Maombi ni silaha mojawapo inayoweza kukuletea matokea makubwa sana, na shetani kwa kulijua hilo,anapiga vita swala la maombi, hivyo hatuna budi kuwa na miongozo ambayo itatusaidia tuzidi kukomaa kimaombi na kuendelea mbele zaidi,
Ipo miongozo mingi itakayokusaidia kuomba ila kwa neema za Bwana tutaangalia ni namna gani tunaweza kuingia kwenye maombi tukiwa tayari tuna mwongozo flani, ijapokuwa kuna wakati Roho Mtakatifu atakuongoza uombe kwa ajili ya jambo tofauti na mwongozo ulionao..
Ukiwa mtu wa maombi bila kuwa na mwongozo utajikuta kuna muda huwezi kufika,na sio kwasababu huna nguvu za rohoni,bali ni kwa kuwa hukwenda na vitu vya kuombea hivyo inaweza kukupa shida kuomba masafa marefu,
Huu ni mwongozo wa maombi yako ya asubuhi ambayo utapaswa kwenda nayo, zingatia kuna wakati Roho atakusemesha kwa namna yake kwasababu hii uisomayo sio kanuni ya daima bali itakusaidia kwa kipindi, Kumbuka hata Bwana Yesu alituonyesha kipimo cha cha kuomba ni lisaa limoja..
1) SHUKRANI
Jambo kuu unalopaswa kuanza nalo Katika asubuhi yako ni shukrani, mshukuru Mungu kwa siku mpya,ulinzi,amani, wokovu pamoja na mengi aliyokutendea, shukrani inaonyesha unathamini kile Mungu alichokutendea..usiamke kama mnyama,piga goti mshukuru Mungu..
Wakolosai 3:15 “…..tena iweni watu wa shukrani”
2) OMBA MWONGOZO WA SIKU MPYA
Huna budi kumwomba Mungu akupe mwongozo wa siku yako mpaka inaisha, upite njia zake yeye alizozikusudia ili usienende nje ya sheria zake na amri zake, ukaishi sawa na mapenzi yake ili siku yako ikawe heri..
Mithali 16:3 “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika”.
3) OMBA KULIISHI NENO LA MUNGU
Mkumbushe Mungu akupe Neema ya kuliishi Neno lake kila siku, Katika siku yako mpya omba kulitendea kazi Neno la Mungu,usilisahau au kuliacha Neno lake,uishi Katika Neno
Zaburi 119:16 “Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako”.
4) OMBA KUZUIA ULIMI
Omba kwa Bwana siku yako mpya akupe nguvu ya kuzuia ulimi wako usinene maneno yasiyompendeza au kujikwaa kwa namna yoyote,omba ulinzi Katika kinywa chako
Zaburi 141:3 “Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu”
5) UTUKUFU KWA MUNGU
Kila tulifanyalo kwa neno au kwa tendo mwombe Bwana utukufu umrudie yeye, siku yako mpya ikawe ya kumrudishia utukufu yeye kwa matendo yako na kuenenda kwako..
1Wakorintho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu”
6) KUKOMBOA WAKATI
Ni jambo la msingi sana umwombe Mungu akupe Neema ya kuuomboa wakati,usiutumie muda vibaya bila vitu vya msingi bali ukaukombe wakati kwa kufanya mambo yaliyo na maana na msingi kwenye wokovu na roho yako
Waefeso 5:15 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; 16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu”
7) KUHUBIRI INJILI
Mwombe Bwana nguvu ya kuhubiri injili bila woga wala wasiwasi,omba ujasiri wa kuwahubiria na wengine ili wamjue yeye,ombea na kazi ya Mungu inayofanyika Katika ulimwenguni kote bila kuwasahau na watumishi wa Mungu wazidishiwe nguvu zaidi Katika kuitenda
Matendo 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”
8) NDUGU NA FAMILIA
Waombee ndugu zako na familia yako, Bwana awape wokovu ndani ya roho zao, ombea Neema ili wadumu katika imani, kwasababu kwa kusimama kwako utawasimisha na wa kimaombi
Warumi 10:1 “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe”.
9) JAMII INAYOKUZUNGUKA
ombea jamii yote inayokuzunguka, omba amani, utulivu na kila utakayekutana naye Katika mazingira mbalimbali, utulivu Katika jamii yako ndiyo Amani yako Katika kumtumikia Mungu, omba
Yeremia 29:7 “Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani”.
10) UEPUSHWA NA ADUI
Omba Bwana akuepushe na yule mwovu,hila zote zilizokusudiwa juu yako zisikupate kabisa,mwombe Bwana ulinzi kwenye afya yako, na uepushwe na majaribu ya rohoni na mwilini..
Vitumie Vipengele hizi kuianza siku yako mpya, na kila kipengele kina dakika sita (6) ili litimie lisaa limoja, fanya hivi kwa Uaminifu na utaona mabadiliko makubwa kwa roho yako hata mwilini, Kumbuka maisha ya wokovu bila Maombi,hutafika popote ndugu..
Shalom..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.