Usijifiche chini ya maneno yasiyo kweli.

Uncategorized No Comments

Usijifiche chini ya maneno yasiyo kweli.

Isaya 28:15-19 “Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana TUMEFANYA MANENO YA UONGO KUWA KIMBILIO LETU, TUMEJIFICHA CHINI YA MANENO YASIYO KWELI;

[16]kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.

[17]Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri.

[18]Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.

[19]Kila wakati litakapopita litawachukueni. Maana litapita asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku; na kuifahamu habari ile kutakuwa kitisho tu”.

Wapo watu wanaosema mtu akishaokolewa ameokolewa hata akifanya dhambi hawezi kwenda motoni (Once saved, always saved), wengine wanasema tunaishi kwa neema hivyo kuishi utakatifu ni sheria na hivyo mtu anaweza kuishi tu atakavyo, na wengine wanasema Mungu haangalii mwili anaangalia moyo tu!. Wengine wanadai Mungu ni mmoja lakini kila mtu ana njia yake ya kumwabudu, wengine wanasema ukishika amri kumi zote inatosha kumpendeza Mungu, wengine wanafundishwa na wanaamini kuwa kuna nafasi ya pili kuokolewa baada kifo, N.k n.k

Hayo ni maneno ambayo shetani ameyatengeneza ili kuwafanya wengi wakose mbingu na mwisho waende jehanumu.

Na watu wengi wapo kuzimu kwasababu ya maneno haya ya uongo,

Ndugu, Dada acha kujificha chini ya maneno yasiyo kweli, fahamu kuwa Neno la Mungu linasema pasipo utakatifu hakuna atakayemuona (Waebrania 12:14), na hakuna nafasi ya pili ya kuokoka baada ya kufa soma Waebrania 9:27.

Utakatifu sio sheria, ni jambo linalotoka ndani ya mtu. Huwezi kusema unakula kwasababu ni sheria kula hapana!, ni jambo linalotoka ndani.. bila kula huwezi kuishi na hakuna mtu anayejilazimisha kula labda awe anaumwa.

Na vivyo hivyo utakatifu ni maisha ya kila mwamini aliyeokoka kweli kweli..bila utakatifu huwezi kuwa hai rohoni, na ukiona unashindwa kuishi utakatifu au unaishi kwa shida/unajilazimisja ujue kuwa kuna shida katika wokovu wako, yakupasa uangalie ulivyosikia na kupokea.

Na utakatifu kamili ni ule wa ndani na nje, ukiona watu wanasema Mungu anaangalia moyo haangalii mwili ujue hata ndani yao kumeoza, kwasababu Bwana Yesu alisema kimtokacho mtu ndicho kimjazacho moyoni mwake na hayo ndio yanayotia mtu unajisi. (Marko 7:20) Na tena Neno la Mungu linasema katika…

Ayubu 14:4 Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye.

Umeona, huwezi kuwa safi mwilini ingali moyoni mwako umebeba mawazo mabaya, tamaa mbaya, uzinzi, kiburi, n.k kwasababu kila kitu kinaanzia ndani. Ulivyo nje ndivyo ulivyo ndani.

Sasa ni kwa jinsi gani Mungu anaweza kuangalia moyo uliojaa uasherati, usengenyaji, na mambo yote mabaya.

Hebu jiulize kwanini umejipodaoa namna hiyo, kwanini umevaa hivyo vitu bandia (hayo manywele bandia, hizo bangili/hereni, vipuli, kucha bandia) na Neno la Mungu linasema kujipamba kwenu kusiwe kwa nje (1Petro 3:3).

Nikuulize wewe dada uliyevaa suruali, vimini, nguo za kubana kwanini umevaa hivyo na unajua ni machukizo kwa Mungu? Kwanini umesuka nywele zako, kwanini umepaka kucha zako rangi? Je! hayo yote sio yameanzia moyoni mwako? Sio kwamba umetamani kuonekana na watu fulani sindiyo!. huo Ndio ukweli. Ndio maana leo unajificha chini ya maneno yasiyo kweli na kusema Mungu haangalii mwili anaangalia moyo.

Hebu acha kujidanganya, leo amua kuachia hayo maneno ya uongo..tubu na uamue kuokoka kweli kweli.

Acha kujidanganya kuwa tunaishi kwa neema kwahiyo naishi navyotaka, fahamu kuwa neema haikubaliani na uovu wala tamaa za udunia ( Soma Tito 2:11-12)

Acha kujidanganya kuwa matendo yako yatakuokoa ingali hauna Roho Mtakatifu biblia inasema wasio na Roho wa Kristo sio wake (Warumi 8:9), acha kujidanganya kuwa utaokolewa kwasababu unashika amri kumi na huku umeacha amri kuu (upendo), fahamu kuwa pasipo upendo wewe sio kitu haijalishi unafanya nini kizuri kwa Mungu Soma 1Wakorintho13).

1 Wakorintho 6:9 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? MSIDANGANYIKE; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

[10]wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.

Acha kutumainia maneno ya uongo, acha kujificha chini ya maneno yasiyo kweli. (Jehanumu ya moto ipo).

Tubu dhambi zako mgeukie YESU leo akuokoe kwa maana tunaishi ukingoni mwa nyakati na unyakuo upo karibu sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *