Usitoe sadaka yenye kasoro mbele za Mungu

Maswali ya Biblia No Comments

 

Bwana Yesu Kristo asifiwe, karibu tujifunze maandiko Matakatifu ili tuzidi kumjua Mungu wetu katika kila namna.. ingali bado tunapumua.

Siku ya leo tutaenda kujifunza umuhimu wa kumtolea Mungu sadaka isiyo na kasoro yoyote..

Upo umuhimu mkubwa sana wa kumtolea Mungu vitu vyenye hadhi ya hali ya juu ambavyo vinamgharimu mtu hadi kuvitoa. Tusitoe tu kwa mazoea ilimradi tunatoa, Mungu wetu ni Mungu mwenye hekima nyingi zaidi yetu, ana uwezo wa kuchunguza nafsi zetu kwa undani zaidi. kwa mfano wewe unapopokea zawadi fulani..halafu ukaja ukajua kuwa zawadi uliyoipokea ilikuwa haijakusudiwa uipokee,

Ila umepokea baada ya yule aliyekusudiwa kukosekana ndipo wewe ukapewa, bila shaka hautafurahia sana zaidi ya ile ambayo ilikusudiwa moja kwa moja kwako, ila ile ambayo unakuja kupewa baada ya kukosekana kwa mlengwa ndipo unapewa hautapendezwa nayo sana, zawadi umepokea kweli, na ni jambo zuri na la kushukuru, hata kwa hicho ulichopokea, lakini ile zawadi ingekuwa na heshima zaidi endapo ingeelekezwa kwako moja kwa moja. Sasa Kama sisi wanadamu tuna hisia kama hizo..Si zaidi Mungu naye kutofurahia sadaka za namna hiyo ambayo ni kama masalia.

Mungu anapendezwa na matoleo ambayo mtu tayari alishapanga kutoa na si kutoa kile ambacho tumebakiza baada ya matumizi yetu, hafurahishwi kuwekwa wa pili…Kumfanya wa pili ni kutomheshimu na kumjali tena ni dharau kubwa…

Mungu haangalii wingi wa matoleo yetu bali anaangalia zaidi ubora wa ile sadaka. Sadaka unayomtolea ina thamani kiasi gani..je! ni kwa kiasi gani inagusa moyo wake? umegharamikia kiasi gani? hata kama ni sh.50 lakini haikuwa mabaki ama chenji uliyobakiwanayo baada ya matumizi yako.

Wakati wa Torati ya Musa ambapo matoleo yalihusisha uchinjaji wa wanyama…Mungu alitoa amri kuwa wasije wakatoa wanyama wenye kasoro yoyote mfano vilema, wagonjwa, n.k,

Mtu akitoa mnyama yoyote mwenye hitilafu au udhaifu wowote mfano mwenye kasoro ya macho(chongo), mwenye shida ya ulemavu wa aina yoyote ni dhambi, au kutoa mnyama ambaye amewahi kurekodiwa kuwa na sifa mbaya labda ya kumsababishia mtu kifo, au kuua mnyama mwingine ilikuwa ni dhambi kumtolea Mungu wanyama kama hao kama sadaka….

Walawi 22: 20 “Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu”

Pia maandiko yanaendele kuthibitisha juu ya hilo…soma

Kumbukumbu 17:1“Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng’ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako”

Pia na…

Malaki 1:13 “Tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatikana kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je! Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana.

14 Lakini na alaaniwe mtu mwenye kudanganya, ambaye katika kundi lake ana mume, akaweka nadhiri, ila amtolea Bwana kitu kilicho na kilema; kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa”.

Wakati wa agano la kale sheria haikuruhusu hata kutoka nje na kwenda kununua mnyama wa mtu usiyemfahamu.. ni kwasababu huwezi kujua historia ya huyo mnyama labda alikuwa na tatizo fulani huko nyuma.. pengine alishaleta maafa ya kuua watu au wanyama wenzake utawezaje kujua!..

kwahiyo ili kuepuka kumtolea Mungu mnyama mwenye hitilafu ilimbidi mtu aingie kwenye zizi lake mwenyewe au aende kwa mtu anayemfahamu na anajulikana kuaminika na watu kwa uaminifu wake.

Je! Umewahi kufikiri kwamba kwanini ile siku Bwana Yesu alipoingia hekaluni biblia inasema alikuta watu wanauza ng’ombe, mbuzi, na njiwa, na kwanini hajawakuta labda wakiuza vitunguu, nyanya, mizabibu,tini, na matunda mengine, au vitenge, mashati, magauni, makoti, mikanda,au nguo zozote na vyakula mbali mbali?. Hebu tusome…

Yohana 2:13 “Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.

14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi”

Unaelewa sababu?. Ni kwasababu hii, watu walikuwa wanatoka sehemu za mbali..wengine walitoka mataifa ya mbali sana Kwahiyo ikawapelekea kuona uvivu wa kwenda huku na huku kutafuta mnyama asiye na kosoro wala hitilafu yoyote,….

Wakaona ni jambo ambalo litawagharimu kutumia muda mwingi na kiasi kikubwa cha fedha kutafuta hawa wanyama wenye hadhi na ubora mkubwa..wasio na lawama yoyote, tena wakiangalia na gharama ya kumsafirisha huko na kumleta hekaluni kwa Mungu ili awe sadaka ya kuteketezwa ni kubwa.

Kwahiyo ikawabidi watumie njia fupi isiyo na miangaiko na isiyotumia gharama ili kupata hao wanyama maeneo ya karibu na hekaluni,..hiyo ikawafanya watu wengine wafanya biashara..watu wa mataifa watumie hiyo fursa na kupeleka mifugo yao kwenda kuuza huko hekaluni..jambo ambalo liligeuza hekalu la Mungu kuwa mnada wa kuuzia mifugo, watu wengine walileta mifugo yenye kasoro ambayo ni machukizo mbele za Mungu,..

Mfano mifugo ya wizi, wenye magonjwa yasiyoonyesha dalili, n.k, maadamu tu wamenona..dhumuni ni kupata tu fedha, kwahiyo hawakujalisha tena kufuatilia kumbukumbu ya mnyama, pengine huyo mnyama labda alifanya tukio nyuma baya,.. pengine alihusika kwenye mauwaji, au hata alilala na mwanadamu…halafu anapelekwa kutumika kwenye nyumba ya Mungu.. jambo ambalo ni machukizo makubwa, kwahiyo kwa jinsi hiyo nyumba ya Mungu ikawa kama soko…watu wakageuza kuwa sehemu pa kupatia fedha bila kujalisha ni aina gani ya mifugo wanapeleka hapo,..

Michanganyiko ya watu mbalimbali ikatokea ndani ya nyumba ya Mungu.. pengine hata vibaka,majambazi, na biashara nyingine zikaibuka huko ndani,..nani anajali tena, ilimradi tu watu wanaingiza fedha, si ajabu hata kuna watu walikuwa wanacheza kamari huko kwenye nyumba ya Mungu,

Na kwasababu Wayahudi wanaoenda huko kumtolea Mungu walitokea mbali..hawakutaka tena kujiangaisha na kuingia gharama ya kutafuta wanyama walio safi kwa Mungu,.. Hivyo wakakubali kuuziwa na watu wa mataifa wanyama ambao ni machukizo mbele za Mungu, ambao hawajulikani hata walikotoka wana usalama gani,..

Kwahiyo wakawa wanatoka manyumbani mwao mikono mitupu wakijua wakifika hekaluni kuna wanyama wa kununua,..hivyo wakifika maeneo karibu na hekaluni wananunua hao wanyama halafu wanaingiza ndani ya nyumba ya Bwana…

Makuhani wanapokea na kutoa sadaka ya kuteketezwa bila kujali ubora na usafi wa huyo mnyama,.. baadaye wakishatoa wanarudi zao makwao wakidhani tayari Mungu amepokea sadaka zao na kuwabariki,..kumbe wameenda kumchukiza Mungu na kupokea laana,.. wenyewe wanafikiri wanachokifanya kinampendeza Mungu na kinamfurahisha wasijue kuwa wamemvunjia Mungu heshima na kumdharau ni heri hata wasingetoa kabisa,.. Ndio sababu Bwana Yesu aliwatoa wote waliokuwa wakiuza hao wanyama huko hekaluni,.. kwasababu walichokuwa wakifanya ilikuwa ni machukizo makubwa sana.

Jiulize leo ndugu, je! sadaka yako unayomtolea Mungu kila siku, unaipa uthamani gani!. je! ni kweli haina hitilafu yoyote mbele za Mungu,..chunguza sadaka zako kabla hujamtolea Mungu,..isiwe imetokana na mapato ya dhuluma, au imetoka kwenye njia za wizi, au biashara haramu kama kuuza pombe, sigara,madawa ya kulevya, kujiuza, kubeti, rushwa, n.k,

Sadaka zilizotoka kati ya njia hizo ni machukizo mbele za Mungu,..ni heri usitoe kabisa,..vile vile kama sadaka unazomtolea Mungu ni vichenji chenji vilizosalia baada ya kufanya matumizi yako usimtolea Mungu kabisa…kama unaona shida kupanga kumtolea Mungu sadaka yako kabla hujapanga matumizi yako..na ukaenda kufanya kwanza manunuzi kisha unamletea Mungu masalia…ni heri usitoe kabisa, Mungu si wa kupelekewa makombo huko ni kumdharau Mungu…na kutafuta laana badala ya baraka,

Pia unapomtolea Mungu na wewe mwenyewe njia zako haziko sawa kwake…. tayari unamchukiza Mungu huku ukidhani yeye anakufurahia..Kwani neno lake linasema…

Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana..”

Kumbuka ni haya mambo tu ya utoaji ndiyo ilimpelekea Anania na Safira mkewe kupoteza uhai.. baada ya kuuza kiwanja na wakapanga kumtolea Mungu kiasi chote cha fedha walichouzia kiwanja,..

Tunasoma baada ya kuuza kiwanja Anania akaenda kumtolea Mungu chenji huku fedha nyingine kazuilia kwenye matumizi yake..kilichompata ni yeye na mke wake walikufa..na habari hiyo tunaipata kwenye agano jipya sio agano la kale,.. soma Matendo 5:1-11

Kwahiyo kama unataka kumtolea Mungu na kubarikiwa zaidi toa kile kinachokugharimu ambayo hata we mwenyewe itakugusa… Mtolee Mungu sadaka isiyo na hitilafu yoyote na tena iliyo ya thamani kubwa ambayo hata mtu mwingine akikukuona atakushangaa sana na kukuona umerukwa na akili..

Ndivyo sadaka yako itaenda kugusa moyo wa Mungu na Mungu ataona umemheshimu sana…na Kamwe hataacha kukubariki na kukuinua..hakikisha tu sadaka unayotoa ni ya halali.. haina kasoro yoyote,..na we mwenyewe ni msafi mbele za Mungu.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *