Vitu vitatu ambavyo unapaswa kufanya mara tu baada ya kuokoka ili ufikilie utakatifu.
Nakusalimu katika jina la Mwokozi YESU KRISTO Mfalme wa wafalme na Bwana wa Mabwana.
Kama kijana, mzee na mtu yoyote uliyemwamini Yesu Kristo na kukubali kumfuata, vipo vitu vitatu ambavyo ni lazima uvifanye ili uweze kufikilia utakatifu.
Kwanini utakatifu? Ni kwasababu pasipo huo hakuna wokovu, kuokoka sio kujiunga na kanisa au kutoa sadaka aina zote, au kuhudumu kanisani na kwingineko, hayo ni vizuri na mtu aliyeokoka hana budi kuvifanya, lakini pamoja na hayo yote pasipo UTAKATIFU bado wokovu haujakamilika, haijalishi utakuwa na huduma kubwa kiasi gani!
Hivyo kila mtu aliyeokoka au ambaye anatazamia kuokoka, ni vizuri aweke akili hilo, kuwa wokovu ni kufikilia utakatifu.
Utakatifu unawezekana kabisa, sio jambo ambalo haliwezekani kama mahubiri ya shetani yanavyodanganya, ingekuwa kweli utakatifu ni jambo ambalo haliwezekani kwa mwanadamu, basi, Mungu asingesema tuwe watakatifu kama yeye alivyo (1Petro 1:16)
Tena Bwana anashuhudia mwenyewe kuwa kuna watakatifu duniani na ndio anaopendezwanao.
Zaburi 16:3 Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.
Hivyo, usipoamini hilo, basi huwenda bado hujataka kuwa hivyo, lakini kwa wewe ambaye unataka kufikilia utakatifu baada ya kumpokea Yesu kabisa kabisa, yapo mambo makuu matatu ambavyo ni lazima uvifanye ili kufikia katika kimo cha Kristo yaani utakatifu.
Jambo la kwanza ni KUJIKANA NAFSI.
Neno kujikana linamaana kuwa, ‘kukataa matamanio yako binafsi au malengo yako kwa sababu fulani’. Hivyo kujikana kunakozungumziwa katika biblia ni kujikana kwa Kristo. Hii ikiwa na maana kuwa unapoamua kumfuata Kristo unakuwa tayari kuyakataa matamainio yako hata kama ni mazuri kiasi gani, hata kama yanatia maanani kiasi gani, unayaweka chini na kukubali kuyafuata yale ya Bwana Yesu tu. Na ndio maana mtume Paulo aliweka wazi na kusema hivi:
“7..Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.
8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; (Wafilipi 3:7-8)”.
Unaona hii ni nguzo kuu na ya muhimu sana, inayomtambulisha mtu kama amemfuata Kristo. Wanaotubu dhambi zao ni wengi lakini wanaodhamiria kumfuata Kristo ni wachache sana. Unapoamua kuwa binti wa kikristo, uwe tayari kuukana uzuri wako, na kuacha kuvaa vimini na suruali, nguo za kikahaba, na mapambo ya kiulimwengu…ili ufanyike mwanafunzi wa Yesu vinginevyo bado hujawa mkristo hata kama utasema umeokoka.
Vile vile kijana unapokuja kwa Kristo uwe tayari kukataa tamaa zote za ujanani, disco, miziki ya kidunina, pombe na sigara, uasherati, unavipiga vita unaamua kumwangalia Kristo kuanzia huo wakati na kuendelea. Ni mambo ambayo ungeweza kuyafanya kama vijana wengine katika ujana wako lakini unajikana kwa ajili ya kuujua uzuri ulio katika Kristo. Na Bwana Yesu akishaona huo moyo wako hapo ndipo na yeye anapochukua nafasi ya kukufanya kuwa mtu mwingine wa tofauti kabisa katika viwango vya rohoni. Unafanyika kuwa mwanafunzi wake kweli kweli kama mitume wake.
Na hili ni tendo endelevu ambalo linapaswa liwe kila siku, hata katika kuifanya kazi ya Mungu unapaswa ujikane mwenyewe, muda ambao ungetakiwa kufanyabiashara kama watu wengine wewe unaifanya kazi ya Mungu, Vilevile tumeagizwa tudumu katika sala, wakati ambao ungepaswa ulale usiku kama watu wengine wewe unaamka kuomba, huko ni kujikana nafsi. Bwana anakokuzungumzia. Lakini pamoja na hayo katika kujikana huko, na kupoteza matamanio yako au vitu vyako kwa ajili ya Kristo yeye mwenyewe anatuambia, kwa kufanya hivyo ndivyo tunavyozipata. Kwa Mungu hakuna matujo kwani sikuzote mawazo anayotuwazia sisi na ya amani wala sio mabaya ili kutupa sisi tumaini zuri katika siku zetu za mwisho (Yeremia 29:11).
Na ndio maana hatuoni shida hata anapotuambia tuache kila kitu kwa ajili yake. Faida yake tutaiona kama sio katika ulimwengu huu basi katika ulimwengu unaokuja. Kwasababu anatuwazia kusudi jema siku zote. Hivyo, Ni heri uonekane unapoteza kila kitu sasa kwasababu tu umeamua kumfuata Kristo, kuliko kupata kila kitu cha ulimwengu huu na mwisho wa siku unaishi katika ziwa la moto, itakufaidia nini?.
Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na AJIKANE MWENYEWE, ajitwike msalaba wake, anifuate.
25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”.
Jambo la pili KUJITENGA/KUACHANA NA MAKUNDI
Silaha moja shetani anayoitumia kuharibu maisha ya kiroho ya watu wengi, hususani vijana ni MAKUNDI!..
Na mtu mkamilifu ni Yule anayeweza kuchagua aina ya watu wa kutembea naye. Biblia inatufundisha kuwapenda watu wote, lakini si kuambatana na watu wote.
2Wakorintho 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani KATI YA HAKI NA UASI? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”
Umeona?..maana yake ni kwamba kama unaambatana na mtu ambaye si wa aina yako, basi unajiharibu mwenyewe!, Baada tu ya kumkiri Yesu, jambo lingine la muhimu linalopasa kufuata ni KUCHAGUA AINA YA WATU, utakaoanza kuwa nao karibu, kuanzia huo wakati na kuendelea.
Wengi wanalikwepa hili na mwisho wa siku wanajikuta wameurudia ulimwengu tena kwa kasi kubwa.. Ndugu ukishaokoka yale makundi ya walevi uliyokuwa unashinda nayo, ni sharti uyaache!, ukishaokoka zile saluni ulizokuwa unaenda ambazo kutwa kuchwa ni kuzungumzia mambo ya watu wengine, unaziacha.. Ukishaokoka wale watu uliokuwa unakula nao rushwa, au unaiba nao unawaacha!
Sasa unawaachaje?
Awali ya yote unapaswa uwaambie na uikiri imani yako mbele yao, na endapo wakikusikia na wao wakakubali kubadilika na kuwa kama wewe basi utakuwa umewapata, lakini kama hawataki kubadilika na zaidi sana njia zao ni zile zile, basi hapo UNAPASWA UWAACHE!!, Kwa usalama wa roho yako, anza kutafuta marafiki wengine wa imani moja na wewe, hao panga ratiba mara chache chache kwenda kuwatembelea na utakapowatembelea habari utakazowapelekea ni za injili kuanzia mwanzo wako hadi mwisho wako.
Na kamwe usijaribu kuwaza kuwa unaweza kuwa shujaa na kwamba hawataweza kukurudisha nyuma endapo utashikamana nao..Ni kweli katika siku za mwanzo unaweza kujiona wewe ni mshindi, lakini nataka nikuambie kwa kadiri siku zitakavyozidi kwenda tabia yako njema kidogo kidogo itaanza kuathirika, na baada ya kipindi fulani, utajioni umepoa kabisa na kufanana na hao, au kuishia kuwa mkristo vuguvugu tu!.
Ukitaka ukristo wako uimarike siku baada ya siku, watafute wakristo wa kweli ungana nao!..na iache kampani mbaya!.. binti ukitaka udumu katika kuvaa vizuri na kwa heshima, na katika usafi watafute mabinti wenzako wa imani kama yako hiyo, dumu nao hao!.. utautunza utakatifu wako kwa viwango vya juu.. lakini ukitaka kuanza na moto na kuishia baridi, basi endelea na makundi yale yale uliyonayo baada ya kuokoka. (Maisha yako ya wokovu hayatafika mbali).
Vile vile ukitaka kudumu katika eneo la Maombi, yaani uzidi kuwa mwombaji, na mtu wa ibadani na mtu wa kumpenda Mungu, sharti uwatafute watu wa namna yako!.. ambao ni wacha Mungu tena wanaopenda maombi, lakini kama hutawatafuta hao na ukasema mimi ninaweza kuendelea kuwa mwombaji hata nikiwa na makundi yangu yale yale, nataka nikuambie ndugu yangu, unapoteza muda.. mwisho wako utakuwa mbaya sana, na hautajua ni saangapi umepoa kiroho au umeanguka kabisa.
Sasa tunazidi kulithibitisha vipi hili kimaandiko?
Tusome,
2Timotheo 2:22 “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, PAMOJA NA WALE WAMWITAO BWANA KWA MOYO SAFI”.
Hapo anasema tuzikimbie tamaa za ujanani, tukatafute “haki, imani, upendo na amani.” Lakini sasa tunatafuta hii haki, imani, upendo na amani pamoja na watu gani???..je! pamoja na walevi?, au pamoja na wazinzi?, au pamoja na watu wenye mizaa? Au pamoja na wahuni?..jibu ni la! Bali pamoja na WALE WAMWITAO BWANA KWA MOYO SAFI!!… Na wanaomwita Bwana kwa moyo safi si wengine zaidi ya wale wakristo waliosimama kikweli kweli, ambao Bwana kawapanda kila mahali.
Ukidhani kuwa unaweza kulirekebisha hilo andiko na kwamba wewe unaweza kwenda kutafuta Imani pamoja na walevi, unapoteza muda!, ukidhani unaweza kuitafuta amani na kuipata pamoja na wazinzi, au wahuni, au wauaji, au watu wa masengenyo basi nataka nikuambia kuwa unapoteza muda wako mwingi..Hata mwanafunzi hawezi kupata maarifa yoyote ya darasani endapo akikaa na wanafunzi wasiopenda shule, lakini akikaa na wenzake wapendao shule basi atapata faida anayoitafuta.
Vile vile na wewe leo hii, punguza makundi ya watu wa kidunia, na ongeza makundi ya watu wamwitao Bwana kwa moyo safi.
Jambo la tatu na la mwisho ni kukaa mbali na vichocheo vyote vya dhambi.
Mithali 26:20a, inasema moto hufa kwa kukosa kuni..” ukitaka kufanikiwa kushinda dhambi hasa ya uasherati, ulevi, usengenyaji, tamaa n.k huna budi kukaa mbali na vichocheo vyake baada ya kuokoka, kila dhambi ina kichocheo chanzo chake hivyo ni lazima kukaa mbali na hiyo chanzo..hapo ndipo utaweza kufiklia utakatifu.
Baadhi ya vichocheo hivyo ni..
1)Kutazama Picha na Video za kizinzi (Pornography).
Hii ni nyenzo kubwa sana shetani ameitumia kwa kizazi hiki kukiangamiza, Hii ni njia yenye ushawishi mkubwa kuliko zote, kiasi kwamba mtu akijiingiza huko uasherati hawezi akaukwepa kwa namna yoyote iwe ni ameshaingia kwenye ndoa au hajaingia, iwe ni kijana, au mzee haikwepeki, mtu huyo atabakia kuwa mwasherati au mzinzi daima.
2 Njia ya pili ni ‘Mazungumzo mabaya’;
Biblia inasema 1Wakoritho 15: 33 Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema . “ Haya ni mahubiri ambayo utakuta shetani anamuhubiria mtu pasipo hata yeye mwenyewe kujua, utakuta vijana au wazee kutwa kuchwa wanazungumza habari za wanawake, na wanawake vivyo hivyo utawakuta wana jadili habari za wanaume muda wote, lakini muda wa kutafakari mambo ya muhimu ya Mungu hakuna, sasa hapo watu kama hao ni rahisi sana kutawaliwa na roho za tamaa, kwasababu vichwa vyao wakati wote vimejazwa hayo mafundisho ya zinaa. Biblia inasema “hata uasherati usitamkwe kati yenu.”Utakuta kijana muda wote anaumalizia mtandaoni..ukitazama ni kitu gani anafanya, utagundua kuwa anachati katika magroup ambayo misingi yake ni uasherati, sasa kwa tabia hiyo haiwezekani wewe kuushinda uasherati hata uombeweje ni wewe tu kuamua kuacha hivyo vitu na kuanza kutii mahubiri ya Roho Mtakatifu ndani yako.
3 Mavazi:
Vimini, suruali, kaptura, nguo zinazobana na zinazoonyesha vifua na migongo wazi kwa wanawake n.k., hivi vyote ni vichecheo vya uasherati, mavazi hayo yalibuniwa kwa kazi hizo, kuwavuta wazinzi wasogee karibu na wewe, hivyo mtu anayejiita mkristo na kuanza kuzivaa moja kwa moja anakaribisha uwepo wa uzinzi ndani yake.
4) Mziki na filamu za kidunia:
Kusikiliza miziki ya kidunia hii pamoja na filamu za kimapenzi ni kichecheo kikubwa cha kubebwa na roho hizi, asilimia 99 ya miziki yote ya kidunia zina mahudhui ya kiasherati ndani yake unategemea vipi uepukane na tabia hizo?. Na ndio maana utakuta mtu analalamika hawezi kuacha kuwa mzinzi/mwasherati wakati muda wote anaumalizia kwenye vitabu, filamu na tamthilia za kimapenzi. Viache hivi vitu kwanza na ndipo utakapoanza kuona wepesi.
Na mambo hayo yakishakaa ndani yako sana, sasa yanakuwa yakijirudia rudia yenyewe tu kwenye akili yako, mpaka inakuwa ngumu kuyakwepa kwasababu ndio yaliyoujaza moyo wako,
Hivyo hayo ni mambo ya kuzingatia sana ikiwa unataka kuitwa mtakatifu na kumpendeza Bwana.
Kumbuka, maandiko yanasema..
Waebrania 12:14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
Maran atha.
Bwana akubariki
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.