Umuhimu wa kuwa ndani ya Yesu.

Uncategorized No Comments

Umuhimu wa kuwa ndani ya Yesu.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana Yesu Kristo Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana.

Karibu tujifunze biblia kitabu cha uzima, na leo tutajifunza umuhimu wa kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. (Kuwa ndani ya Yesu).

Kwanza ndani ya Yesu kuna ulinzi. Na leo nitakuongezea chachu ya kuzama ndani ya Yesu zaidi.

Unapokuwa karibu na Mungu, yapo mabaya mengi kutoka kwa yule adui ambayo Mungu atukuepushanazo.

Kwa ufupi jua halitakupiga mchana, wala mwezi wakati wa usiku. Kama maandiko yasemavyo

Zaburi 121:5 ”BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume.

[6]Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.

[7]BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.

[8]BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”

Unaona umuhimu wa kuwa ndani ya Yesu, sehemu nyingine alisema..

Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, Ndivyo BWANA anavyowazunguka watu wake, Tangu sasa na hata milele.” (Zab 125:2).

Unapokuwa ndani ya Yesu, ondoa shaka kabisa na hofu ya kuogopa mtu yoyote au kuogopa wachawi, majini n.k fahamu kuwa we ni mwana wa Mungu na Baba ametuhakikishia ulinzi… hakuna chochote kitakachogusa.

Ni kweli wapo watu wanakuwangia kila siku, yapo mapepo yanatumwa kwako kila siku kukudhuru, wapo watu wanaotumiwa na Ibilisi kuharibu kazi yako, familia yako, elimu yako, afya yako n.k lakini fahamu kuwa lipo jeshi la malaika wa Mungu linakuzunguka. Unakumbuka ile habari ya Elisha na yule mtumishi wake Gehazi, Gehazi alipoona maadui waliojipanga kuwashambulia ni wengi akaogopa, lakini Elisha mtu wa Mungu alimsihi Bwana amfumbue macho, na alipofumbuliwa aliona jeshi kubwa la malaika wa Mungu limewazunguka..akapata nguvu na ujasiri.

2 Wafalme 6:15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?

[16]Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.

[17]Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.

Hauna haja ya kuangaika kwasababu ya watu wanaokuchukia, au kwasababu ya wachawi, au kwasababu ya kitu chochote. We mtazame Bwana na mwamini kuwa hawezi kukugeuzia kisogo, ukikutana na matatizo mbali mbali usikimbie huku na huku kulia. Afya yako au biashara yako ikiyumba kidogo usikimbilie mafuta ya upako, wala usihangaike na wanadamu wenzako na kuwaona kuwa ndio maadui, maadui zako ni shetani na dhambi, na kama mahusiano yako na Mungu yako vizuri..yanini kuwa na hofu..na Bwana ameshakuhakishia kuwa yupo karibu na wewe, hatasinzia wala hatalala usingizi (Zaburi 121:3-4)

Hivyo ukutanapo na changamoto yoyote fahamu kuwa haimanishi Mungu amekuacha, wapo wengi ambao walipitishwa kwenye hali kama yako na hata zaidi yako, angalia wakina Ayubu, na wengine wengi tu, walipitia hayo sio kwasababu walikuwa na dhambi, hapana..ni mapenzi ya Mungu tu yatimizwe. Hivyo na wewe leo ondoa presha na hofu ya maisha. Hakikisha tu mahusiano yako na Mungu yako vizuri, hayo mambo mengine muachie yeye.

Warumi 8:31 Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?

[32]Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?

Je! Upo ndani ya Yesu? Fahamu kuwa ukiwa nje ya Yesu hauwezi kushindana na adui, ni haki yako kuogopa wachawi, na majini, na kila namna ya matatizo. Lakini leo ukikubali kuzama ndani ya Yesu kweli kweli ukaacha ule uvuguvugu, nakuhakikishia kuwa utakuwa na furaha siku zote na hofu zote zitakimbia mbali na wewe, hata hofu ya kufa haitakutawala .. shetani na mapepo yake watapita mbali na wewe. Naam utapokea baraka zote za Mungu, atakayekubariki atabarikwa na atakaye kulaani atalaaniwa, na hakutakuwa na uchawi wala uganga juu yako kwasababu imeandikwa hakuna uchawi juu ya Yakobo. (Hesabu 23:23).

Na zaidi ya yote kuna ahadi ya uzima wa milele ndani ya Yesu.

Je! upo tayari sasa kumpokea?

Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo, na kutaka akuokoe na kukusamehe dhambi zako kabisa, Basi ni uamuzi wa busara sana ambao, utaufurahia maisha yako yote, kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Kumbuka..

-Kwa Yesu lipo tumaini la uzima wa milele.

-Kwa Yesu Unapata utulivu wa nafasi na faraja. Alisema.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

-Kwa Yesu zipo Baraka.

-Na kwa Yesu upo msahama wa kweli:

Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”.

Kwa hiyo unapokuja kwake leo hii kwa kumaanisha, ujue kuwa hiyo mizigo ya dhambi uliyonayo haijalishi ni mingi kiasi gani ataitua mara moja, haijalishi uliuwa watu wengi namna gani, haijalishi ulizini nje ya ndoa mara nyingi kiasi gani, haijalishi ulikwenda kwa waganga mara nyingi namna gani..Ikiwa tu upo tayari leo kumkaribisha Yesu moyoni mwako basi ataitua, na kukusamehe kabisa kana kwamba hakuna chochote ulichowahi kumkosea..Na atakupa amani.

Hivyo kama leo ni siku yako ya kuyasalimisha maisha yako kwake, jambo la kwanza unalopaswa kufahamu ni kwamba, unapaswa umaanishe kutoka katika moyo wako, kuwa kuanzia sasa, wewe na dhambi basi, wewe na ulimwengu basi kabisa..

Hivyo kama umeshakuwa tayari kufanya hivyo basi..

Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Hongera kwa kuokoka.

Hivyo ikiwa utahitaji msaada zaidi basi, wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *