Kwanini Yesu ni njia ya kweli na uzima, na pasipo kupitia kwake hatuwezi kumwona Mungu

Biblia kwa kina No Comments

Kwanini Yesu ni njia ya kweli na uzima na pasipo kupitia kwake hatuwezi kumwona Mungu.

Yohana 14:6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

Kwanza ni vizuri kufahamu kigezo cha kumuona Mungu ni UTAKATIFU, na ndio maana biblia inasema..

Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” (Waebrania 12:14).

Sasa kiuhalisia hakuna mwanadamu mkamilifu asiye na dhambi hapa duniani, maandiko yanasema..

Zaburi 14:2-3 Toka mbinguni BWANA aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.

[3]Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.

“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;” (Warumi 3:23)

Sasa kama wanadamu wote wametenda dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, tutawezaje basi kuwa watakatifu na wakamilifu kama Mungu atakavyo.

Jibu ni kwamba kwa akili zetu na nguvu zetu hatuwezi kuwa watakatifu mbele za Mungu na hatuwezi kumuona Mungu haijalishi tutajiwekea sheria nyingi kiasi gani, bado tu tutaonekana wenye dhambi mbele za Mungu maana tulizaliwa pia na ile dhambi ya asili ambayo tumeiridhi kutoka kwa mababu zetu Adamu.

Ndio maana mtoto akizaliwa, anakua na vimelea vya dhambi ndani yake mfano hasira, uchoyo, ugomvi, wivu, n.k ambavyo unaweza usivione mapema lakini kadri siku zinavyoenda hizo tabia zinaoneka wazi wazi.. tatizo sio yeye ni ile dhambi ya asili.

Sasa ni vizuri kufahamu hili..

Mungu alipomwumba Adamu alikuwa mkamilifu (hakuwa na dhambi) na alipewa mamlaka yote ya duniani..ikiwemo kutawala kila kiumbe pamoja na kuitiisha nchi..Adamu na uzao wake akafanywa kuwa mtawala wa vitu vyote..Hata shetani alikuwa chini yake,..hakuna kiumbe chochote kingekuwa na mamlaka ya  kusogeza hata jani moja isipokuwa kwa mamlaka ya Adamu, mamlaka hiyo Adamu aliendelea kuwa nayo mpaka  siku Hawa alipodanganywa na nyoka na kula tuna na kumpa mumewe..na wote wawili walipoasi hiyo mamlaka yote waliyopewa wakamwuzia shetani. Hivyo shetani akawa mtawala wa ulimwengu..akitaka kumtupia mwanadamu ugonjwa anweza, hata akitaka kumwua anao uwezo huo. Akitaka kuleta tufani anaweza na mwanadamu yoyote asimzuie..na kuanzia huo wakati mwanadamu akapoteza utakatifu na hakuweza tena kumuona Mungu..na wanadamu wote waliaofuata vizazi na vizazi hakuna hata aliyempendeza Mungu (ambaye aliweza kuishi pasipo na dhambi), wote walikuwa wamepotoka.

Lakini kwa huruma za Mungu..akatengeneza njia ya wokovu kwa mwanadamu….kwamba mwanadamu aokolewe..yaani ni kama bahati tu!..shetani na mapepo yake hawakupata hiyo bahati ya nafasi ya pili kama tuliyopata sisi. Na kwasababu ni mwanadamu ndiye aliyejiharibia hamna budi kwa njia ya mwanadamu huyo huyo ukombozi utokee.

Hivyo Mungu akaanza uumbaji mwingine wa mtu mwingine, ambaye huyo atakuwa kama Adamu..ambaye atapewa mamlaka yote ya duniani, atawale kila kitu na kila kiumbe,na vitu vyote viwe chini yake, kama Adamu, mtu huyo Ataumbwa akiwa mkamilifu na bila dhambi kama alivyoumbwa Adamu. Na huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO..Huyu Yesu ni Adamu wa Pili….Ameumbwa kwa viganja vya Mungu kwa uweza wa Roho katika tumbo la Bikira. Huyu Yesu ni Adamu wa Pili….Ameumbwa kwa viganja vya Mungu kwa uweza wa Roho katika tumbo la Bikira. Huyu alikuwa ni mwanadamu kabisa, lakini kuna SIRI kubwa iliyokuwepo ndani yake…japokuwa alionekana kama mwanadamu lakini alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyeuvaa mwili..(kasome 1Timotheo 3:16). Lakini hilo halikuwa la muhimu sana sisi kulijua ndio maana biblia ikaliita ni siri..

Sasa, kwa neema za Mungu na huruma zake nyingi, sisi ambao tulikuwa tumepotoka na kuoza, kupitia huyu Yesu na sisi tunahesabiwa haki pasipo sheria yoyote, yaani tunakuwa watakatifu kabisa mbele za Mungu.

Unapomwamini Yesu na kuamua kumfuata kwa kujikana nafsi kabisa, unahesabika we ni mtakatifu hata kama bado haujakamilika..unakuwa mtakatifu kabisa kiasi kwamba hata leo ukifa au unyakuo ukipita unaenda kumuona Mungu. (Hii ni neema ya ajabu sana)

Warumi 3:20-26 kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.

[21]Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii;

[22]ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;

[23]kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;

[24]wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;

[25]ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa;

[26]apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki YEYE AMWAMINIYE YESU.

Sasa ni vizuri kufahamu pia kuwa unapomwamini Yesu Kristo na kukubali kutubu dhambi na kuziacha kabisa, ni kweli kuanzia wakati huo unahesabika kuwa mwana wa Mungu na dhambi zako zote zinafutwa, na unaitwa mtakatifu hata kama bado hajafikia utakatifu wenyewe, ukamilifu.. Lakini hii haimanishi kuwa utaendelea kuishi na dhambi kwasababu umeokolewa kwa neema.

Kuna tofauti ya kuwa na dhambi na kuishi na dhambi.. mtu yoyote aliyeokoka kweli kweli (aliyemwamini Yesu Kristo) hawezi kuishi na dhambi ingawa anaweza kuwa na tabia fulani fulani ambavyo sio sawa, lakini kwa wakati huo anahesabika tu kuwa ni mtakatifu kwasababu bado hajui, lakini akisikiliza mahubiri au akasoma biblia na kufahamu kuwa tabia na vitu anavyovifanya hazimpendezi Mungu, basi anakuwa tayari kuziacha haraka.

Kwa mfano, alikuwa anashabikia mipira, na kufuatilia movies za kidunia ambavyo havina maudhui ya kiMungu, akihubiriwa kuwa vitu hivyo havifai kwa mtu aliyeokoka anaviacha haraka, alikuwa anabeti, anacheza kamari, magemu, anaishi na boyfriend au girlfriend, ananyoa mitindo ya kidunia kama kiduku, au anasuka, anavaa wigi, anavaa nguo zizonautukufu mbele za Mungu kama kaptula, suruali, na nguo zinazochora maumbile yake, akihubiriwa kuwa binti wa Kristo au kijana aliyemwamini Yesu Kristo hafai kuwa hivyo, akuwa mwepesi kubadilika..na hii ndio tofauti ya kuishi na dhambi na kuwa na dhambi.

Ukiona, unahubiriwa na kujulishwa makosa yako na hutaki kubadilika, basi fahamu kuwa kuna kasoro, kwenye wokovu wako, huenda bado hujamwamini Yesu kweli kweli na bado hujahesabiwa haki.

Mtu ambaye ameokoka kweli kweli, kila siku anatafuta kumpendeza Mungu, hivyo yupo tayari kujirekebisha muda wowote anaposikia kweli, na huu ndio utakatifu.

Utakatifu sio kutokuwa na dhambi kabisa, utakatifu ni kumwamini Yesu Kristo sawa sawa na kukubali kubadilishwa na kubadilika kila siku.

Ndio maana, Neno la Mungu linasema..

Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA”. (Ufunuo 22:11)

Mtakatifu ni nani? Ni mtu aliyezaliwa mara ya pili, yaani aliyemwamini Yesu na kubatizwa kwa usahihi..sasa huyu mtu ndiye anapaswa kuendelea na utakatifu wake, kuendelea kujitakasa.

Kumbuka, kiuhalisia hakuna mtakatifu mbele za Mungu isipokuwa tu mmoja ambaye alizaliwa pasipo na dhambi na akaishi bila kutenda dhambi hata moja, naye ni YESU KRISTO, sasa kupitia huyu na sisi tunahesabiwa kuwa ni watakatifu bure..na kuanzia huo wakati tuliomwamini na kumpokea tunazidi kutafuta utakatifu kwa bidii (tunazidi kujitakasa)

Na hapo sasa tunaweza kumuona Mungu wetu, lakini sharti kwanza kabla hatujafikia utakatifu wenyewe ni lazima tumwamini Yesu Kristo ili tuhesabiwe kuwa watakatifu.. ili Hata tukifa kabla hatufikia kimo cha utakatifu tuweze kumuona Mungu.

Na hiyo ndio sababu kwanini Yesu Kristo ni njia ya kweli na uzima na kwamba pasipo yeye hatuwezi kumuona Mungu, ni kwasababu Mungu ni mtakatifu na hakuna atakayemuona asipokuwa na huo utakatifu, na utakatifu huu tunaupata kwanza kwa kumwamini Yesu Kristo ambaye yeye ni Bwana wa utakatifu.

Yohana 14:1-6 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

[2]Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

[3]Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.

[4]Nami niendako mwaijua njia.

[5]Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?

[6]Yesu akamwambia, MIMI NDIMI NJIA, NA KWELI, NA UZIMA; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

Je! Umemwani huyu Yesu ipasavyo, au umemwamini kwa jinsi ile ya kidhehebu?

Kama bado hujampokea kisawasawa na unahitaji msaada, basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii tutakusaidia.

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *