
Umepewa muda ili utubu
Ufunuo wa Yohana 2:20 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.
[21] NAMI NIMEMPA MUDA ILI ATUBU, WALA HATAKI KUUTUBIA UZINZI WAKE.
[22]Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;”
Biblia inatufananisha sisi na kama miti izaayo matunda, hivyo kila mmoja wetu anapaswa azae matunda kwa Mungu, kadhalika biblia imetuonya pia mti usiozaa matunda utakatwa, kama tunavyosoma mfano Bwana wetu alioutoa katika..
Luka 13:6 “Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.
7 Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, MIAKA MITATU HII naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?
8 Akajibu akamwambia, Bwana, uuache MWAKA HUU NAO, hata niupalilie, niutilie samadi;
9 nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.”
Mtini huo ulipewa muda wa miaka 3, ili uzae matunda, lakini haukuzaa, hivyo mwenye shamba alitaka kuukata lakini akauongezea neema ya mwaka mmoja zaidi iwe 4 ili kwamba ukizaa katika huo muda itakuwa ni vema lakini usipozaa ndipo ukatwe. Mfano huu ukitufundisha kwamba kila mmoja wetu amepewa muda wa kumzalia Mungu matunda, hichi ni kipindi kilichoanza tangu wakati ule uliposikia kwa mara ya kwanza NENO LA KRISTO katika masikio yako mpaka wakati huu uliopo sasa..Ni dhahiri kuwa pengine imeshapita miaka zaidi ya mitatu, lakini je! Tangu huo wakati uliosikia ulilikubali kwa kulizalia matunda? Au ulilipuuzia na kusema bado bado kidogo?.
Na kama kilishapita kipindi kirefu namna hiyo na bado hujabadilika basi ujue upo katika muda wa nyongeza, na wakati wowote unaweza UKAKATWA. Leo hii umeongezewa neema fupi, Mungu analia kwa nguvu ndani ya moyo wako, uache dhambi, umgeukie yeye, na dhamiri yako inakushuhudia kabisa kuwa unamuhitaji Mungu katika maisha yako, unaona kabisa upo katika vifungo vya uovu na dhambi na bado umesikia injili mara nyingi lakini hutaki kugeuka unaufanya moyo mwako kuwa mgumu, upo katika hatari ya kukatwa.
Kumbuka ni neema za Mungu tu unaishi katika muda huu wa nyongeza, hiyo sauti ya Mungu inayolia ndani yako inayokushuhudia hiyo njia yako sio sawa, haitadumu milele ipo siku itanyamaza,. Usitamani ufikie hiyo hatua kwa maana utakuwa ni wakati mgumu sana ambao hata uhubiriweje Injili hautashawishika tena kugeuka kwasababu umeshakatwa. Hali itakuwa mbaya hicho kipindi kiasi ambacho hata ukifanya uzinzi hautasikia kushitakiwa ndani yako, hata ukiwa mlevi utaona ni sawa tu, ukielezwa mambo yahusuyo wokovu utaona ni hadithi za kutunga, Utaishia kukosoa biblia na watakatifu kila siku kwasababu kifo cha kiroho kimeshakuvaa, mwisho wa siku utakufa na utaenda kuzimu kwenye majuto ya milele.
Hivyo usifurahie tu kusikia injili kila siku fahamu kuwa muda uliopewa unazidi kuyoyoma, usifurahie tu makala ya Neno la Mungu na hutaki kugeuka upo hatarini kukatwa.
Unapoamka na kuona jua tena, fahamu kuwa umepewa hiyo siku ili utengeneze maisha yako na Kristo, usifurahie tu kuona jua linachomoza na kuzama upo wakati ambao hautakuwa hivyo, wakati huo utatamani hata dakika moja lakini utakuwa umechelewa.
Hivyo saa ya wokovu ni sasa usiendelee kukawia kawia maana muda hakusubirii!! Neema ikishaondoka hairudigi tena, utakuwa kama hili Kanisa ambalo Kristo alilipa muda atubie uzinzi wake lakini akakataa kutubu na hatimaye likaachwa mpaka leo…haliwezi tena kubadilika.
Hivyo ni vema ukaitendea kazi neema ya Mungu, kwa kuizalia matunda unaposikia NENO lake kwa kumruhusu ayabadili maisha yako mapema angali wakati bado upo.
Mithali 28:13 inasema..” Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”
Tubu mgeukie Mungu ikali bado unao muda.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.