Usichukie Kuambiwa ukweli
Upo usemi unaosema ”ukweli unauma” hilo ni kweli kabisa, ni watu wachache sana ambao wanaweza kupokea ukweli kama ilivyo hata kama unawakosoa, wengi huwa hawataki kuambiwa ukweli wa mienendo yao mibovu, tabia zao mbaya, udhaifu wao, kasoro zao.. na hali zao za kiroho.
Katika biblia tunasoma mtu mmoja ambaye aliambiwa ukweli wa mwenendo wake..lakini kwasababu ukweli unauma hakusubiria hata kusikiliza mpaka mwisho, Hebu tusome…
Yeremia 36:1-4,21-23,27-29 “Ikawa katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,
[2]Twaa gombo la chuo, ukaandike ndani yake maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, na juu ya Yuda, na juu ya mataifa yote, tangu siku ile niliponena nawe, tangu siku za Yosia, hata siku hii ya leo.
[3]Huenda nyumba ya Yuda watasikia mabaya yote niliyokusudia kuwatenda; wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya; nami nikawasamehe uovu wao na dhambi yao.
[4]Kisha Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; naye Baruku akaandika katika gombo la chuo maneno yote ya BWANA, yaliyotoka kinywani mwa Yeremia, ambayo BWANA amemwambia.
[22]Basi mfalme alikuwa ameketi katika nyumba iliyotumika wakati wa baridi, mwezi wa kenda; na pale palikuwa na moto wa makaa mbele yake.
[23]Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.
[27]Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, hapo mfalme alipokuwa amekwisha kuliteketeza gombo lile, na maneno yale aliyoyaandika Baruku, yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, kusema,
[28]Haya! Twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza.
[29]Na katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema, BWANA asema hivi, Umeliteketeza gombo hili, ukisema, Mbona umeandika ndani yake, ukisema, Bila shaka mfalme wa Babeli atakuja, na kuiharibu nchi hii, na kukomesha mwanadamu na mnyama pia ndani yake?
[30]Basi, BWANA asema hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi.
[31]Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, LAKINI HAWAKUKUBALI KUSIKILIZA.
Hata katika hizi siku za mwisho watu wengi hawataki kusikia injili ya kweli.. wanapenda injili za uongo zinazowafariji na kuwaambia uongo na ukweli nusu, japokuwa wao wenyewe wanajua ni uongo ila wanapenda hivyo hivyo.. kwasababu wanaasi sana.
Isaya 30:9-10 Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA;
[10]wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;
Ndiyo hali ilivyo sasaivi, watu hawataki kuambiwa ukweli, hawataki kufichuliwa maovu yao..wanataka wafunikwe funikwe, waambiwe maneno ya faraja, maneno malaini laini.
Ndugu yangu ni heri leo ukakubali maneno ya kweli hata kama yanauma..kwa maana lengo la kuambiwa ukweli ni ili usipotee, anayekuambia ukweli anakupenda.. Hivyo Mungu anatuambia ukweli mapema ili tusipotee maana yeye hapendi hata mtu mmoja apotee..ndio maana alimtoa mwanaye mpendwa “Yesu” ili kila mtu atakayemwamini asipotee, Bali awe na uzima wa milele.
Yohana 3:16-18 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
[17]Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.
[18]Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
Kwahiyo ukweli wa Mungu hapo ni kwamba ”Amwaminiye mwana hahukumiwi, asiyeamini amekwisha kuhukumiwa” sehemu nyingine anasema..
1 Yohana 5:10-12 Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe.
[11]Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.
[12]Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
Huo ndio ukweli, kwamba usipomwamini huyu Yesu na ukatubu dhambi zako..huna uzima wa milele bali ghadhabu ya Mungu ipo juu yako.
Yohana 3:36 Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.
Nami leo nakuambia ukweli, usipoacha uasherati, uzinzi, uchawi, ulevi, uzinzi, ukahaba, wizi, uongo, usengenyaji, kutukana, kujichua, kutazama picha chafu mitandaoni, kusikiliza miziki ya kidunia, kubeti, kuangalia mipira, filamu, kucheza magemu, kunyoa kiduku/denge, kujipamba kwa mapambo yoyote ile iwe ni hereni, mikufu, bangili, vipini, mekaup, lipustiks, wanja, wigi, kusuka, na kuweka kucha rangi, pamoja na kuvalia mavazi yaani vimini, kaptula, suruali kwa mwanamke, nguo zinazochora maumbile, fashions, na ulimwengu kwa ujumla.. usipokubali leo kuacha ulimwengu na tamaa zake.. ukaendelea kujidanganya kuwa umeokoka.. nataka nikuambie ukweli kulingana na biblia maneno ya Mungu ya kweli, hauwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Usidanganyike.
1 Wakorintho 6:9-10 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? MSIDANGANYIKE; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
[10]wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo NAWAAMBIA MAPEMA, kama nilivyokwisha kuwaambia, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU.
Sasa, ili usikose mbingu..ikiwa u miongoni mwa hao, kubali leo kumwamini Yesu Kristo na utubu dhambi zako zote na kumaanisha kabisa kuacha ulimwengu..kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu ili upokee zawadi ya Roho Mtakatifu (Roho wa Mungu) ambaye atakusaidia kushinda dhambi na ulimwengu kabisa.
Kumbuka ukweli ni kwamba usipodhamiria kutubu dhambi kwa kumaanisha kuacha kabisa na kuachana na udunia na kubatizwa ubatizo sahihi..na kupokea Roho wa Mungu, basi fahamu kuwa huwezi kuurithi ufalme wa Mungu kwa kuwa bado hujafanyika kiumbe kipya.
Yohana 3:3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
Huo ndio ukweli, na ndio upendo wa Mungu kwetu.. hivyo hutuna budi kuupokea ikiwa tunajipenda.. Lakini kama tumechagua kupotea katika hukumu ya milele, basi tunaweza tusipokee huu ukweli na tukaendelea na maisha yetu ya dhambi huku tukujidanganya na kujifariji kwa maneno ya uongo.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.