO KATIKA ILE SAA YA KUHARIBIWA.

Siku za Mwisho No Comments

TUPO KATIKA ILE SAA YA KUHARIBIWA.

Jina la mwokozi wetu YESU KRISTO litukuzwe mpendwa, karibu tujifunze habari za uzima.

Kama wewe ni msomi mzuri wa BIBLIA utakuwa unafahamu kuwa kuna saa ya kujaribiwa na kuharibiwa kwa huu ulimwengu.

Bwana Yesu alisema mwenyewe..

Ufunuo 3:10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika SAA YA KUHARIBIWA ILIYO TAYARI KUUJILIA ULIMWENGU WOTE, KUWAJARIBU WAKAAO JUU YA NCHI.

[11]Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.

Unaona hapo, kuna saa ya kuharibiwa kwa huu ulimwengu inakuja, lakini pia kuwajaribu watu wakaao juu ya nchi.

Sasa anaposema kuwajaribu wakaao juu ya nchi, hamaanishi watu wote waliopo duniani bali wale wanaolitia jina la Yesu, ndio watakaojaribiwa.

Lakini baada ya kujaribiwa ndipo Uharibifu unakuja kwa wote.

Sasa watu wengi hawajui kuwa tupo katika hiyo saa ya kujaribiwa! Na saa hii ilianza lini?

Saa hii ilianza katika kanisa hili la Laodikia ambalo ndilo kanisa la mwisho kabisa kati ya yale makanisa saba, na Kristo aliliambia lile kanisa la sita (Filadelfia) kwamba atawaepusha na hii saa ya kujaribiwa kwasababu wamelishika Neno lake, maana yake saa hii ilikuwa ianze katika kanisa hilo lakini Kristo aliwaepusha.

Na sasa sisi tunaoishi katika kanisa hili la Laodikia, tupo katika ile saa ya kujaribiwa, ambapo ilianza mwanzoni mwa karne ile ya 20.

Na huu Uharibifu na kujaribiwa ni mwanzo wa utungu tu!, lakini upo uharibifu na jaribu lenyewe ambalo litakuja baada ya watakatifu kunyakuliwa.

Mwanzoni mwa karne ya 20, tulishuhudia uharibifu mkubwa wa dunia kutokana na vita vya kwanza na ya pili, lakini pia uharibifu uliosababishwa na matetemeko makubwa yaliyoikumba ulimwengu, njaa, magonjwa n.k sasa huo ulikuwa ni mwanzo tu wa uharibifu bado uharibifu wenyewe ambapo hii dunia yote itaharibiwa na kufanywa ukiwa.

Isaya 13:9 Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.

Sasa huku kujaribiwa kukoje?

Kama nilivyotangulia kusema, watu wanaojaribiwa ni watu wa Mungu na sio kila mtu anapitia jaribu hili. Na jaribu hili ni Mungu mwenyewe anawajaribu watu wake aone kuwa wanampenda kweli?

Na ni kwa namna gani tunajaribiwa? Tusome..

Kumbukumbu la Torati 13:1 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

[2]ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

[3]wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, KWA KUWA BWANA, MUNGU WENU, YUAWAJARIBU, APATE KUJUA KWAMBA MWAMPENDA BWANA, MUNGU WENU, KWA MIOYO YENU YOTE NA ROHO ZENU ZOTE.

[4]Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.

Umeona hapo, kumbe Mungu anawajaribu watu wake apate kujua kwamba wanampenda kwa mioyo yao yote, kama alivyoagiza akisema..

“Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja.

[5]Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.” (Kumb 6:4-5).

Kwahiyo Mungu anawajaribu watu wake ajue mioyo yao kupitia manabii wa uongo!! Hii ni siri kubwa tunapaswa tufahamu.

Katika hili kanisa tunaloishi, sisi wote ni mashuhuda tumeshudia jinsi manabii wa uongo wanavyozidi kuongezeka kwa kasi kila siku!! Jambo ambalo halikuwahi kutokea katika makanisa yaliyopita.

Hii ni kuonyesha kuwa tupo katika ile saa ya kujaribiwa!!

Na biblia inasema Mungu hamjaribu mtu bali mtu hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe (Yakobo 1:13-14).

Maana yake moyo wako ukitamani mambo ya ulimwengu huu, tamaa za kidunia, unamwendea Mungu kwasababu ya kutaka kutimiziwa haja zako, lakini moyoni mwako hutaki kutii maagizo yake, Bwana anasema mtu kama huyo ataangukia katika mikono ya manabii wa uongo ambao Mungu mwenyewe amewaandaa kwa kazi hiyo ya kuwatabiria watu uongo sawa sawa na matamanio ya mioyo yao, na mwisho watadhani kutabiriwa na kujibiwa tamaa zao ndiko Mungu anawapenda kumbe wameshapotea.

Ndicho kilichomtokea Ahabu, hakutaka kutii sheria za Mungu lakini alitaka tu atabiriwe mafanikio, aende vitani ashinde, kwasababu ya tamaa zake Mungu akamletea nguvu ya upotevu kupitia wale manabii wa uongo ili kwamba atabiriwe mafanikio aende vitani apotee. Tunasoma

2 Mambo ya Nyakati 18:19 BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

[20]Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani?

[21]Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo.

Soma pia..

Ezekieli 14:7 Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, BWANA, nitamjibu, mimi mwenyewe;

[8]nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

[9]Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, BWANA, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.

Umeona hapo kuna nguvu ya upotevu ambao unatoka kwa Mungu, kuwapoteza wale ambao wanamtafuta Mungu kwa tamaa zao (wale wasiompenda Mungu kwa mioyo yao na roho zao), hiyo nguvu imeachiliwa katika kanisa hili la Laodikia, tupo katika ile saa ya kujaribiwa.

Fahamu kuwa huu ni mwanzo tu wa utungu, kuna jaribu kubwa litakuja baada ya unyakuo, ambayo kwa wewe uliyebaki utaingia katika jaribu hilo la mpinga-kristo, aidha ukubali chapa au ufe kwa mateso.

Wapo wengi wanaojifariji kuwa baada ya unyakuo watakuwa na nafasi ya pili. Ndugu Kama hutataka kuitii nguvu ya Roho Mtakatifu itokayo kwa Mungu inayokushawishi leo hii umgeukie Mungu, basi fahamu kuwa hutakuwa na tumaini lolote huko mbele baada ya unyakuo biblia imeweka wazi kabisa kuna NGUVU nyingine itakayoachiwa kutoka kwa Mungu juu ya watu waliosalia kuwafanya wauamini uongo wa mpinga-kristo. Nguvu hiyo biblia inaiita nguvu ya upotevu. Ndiyo inayofanya kazi sasa hivi katikati ya manabii wa uongo.

Kwasababu ya maasi kuongezeka na upendo wa watu kumpenda Mungu kupoa, Mungu ameachilia hiyo nguvu ya upotevu ili watu waendelee kuuamini UONGO. Ile nguvu ya kumfanya mtu aone njia anayoiendea sio sawa inaondoka ndani yake na inakuja nguvu nyingine mpya ya kumfanya aone na kuamini asilimia mia kwamba yupo katika njia sahihi.

2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

Ndugu mpendwa saa tunazoishi ni za hatari sana….Tujitahidi sana tuupende na kuufuata ukweli ambao upo katika Neno la Mungu, ili Nguvu hii ya upotevu iliyoachiwa duniani sasa ya kuuamini uongo isije ikatumeza, na ghafla tukajikuta kwenye ziwa la Moto.

Hususani katika kipindi hichi cha siku za Mwisho, uongo umezagaa kila mahali…kwasababu hiyo tupo katika ile saa ya kujaribiwa.

Nimewahi kuona muhubiri maarufu akihubiri na kutetea dhambi madhabahuni, hali kadhalika nimeona mwingine akitumia maandiko kabisa kusapoti uvaaji wa suruali na vimini, na kama mtu huyajui maandiko vizuri anakuchukua!..kama ni wa kusoma tu mstari mmoja bila kujua mingine unakwenda na maji! Na maelfu tayari wamechukuliwa!. Hiyo ni mifano tu ya nguvu ya upotevu iliyoachiliwa nyakati hizi ili watu waamini uongo.

2Timotheo 3:13 “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”.

Tutubu dhambi, na kujitenga na uovu kwa kadiri tuwezavyo..Bwana atusaidie, tukimwamini yeye, tukimtegemea yeye ni mwaminifu, hawezi kutuacha tukadanganyika au kuchukuliwa na hizo nguvu..Hivyo ni wajibu wetu kumpenda Mungu siku zote kwa nguvu zetu zote, kwa roho zetu zote na kwa akili zetu zote.

Bwana atubariki.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *