Usijigeuze na kuvaa mavazi mengine.

Biblia kwa kina No Comments

Usijigeuze na kuvaa mavazi mengine.

Katika biblia tunamsoma mfalme mmoja wa Israeli ambaye alijigeuza na kuvaa mavazi mengine..na huyu si mwingine zaidi ya Sauli, na lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni yeye asijulikane na kule anakokwenda kwa yule mwanamke mchawi. Tunasoma..

1 Samweli 28:8 Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako.

Tatizo kubwa tulilonalo wakristo ni tatizo la uvuguvugu na hili litawapelekea wengi kutapikwa siku ile, kwa sababu Bwana anasema..

Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

[16]Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.” (Ufunuo 3:15-16)

Matendo yetu ndiyo mavazi yetu (Ufunuo 19:8), na mavazi yetu yanapaswa yawe masafi wakati wowote mpaka siku ya parapanda ya mwisho. Laikini leo hii katika siku hizi za mwisho kabisa, wengi waliokuwa wakristo wa kweli wanajigeuza na kuvaa mavazi mengine ya kiulimwengu.

Kumbuka hapa sizungumzii wale wakristo wanaotembea barabarani na vimini na masuruali au wale ambao wanafanya uasherati na uzinzi kwa siri..halafu jumapili wanavaa vizuri wanaenda kanisani, wakitoka hapo wanajigeuza na kuvaa mavazi yao ya uzinzi, na uchawi.. hapana’, hatuwazunguzii hao na biblia inaposema wakristo vuguvugu haizungumzii kundi hilo.. maana hao sio wakristo! Hao ni washabiki tu wa Kristo (wakristo jina). Kwahiyo hapa tunawazungumzia wakristo wa kweli kabisa.

Mkristo wa kweli ni yule aliyejikana nafsi na kujiwika msalaba wake na kumfuata Yesu, maana yake mkristo aliyeacha ulimwengu na mambo yote ya kidunia…vile vile akabatizwa kwa usahihi na akapokea Roho Mtakatifu. Huyu ndiye mkristo tunayemzungumzia hapa, na ujumbe wa leo unalenga wakristo wa namna hii.

Usijigeuze na kuvaa mavazi mengine!

Mavazi mengine ni yapi? Kama tulivyoona mavazi ya wakristo ni matendo yao. Na matendo yetu yanapaswa yang’are siku zote tuwapo hapa duniani ili wale walipo gizani wavutwe na matendo yetu kama vile nuru ivutayo wadudu gizani.

Ufunuo wa Yohana 19:7-8 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

[8]Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, INGA’ARAYO, SAFI; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. (Soma pia Mathayo 5:14-16).

Kitani inayozungumziwa hapo ni “vazi zuri refu la thamani na leupe”…Hivyo hilo ndio vazi la utu wetu wa ndani na utu wa nje.

Sasa ili tufahamu hayo mavazi mengine ambayo hayapaswi tugeukie, hebu tutazame hayo mavazi ambayo sisi kama wakristo tunapaswa tuyavae siku zote. (Kumbuka mavazi ni matendo yetu).

Yapo mavazi ya nje na ndani.

Mavazi ya nje.

Mavazi ya nje ni yapi?. Ni mwonekano wako wote wa nje kwa ujumla,. Ikiwemo kujistiri kwako, kujipamba kwako, kutenda kwako, kutembea kwako n.k, na hapa ndipo tunaanza kuwatenga magugu na ngano, hapa hatuhitaji kukuchunguza sana kama we ni mkristo au ni mshabiki tu, kwasababu muonekano wako tu unakutambulisha, huwezi ukawa unavaa vimini..wewe ni mwanamke unavaa suruali (mavazi ya kiume), unavaa nguo zinazochora maungo yako, unajipodoa na takatataka zote, halafu tukasema wewe ni mkristo, unatazama picha chafu mitandaoni, unacheza kamari, magemu, unasikiliza miziki ya kidunia, unajihusisha na mahusiano ya kiholelaholela, unatumia madawa ya kulevya sigara, pombe n.k, unapiga punyeto, unajihusisha na uganga na matendo yote ya giza..halafu ukatuambia wewe ni mkristo na umeokoka unampenda Yesu.. ndugu utakuwa unajidanganya mwenyewe na unajipotezea muda, huo sio ukristo na bado hujaokoka… unahitaji kutubu dhambi zako na kumpa Yesu maisha yako..hata kama wewe ni mchungaji, nabii, mwana kwaya, unahitaji neema ya wokovu. Hivyo mkristo wa kweli ni lazima aonyeshe tofauti na watu kiulimwengu.. kupitia muonekano wake wa nje.

Mavazi ya ndani

Mavazi ya ndani ni matendo yetu ya ndani (ndani ya mioyo yetu), Sasa hebu tujifunze mavazi hayo ya ndani ni yapi…

Wakolosai 3:12 “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa REHEMA, UTU WEMA, UNYENYEKEVU, UPOLE, UVUMILIVU,

13 mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

14 Zaidi ya hayo yote JIVIKENI UPENDO, ndio kifungo cha ukamilifu”.

Hapo Biblia inatumia neno “JIVIKENI” Ikiwa na maana kuwa mambo yafuatayo yanafananishwa na mavazi.. na anayataja pale kuwa ni moyo wa Rehema, Utu wema, Unyenyekevu, Upole, Uvumilivu na mwisho anamaliza na Upendo, tutazame moyo baada ya lingine.

1. REHEMA.

Hapo anataja moyo wa rehema,  Mtu mwenye moyo wa rehema wakati wote atajishusha mbele za Mungu, na kujitakasa, kamwe hawezi kujiona ni bora mbele za Mungu, na pia mtu mwenye rehema siku zote atakuwa ni mtu wa kuwarehemu wengine, kuwasamehe na kuachia, kwahiyo nasi hatuna budi kujivika moyo huo wa rehema kila siku.

2. UTU WEMA.

Hapa anasema “Utu” maana yake ni “jambo la ndani” sio nje. Mfano wa Utu ulio mwema ni ule aliokuwa nao Yule Msamaria, ambaye alimwona mtu Yule kaangukia mikononi mwa wanyang’anyi akaenda  kumsaidia kwa moyo wote Luka 10:30-37. Nasi lazima tulivae hili vazi la Utu wema (2Wakorintho 6:6)

3. UNYENYEKEVU.

Unyenyekevu ni hali ya kujishusha,  na kinyume cha unyenyekevu ni kiburi na majivuno, ili tuhesabike tumesitirika kiroho ni lazima tujivike vazi hili la unyenyekevu 1Petro 5:5.

4. UPOLE.

Anasema “Upole” na si “Unyonge”.. Unyonge ni ile hali ya kuwa mtulivu kwasababu ya hofu, au hali Fulani..lakini upole ni hali ya kuwa mtulivu si kwasababu unashindwa kurudisha majibu au kufanya jambo..uwezo wote unakuwa unao lakini hufanyi hivyo, kama alivyokuwa Bwana wetu Yesu, yeye alikuwa na uwezo wa kushusha moto kwa wasamaria lakini hakufanya hivyo.. nasi ni lazima tujivike hili vazi. (Mathayo 11:29)

5. UVUMILIVU.

Uvumilivu ni uwezo wa ndani wa kustahimili jambo baya, laweza kuwa shutuma, mapigo, au jambo jingine lolote, uwezo huo ni muhimu sana sisi wakristo kuwa nao.

Yakobo 5:10 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.

11 Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma”.

6. UPENDO.

Hapa anasema kuwa hiki ndicho kifungo cha ukamilifu.. Maana yake tukiwa na upendo ni sawa na mtu aliyevaa shati sasa anamalizia kuvaa koti juu yake na kufunga vifungo vyake, na tena Biblia inasema pasipo upendo sisi si kitu haijalishi tunanena kwa lugha au tunafanya ishara (1Wakorintho 13:1).

Kwahiyo hayo ndio mavazi tunayopaswa kuyavaa katika utu wetu wa ndani kila siku, na utaona pia yamerudiwa katika Wagalatia 5:22 kama matunda ya roho, na mengine baadhi kuongezeka.

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Ujumbe wa leo unasema ”usijigeuze na kuvaa mavazi mengine ” ikiwa na maana kama kweli umeokoka kweli kweli na umevaa mavazi yote ya ndani na nje, basi hupaswi kujigeuza na kuvaa mavazi mengine. Mavazi mengine ni mavazi mengine kinyume na hayo. Kwa mfano ulikuwa mtu wa kusamehe lakini umejigeuza na kuwa mtu wa vinyongo, visasi, hasira n.k hilo sio vazi lako, ulikuwa unampenda Mungu kwa moyo wako wote na roho yako yote lakini umeacha upendo wako wa kwanza umegeukia kupenda ulimwengu… maana yake unavaa vazi ambalo sio lako, ulikuwa unapenda maombi, kusoma biblia, kushuhudia, lakini leo hata kuomba lisaa limoja kwa siku huwezi, hukumbuki hata ni lini umekesha kuomba.. umejigeuza na kuvaa mavazi mengine. Na huo ndio uvuguvugu.

Ulikuwa unapenda mafundisho ya utakatifu lakini umejigeuza na kuvaa mafundisho ya kichawi kama Sauli alivyojigeuza na kuvaa mavazi mengine ili atafute uchawi, mafundisho yote yanayokuhubiria tu vitu vya ulimwengu huu kama kuwa na mali tu, ndoa nzuri, uchumi na mafanikio ya kidunia tu pasipo kutanguliza utakatifu kwanza, hayo ni mafundisho ya kichawi (mavazi mengine) ambayo mwisho yanakufanya uwe vuguvugu na hatimaye ukose mbingu.

Mafundisho yanayokuhubiria kuwa Mungu anaangalia tu moyo haangalii mwili, Kwahiyo vaa utakavyo, hayo ni mafundisho ya mashetani. Hivyo hupaswi kuyageukia kabisa (kimbia), usijigeuze na kuvaa mavazi mengine. Dumu katika utakatifu maana karamu ya Mwana-kondoo imekaribia, TUNZA MAVAZI YAKO.

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”

Maranatha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *