Usimpelekee Bwana mashitaka ya maadui zako.
Moja ya jambo ambalo linamchukiza sana Mungu ni maombi ya kuwaombea wanadamu wenzetu mabaya, hili linamchukiza sana na linaleta adhabu kwetu badala ya mazuri.
Maombi ya kuwashitaki ndugu zetu kama maadui ni maombi mabaya sana, hata kama ni kweli wametuumiza.
Hebu fikiria wewe ulipokuwa unawangia watu, unaiba vitu vya watu, ulipokuwa msengenyaji, n.k halafu Mungu anakutazama tu bila kukufanyia lolote baya, hebu fikiria leo unapoenda mbele za Mungu na kumwambia Mungu adui zako wapigwe wapotee kabisa, wauliwe, wafe kabisa wasipone….hebu wazia jambo hilo vizuri.
Ni wazi kuwa Mungu angekuwa anapokea hayo maombi hata na wewe usingekuwepo leo kwasababu hayo hayo ambayo unafanyiwa leo ulishawahi kuwafanyia watu huko nyuma. Hebu fikiri ni mara ngapi ulifungua mdomo wako kulaani, au kutukana, au ni mara ngapi ulimuwazia mtu mabaya, ni mara nyingi sana!! Sasa kwanini leo hii unampelekea Mungu mashitaka ya ndugu zako? Kwanini usitumie hiyo nafasi kumsihi Mungu awabadilishe, awape neema ya wokovu.
Na wakiokoka, hao hao ambao leo wanakufanyia hayo mabaya mbona watakuwa marafiki zako tu. Kwahiyo wewe kama mkristo..acha hiyo tabia ya kumpelekea Bwana mashitaka ya wanadamu wenzako, maadui zetu ni ibilisi na mapepo yake, ndio ambao tumembiwa tuvae silaha za vita ili tuweze kushindana nao na wala sio wanadamu wenzetu.
Watu wengi ambao wanaomba maombi ya namna hiyo…wanaishia kupatwa na mabaya kinyume na walivyotarajia. Ndipo kilichowakuta wale watu ambao walimpelekea Daudi taarifa ya kuawa kwa maadui wa Daudi… wakidhani wanampendeza Daudi kumbe wanamchukiza..na hatima yao ni wao pia kuuliwa, na ndivyo ilivyo kwa watu wanaompelekea Bwana mashitaka ya maadui zao.
2 Samweli 4:8-12 Wakamletea Daudi kichwa cha Ishboshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, Tazama, hiki ni kichwa cha Ishboshethi, mwana wa Sauli, adui yako, aliyekutafuta roho yako; BWANA amemlipia kisasi bwana wangu mfalme hivi leo, juu ya Sauli, na juu ya wazao wake.
[9]Naye Daudi akawajibu Rekabu na Baana, nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akawaambia, Aishivyo BWANA, aliyenihifadhi roho yangu katika shida zote,
[10]mtu mmoja aliponiambia, akasema, Tazama, Sauli amekufa, akidhani ya kuwa ameleta habari njema, nalimshika, nikamwua, huko Siklagi, ndio ujira niliompa kwa habari zake.
[11]Basi, iwapo watu waovu wamemwua mtu mwenye haki kitandani mwake, je! Sasa nisitake zaidi damu yake mikononi mwenu, na kuwaondoa ninyi katika nchi?
[12]Ndipo Daudi akawaagiza vijana wake, wakawaua, wakawakata mikono na miguu, wakawatundika kando ya ziwa katika Hebroni. Nao wakakitwaa kichwa cha Ishboshethi wakakizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.
Umeona hapo; hebu anza leo kubadilisha huo mtazamo wako wa kuwaona wanadamu wenzako kama maadui. Anza kuwaona kwa jicho lingine kwamba ni dhambi ikayo ndani yao ndio inawafanya wakufanyie hayo mabaya, ndio inawafanya wakuchukie n.k. kwahiyo badala ya kushindanao, we shida na hiyo dhambi kwa kuwaombea na kuwahubiria habari njema za wokovu.. kama unaweza kufanya hivyo. Halikadhalika vunja nguvu zote adui ibilisi inayotenda kazi ndani yao. Na Bwana atakubariki.
Warumi 12:17-21 Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.
[18]Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.
[19]Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.
[20]Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.
[21]Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Je! umeokoka kweli kweli? Kama bado hujaokoka fahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa nyakati na Yesu yupo mlangoni kurudi. Hivyo ni heri leo ukachukua uamuzi binafsi wa kubadilisha maisha yako na kuacha maisha ya dhambi na udunia, umgeukie Yesu ili uokolewe na hukumu ya ziwa la moto.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.