
Usiwe miongoni mwa makutano wanaofuata Yesu.
Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu..
Kipindi Bwana wetu Yesu alipokuwa hapa duniani, kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wakimfuata, hawa walikuwa tu wanakusanyika kusikiliza mahubiri ya Bwana Yesu ambao mara zote Bwana alikuwa anazungumza nao kwa mifano, na kuwaponya magonjwa yao..baada ya hapo walikuwa wanarejea katika shughuli zao na maisha yao ya kawaida.
Lakini ilifika kipindi Bwana akawageukia na kuwaambia..
Luka 14:25-27 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,
[26]Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.
[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.
Maana yake hao watu walidhani kufuatana na Yesu namna hiyo ndiyo wameshafika, walidhani kwenda kumsikiliza tu maneno yake na kuponywa matatizo yao ndio tayari wamekuwa wanafunzi wake, lakini Bwana aliwaambia vigezo vya kuwa mwanafunzi wake ni kumchukia baba, mama, mke, watoto, ndugu na hata nafsi yake, na kubeba msalaba wake.
Na ukisoma biblia, utagundua ni kundi dogo tu la watu kati ya lile kundi kubwa walikubali kuwa wanafunzi wa Yesu, ni watu 120 tu wakiwemo na wale mitume 12 (Matendo 1:15)
Wengi waliogopa kuingia gharama ya kuwa mwanafunzi, hivyo wakabaki tu kufuatana naye kwa faida zao.
Na hata leo lipo kundi kubwa la watu wanaomfuata Yesu kwa maslahi yao wenyewe, hawataki kuingia gharama ya kuwa wanafunzi wake, wanadhani kwa kuhudhuria kanisani kila siku na kusikiliza mafundisho, na kuponywa shida zao ndio tayari wamekuwa wanafunzi wa Yesu, lakini maneno ya Bwana ni yale yale..
”kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.
Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.
Na maana nyingine ya kuwa mwanafunzi wa Yesu ni kuwa Mkristo kama tunavyosoma katika..
Matendo ya Mitume 11:26 “hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. NA WANAFUNZI WALIITWA WAKRISTO KWANZA HAPO ANTIOKIA.”
Kwahiyo badala ya kutumia hilo neno mwanafunzi tunaweza tukasema mtu yoyote asiye kidhi vigezo hivyo HAWEZI KUWA MKRISTO, hatuongezi wala kupunguza lakini tunasema ukweli ulivyo kulingana na biblia yenyewe inavyojijibu.
Kwahiyo kusema tu mimi ni mkristo nimeokoka kisa unaenda kanisani, unahudumu madhabahuni, unatoa sadaka, au unakemea mapepo hiyo sio tija. Je! we ni mwanafunzi wa Yesu?
Maana yake kama hujafanyika mwanafunzi wa Kristo..haijalishi utakiri kuwa umeokoka mara ngapi bado we sio mkristo, kwasababu kuwa mkristo ni kuwa mwanafunzi wa Kristo.
Na vigezo vya kuwa mkristo/mwanafunzi ni kuacha vyote kama Bwana alivyosema..
Luka 14:33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”
Sasa nini maana ya kuacha vyote na kuchukia ndugu, wazazi, watoto n.k, ikiwa ndio vigezo vya kuwa Mkristo.
Chuki inayozungumziwa hapo sio chuki ile ya dhambi, kwamba umchukie Baba yako au mama yako kwa nia ya kumdhuru, au kumdharau, au kumshushia heshima hapana! Bali chuki inayozungumziwa hapo ni “kuyachukia mapenzi yake ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu”…Baba anakuambia mwanangu tunapaswa tuende kwa waganga na wewe hali unajua kuwa hayo ni machukizo kwa Mungu, hapo unapaswa uyachukie hayo mapenzi ya Baba yako na kumwambia wazi kwa ujasiri kuwa “Baba mimi siwezi kwenda huko, kwasababu ni Mkristo, namwabudu Mungu aliye mbinguni”..
Mama yako anakwambia ukajiuze tupate pesa, wewe unatakiwa umwambie wazi kuwa “mimi siwezi kufanya hivyo kwasababu ni Mkristo”..Mume wako anakuambia ufanye mambo machafu ambayo ni machukizo kwa Mungu, na anakulazimisha, kutenda dhambi.. hapo unapaswa kumweleza wazi msimamo wako kwamba wewe ni Mkristo, na kama hataki kuishi na wewe, basi anayoruhusa ya kuondoka!…Biblia imeruhusu matengano Katika mazingira kama hayo (soma 1Wakorintho 7:15).
Pia mtu asiyeacha vyote alivyonavyo…Maana ya kuacha vyote ulivyo navyo ni kuvitoa vile vitu ndani ya moyo wako…kila mtu anafahamu namna ya kukitoa kitu moyoni, hakuna haja ya kuelezea… “unapotoa kitu moyoni, unakuwa unakifuta ndani yako, kinakuwa sio kitu tena kinachokupa raha, kiwepo kisiwepo ni sawa tu” Wakati mwingine hiyo hali inaweza kuambatana na kuviacha vitu kwa nje kabisa wazi wazi…
Ulikuwa ni Tajiri unauacha utajiri wako unamfuata Yesu, maana yake…Hata mali zote zikipukutika katika safari yako ya kumfuata YESU hilo hujali, kwasababu hazipo tena moyoni mwako, Unamhisi Yesu moyoni kuliko utajiri ulionao…Na pia unakuwa humfuati Yesu ili akupe mali au azilinde mali zako, unamfuata kwasababu Moyoni mwako unaona una haja naye…Kuna upendo fulani ambao unamiminika ndani yako ambao hauwezi kuuelezea, Unajikuta tu unampenda tu Yesu bila sababu kama yeye anavyokupenda wewe bila sababu yoyote.
Kadhalika Ulikuwa ni MASKINI, unauacha Umaskini wako unamfuata YESU. Unauondoa umaskini moyoni mwako….Usimfuate Yesu kwasababu hauna gari! Au kwasababu umaskini unakutesa na kukuumiza… Hapo hujajikana nafsi ndugu! Usimfuate Yesu kwasababu unataka utajiri, au unataka heshima katika jamii, au kwasababu unataka kuwakomesha maadui..Unatakiwa Uuache umaskini wako ndipo unamfuata Yesu kiasi kwamba hata katika safari yako ya Imani, ukiongezekewa na kuwa Tajiri wa mambo ya kimwili, hilo kwako halina maana sana!…mali zikiongezeka ni kama vile moyoni mwako hakuna kilichoongezeka…lakini uhusiano wako na Yesu unapoimarika ndipo unajihisi uchangamfu wa Ajabu unakuvaa….Inafikia mahali umasikini na Utajiri kwako ni sawasawa tu! Kama Ayubu, ilifika wakati hata mali zilipoongezeka hakufurahia (Soma Ayubu 31:25)..
Na pia baada ya kuacha vyote namna hiyo, kitakachofuatia ni kuchukiwa, kutengwa, kuonekana umerukwa na Akili, kuonekana mjinga katika jamii na kuonekana hufai…Na hivyo pia unapaswa uwe navyo tayari! Bwana Yesu hakutuficha kabisa alituambia ili tukikutana nayo tusiseme mbona hivi mbona vile..Upige gharama kabisa kabla ya kuanza kujenga Mnara! Usije ukafika katikati ukashindwa kumalizia…
Ndivyo ilivyo kwa Bwana Yesu kabla ya kumfuata, piga hesabu kuwa kuna kuchekwa huko mbele, kuna kudharaulika, kuna kupungukiwa wakati mwingine hata kwa kipindi kirefu sana, wakati mwingine hata miaka kadhaa, hata miaka 5, au 10, hata 15, lakini haitadumu hivyo hata milele, kuna kutengwa na kuonekana mjinga, hata kwa miaka kadhaa…piga gharama zote hizo..Kama haupo tayari! Kuonekana mshamba kwa kwa muda mrefu hivyo, au kuonekana mjinga kwa miaka kadhaa, au kudharaulika kwa miaka kadhaa, au kama haupo tayari kukosana na mama yako kuhusiana na Imani yako, au kukosana na Baba yako, au Watoto wako, au mke wako..kama unajua yatakushinda huko mbeleni…
Biblia inasema tafuta sharti ya Amani mapema!…Usijiingize mahali ambapo hujajua yatakayokupata mbeleni, ukaja ukakutana na ambayo hukutegemea ukaanza kujuta na kulalamika.
Kwasababu Bwana Yesu anasema:
Luka 12: 51 “Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.
52 Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu.
53 Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu”.
Je! Umejikana nafsi?..Umejitwika msalaba wako na kumfuata Yesu? Fahamu kuwa mtu yeyote anayeingia gharama kubwa kama hizo, Sio bure bure tu, Huyo anapelekwa katika viwango vya juu zaidi vya kuwa karibu na Kristo zaidi ya watu wengine wote, anafanyika kuwa mwanafunzi wake (MKRISTO) na zaidi ya yote Bwana atakuja kumpa mara mia, na siku ile ataketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi akiwahukumu mataifa..(Mathayo 19:27-30)
Hivyo anza leo kujitadhimini Ukristo wako, je umemfuata Yesu kweli? au upo miongoni mwa makutano wanaomfuata Yesu ili waponywe, waitwe wakristo na huku hawataki kuwa wanafunzi wa Kristo.

Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.