
TUPO KATIKA ILE SAA YA KUJARIBIWA.
Ufunuo 3:10 “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, KUWAJARIBU WAKAAO JUU YA NCHI”.
Kuna saa ya kuharibiwa inakuja huko mbeleni, ni wakati ambapo kila mtu kwa macho yake atakuwa anaona jinsi dunia inavyokwenda kuisha ndani ya kipindi kifupi sana, kutokana na dhiki, na mapigo, pamoja na mambo ya kutisha yatakayokuwa yanaendelea duniani wakati huo..
Lakini leo hatutaingia sana ndani kuzungumzia hiyo saa ya kuharibiwa kwa huu ulimwengu, ila tutaangalia hii saa ya kujaribiwa.
Kuna saa ya kujaribiwa na kuharibiwa inayokuja huko mbeleni?
Lakini, je unahabari kuwa tupo katika hiyo saa ya kujaribiwa? kama ulidhani labda hiyo saa itakuwa ni baadaye sana, nataka nikuambie huo ni ukweli nusu, ukweli kamili ni kwamba mpaka sasa tumekwishaingia kwenye hiyo saa na tupo kwenye majaribio.
Je unafahamu hilo?
Ikiwa we ni mkristo halisi, basi, fahamu kuwa upo kwenye saa ya kujaribiwa? Utauliza ni kwa namna gani…Hebu tusome hili andiko kwa umakini kisha tutafakari vizuri..
Mithali 12:13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.
Unalielewa hilo andiko vyema, bila shaka hilo ni fumbo ambalo linahitaji kufumbuliwa.
Kama tunavyojua mdomo kazi yake mbali na kula ni kuongea, sasa mdomo unavyoongea maneno ambayo ni uongo/makosa.. maana yake uongo ule au kosa lile linaenda kuwa mtego kwa mwingine atakayesikiza uongo huo na kupokea kama kweli…hapo tunasema mtu huyo amenaswa au ametegwa kwa makosa ya midomo.
Na hapo anasema, sio wote watanaswa na huo uongo/kosa la mdomo bali ni wabaya… hebu tusome tena..
“Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; BALI MWENYE HAKI ATATOKA KATIKA TAABU”.
Umeona hapo, anasema mwenye haki atatoka katika taabu, maana yake kwenye hilo jaribu.
Na kama tulivyotangulia kusoma… Bwana aliliambia hilo kanisa la Filadelfia kuwa atamlinda na hiyo saa ya kuharibiwa iliyotayari kuujilia ulimwengu wote, na kuwajaribu wakaao juu ya nchi. Na ni kwanini Bwana awalinde..ni kwasababu wamelishika neno la subira yake.
Ufunuo3:10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.
Maana yake ni kwamba ile saa ya kujaribiwa na kuharibiwa kwa huu ulimwengu ilipaswa iijilie ulimwengu katika kanisa la sita/Filadelfia , lakini Bwana aliwaepusha kwasababu kanisa hilo lilitembea katika njia yake yaani utakatifu.
Kwahiyo sisi ambao tupo katika kanisa la saba/lauodikia ndio tunaishi katika hiyo saa ya kujaribiwa na kuharibiwa ambayo imeanza katika karne ya 20..na itakuja kuwa wazi kabisa kwenye kilele chake.. yaani wakati wa mwisho wa hii dunia.
Ndio maana..tumekuwa tukishudia dalili kadha wa kadha ya hiyo saa tangu ile karne ya 20.. mambo ambayo hapo mwanzo hayakuwepo, mfano vitu kama matetemeko makubwa ya ardhi, magonjwa hatari, vita, njaa n.k ambayo vimekuwa vikileta uharibifu mwingi sana katika dunia..Hii ni kutuonyesha kuwa huo wakati mbaya umekaribia sana.
Sasa tutajuaje kuwatupo katika majaribio hayo? Au ni kwa namna gani tunajaribiwa?
Tukirudi katika ile mithali 12:13, Neno la Mungu linasema..
“Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; BALI MWENYE HAKI ATATOKA KATIKA TAABU”.
Kama tulivyoona maana ya hiyo mithali…kwamba ikiwa mdomo utanena makosa au uongo..moja kwa moja kwa mtu mbaya itakuwa ni mtego/jaribu..bali kwa mwenye haki atatoka kwenye hilo jaribu.
Kwanini mtu mbaya ataingia kwenye huo mtego au hilo jaribu kirahisi..ni kwasababu hana kweli ndani yake hivyo hawezi kutambua uongo/kosa la mdomo… hivyo unakuwa ni mtihani mgumu kwake…Bali mwenye haki atatoka/atafaulu.
Kwahiyo anachokifanya Bwana katika siku hizi za mwisho mwisho, ili awajue walio wake kweli kweli..anatoa mtihani/jaribio kwa wanafunzi wake (wakristo wa kweli) na atakayeshinda.. basi atakuwa amefaulu na kuepushwa na ule uharibifu wenyewe unaokuja.
Na ili kufanikisha hili, Bwana amenyanyua midomo mingi kwaajili ya hiyo kazi! Na midomo hii kazi yake ni kuzungumza uongo/makosa ili iwe mtego kwa wale wabaya..na hii ndio jaribu ambalo tunauzungumzia hapa.
Manabii wote wa uongo ni midomo ambayo Bwana ameinyanyua kutimiza kusudi lake la kuwajaribu watu wake ili kuwajua wenye upendo wa kweli na wale ambao ni wasindikizaji, hebu tusome haya maandiko tuelewe vizuri…
Kumbukumbu la Torati 13:1-3 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
[2]ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
[3]wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, YUWAJARIBU, APATE KUJUA KWAMBA MWAMPENDA BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
Umeona hapo, tupo katika saa ya kujaribiwa!!.
Lakini, lipo jaribu hasa ambalo lipo mbeleni kwa wale wakristo vuguvugu watakaoachwa kwenye unyakuo, hao watapitia jaribu kubwa sana kutoka kwa shetani mwenyewe..wakati ambao shetani amepewa muda mfupi kutawala dunia…chini ya mpinga Kristo…itakuwa ni kuchagua kimoja, aidha upokee chapa uishi au ukatae ufe kwa mateso mengi. Hilo ndilo jaribu hasa ambalo lipo karibu sana.
Hivyo ndugu, angalia jinsi muda unavyozidi kukimbia..tunaishi ukingoni kabisa.. unyakuo wa kanisa upo karibu sana kuliko tunavyodhania, hebu fumbua macho yako utoke usingizini…tumeambiwa tukeshe katika kuomba na kusali huku tukizidi kujiweka katika hali ya usafi/utakatifu mwili, nafsi na roho.
Kumbuka tupo katika saa ya kujaribiwa, manabii wa uongo ambao ni pamoja na wachungaji wa uongo, wainjilisti wa uongo, mitume na waalimu wa uongo, waimbaji na wanakwaya wa uongo… hao wote wametapakaa kila kona ili kutimiza kusudi hilo.
Mpende Bwana kwa moyo wote na nguvu zote, kaa mbali na udunia, tafuta utakatifu kwa bidii..na Bwana atakujaza Roho wake mtakatifu na hivyo utaenda kwenye unyakuo.
Lakini..ikiwa injili unayopenda ni kuhubiri tu mafanikio ya hapa duniani na kufarijiwa farijiwa katika dhambi… basi ni wazi kuwa huwezi kutoka katika huu mtego/hili jaribu.
Bwana atusaidie sana.
Je umempokea Yesu kweli kweli na kutoka kwenye kamba ya madhehebu, au bado umeshikilia ukristo na ulimwengu? Bado unalewa na hii dunia, bado unaendelea kuishi na mke/mume wa mtu, bado unavaa mavazi ya ukahaba, bado unafanya mastabartion/kujichua, bado unavuta sigara na kutumia vilevi, na madawa ya kulevya, bado unacheza kamari, na magemu? Bado unatumia mkorogo na nywele bandia?
Hebu, leo dhamiria kuacha hayo yote na kumkabidhi Kristo maisha yako..ili akufanye kiumbe kipya… kumbuka dhiki kuu imekaribia na hata kama utasema bado sana, hukumu ipo pale pale, na haujui siku wala saa ya kuondoka duniani… hivyo suluhisho tu ni kumpokea Yesu Kristo.
Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi.
Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwa Yesu, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa.
Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..
Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.
Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Hongera kwa kuokoka.
Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namna hizi hapa chini..+255 789001312
- Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.