WAFU WATAFUFULIWA

Siku za Mwisho No Comments

WAFU WATAFUFULIWA

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo, Mfalme wetu, Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Kabla hatujaendelea mbele, Naomba usome ushuhuda huu mfupi utakuwa msingi wa somo letu.

“Ilikuwa ni tarehe 17/10/2025 majira ya alfajiri, Bwana alinipa huu ujumbe kupitia ndoto. Niliona miili ya watu wengi ikifufufuka kutoka ardhini, waliposimama nikawaona baadhi ambao nawajua, walikuwa wakiangaliana kwa mshangao, wakawa wanasogea mbele kama kuna mahali wanaelekea kwa pamoja(niliwaona kama walikuwa wanafahamu kinachoendelea), nilisikia mmoja akimwambia mwingine “tofauti ya huku na kule tulipokuwepo ni giza, kule kuna giza kuu” walikuwa ni vijana kwa wazee niliwaona. Nikaona wakatokea watu wawili ambao walikuwa ni walimu waliowahi kunifundisha nikiwa shuleni, wakaketi mbele ya hao wafu, na meza mbili ikawekwa mbele yao, walikuwa wameshika vitabu vyenye makosa mbali mbali ya hao wafu, ambao walikukusanyika kusikiliza mashitaka zao, kila mmoja alikuwa anahojiwa na kupewa nafasi ya kujitetea. Wakati huo mimi nilikuwa ndani pamoja na watu wengineo ambao siwakumbuki, hivyo kilichokuwa kinaendea kule nje hatuoni, lakini muda kidogo tukaona miongoni mwa wale wafu, watu wachache wakiingia ndani mtu mmoja moja, wakeenda kusimama mbembeni… walikuwa wana nyuso zilizojaa huzuni na majuto. Nilipoangalia chini mahali niliposimama nikaona shimo refu sana(kwa kweli lilikuwa linatisha sana), nikawahurumia sana hao wafu maana walionekana wote wanastahili hukumu japokuwa kuna wachache ambao hukumu yao ni tofauti na wengine. Nikakumbuka kweli kwenye lile ziwa la moto kila mtu anakuwa na sehemu yake kulingana na makosa yake, (Bwana alisema Luka 12:47-48 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana, Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.) Baada ya hapo niliamka usingizini.”

Nikiwa katika hali ya kutafakari hilo jambo nililoliona, nikiwa kwenye mawazo mengi Bwana akanifundisha kuwa ulichokiona ndicho kitakuja kutokea mbeleni, na ndivyo hali za watu itakavyokuwa, itakuwa ni majuto na huzuni isiyoelezeka siku hiyo kwa wale waliokufa kwenye dhambi.

Ndugu haya siyo maneno tu ya kutunga, au siyo mawazo ya kichwa changu tu. Ni ujumbe wa Bwana kwangu na kwako unayesoma. tutengeneze maisha yetu sasa na Bwana ingali tunayo nafasi. Maana kuna hukumu mbeleni haikwepeki.

Hebu tusome maandiko tuone yanasemaje kuhusu hili.

Danieli 12:1 ”Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.

[2]Tena, WENGI WA HAO WALALAO KATIKA MAVUMBI YA NCHI WATAAMKA, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.”

Unaona hapo, wafu watafufuliwa, wengine wapate uzima wa milele na wengine aibu na kudharauliwa milele.

Sasa ni vizuri kufahamu kuwa kuna aina mbili za ufufuo ambao umetajwa katika biblia.

Ufufuo wa kwanza, umejumuisha wale watakatifu waliofufuka na Bwana Yesu ukisoma (Mathayo 27:52) utaona..,pamoja na watakatifu watakao fufuka katika unyakuo, na watakao fufuliwa wakati wa kuingia kwenye ule utawala wa miaka 1000 (Ufunuo 20:4) haya ni makundi matatu yanayotengeneza aina ya kwanza ya ufufuo.

Ufunuo 20:6 “….Heri na mtakatifu ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza, juu ya hao mauti ya pili haina nguvu…”  

Na ufufuo wa pili utakuja mara tu baada ya utawala wa miaka 1000 kuisha..ambapo wafu wote ambao hawakuwepo katika ufufuo wa kwanza watafufuliwa na kuhukumiwa na Kristo mwenyewe katika hukumu ya kile kiti cheupe cha Enzi cha Yesu Kristo tukisoma ..

Ufunuo 20:11 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.

12 NIKAWAONA WAFU, WAKUBWA KWA WADOGO, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; NA VITABU VIKAFUNGULIWA; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.

13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. WAKAHUKUMIWA KILA MTU KWA KADIRI YA MATENDO YAKE.

14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”

Kwahiyo ndugu biblia inasema wana heri wale watakaokuwepo katika ule ufufuo wa kwanza. kwasababu mauti ya pili haitakuwa na nguvu juu yao. Na mauti ya pili ni ziwa la moto. Hivyo tujitahidi hata kama Bwana atakupokuja akatukuta tumelala(tumekufa), basi tuwe na nafasi katika ule ufufuo wa kwanza.

Kumbuka leo hii ukifa kwenye dhambi, yaani nje ya Yesu Kristo. Moja kwa moja unashuka kuzimu ambapo huko utakaa kwenye mateso kusubiria hukumu ya ziwa la moto.

Hivyo usidanganyike kuwa baada ya kifo kutakuwa na nafasi ya pili, hapana biblia imeweka wazi kabisa katika..Waebrania 9:27 “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”;

Ukishakufa leo, shughuli zote za hukumu zinaendelea juu yako, hakuna maisha tena hapo, mti ukianguka kuelekea kusini au kaskazini paangukapo ule mti papo hapo utalala (mhubiri 11:3).

Usitarajie kuna badiliko lolote litakalotokea endapo utakufa kwenye ulevi, au uasherati. Ukifa katika hali hiyo unashuka mahali pa wafu kuzimu kungojea hukumu,

Hivyo Dada, fahamu kuwa leo hii ukifa na hayo mawigi kichwani mwako na hizo kucha bandia, hereni, vipini, lipustiks, wanja, n.k moja kwa moja unashuka kuzimu. Leo hii unahubiriwa injili ya kweli kuwa mwanamke kuvaa mavazi yampasayo mwanaume (suruali) ni machukizo sawa sawa na kumbu kumbu la torati 22:5, na mavazi mengine ya aibu (vimini, kaptula, nguo za kubana) halafu hutaki kusikia..unajitetea kuwa hilo ni agano la kale na kwamba Mungu sasa haangalii mavazi anaangalia moyo tu. Nataka nikuambie ile siku itakuwa ni majuto makuu sana kwako..ni heri hata usingesikia habari hizi.

Hebu badilika leo, mpe Yesu maisha yako acha kufuata mkumbo wa dini na madhehebu, acha kuangalia idadi ya watu wanaofanya maasi. Maana utasimama na kujitetea siku hiyo mwenyewe.

We Kijana acha kujichua, acha kamari, acha magemu, acha kusikiliza miziki ya kidunia, acha kufuatilia filamu za kidunia, acha kufuatilia mipira, acha kubeti, acha kunyoa denge/kiduku, acha mahusiano ya kiholelaholela, futa picha chafu zote unazozitama kwenye simu yako, acha kuperuzi peruzi huko mitandaoni bila sababu, achana na kampani za watu wabaya, wavuta sigara, walevi, wazinzi, wahuni, n.k jitenge nao leo, waaambie umeokoka na wahubirie nao waokoke, waaambie kuna hukumu iko mbele.

Bwana atusaidie tutambue haya mapema na tubadike.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *