WALAKINI MAHALI PA JUU HAPAKUONDOLEWA.
2 Wafalme 14:4 “Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.”
Jina la mwokozi Yesu libarikiwe daima, karibu tujifunze biblia neno la Mungu lililo taa na mwanga wa njia zetu.
Katika Agano la kale nyakati za Wafalme, kuna watu walikuwa wanatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali paa juu..jambo ambalo lilikuwa ni machukizo makuu kwa Mungu, na iliendelea kwa muda mrefu mpaka hatimaye alipokuja kutokea mfalme mmoja ambaye aliondoa na kuharibu mahali pa juu kabisa.
Sasa mahali pa juu ilikuwa ni wapi?
Mahali pa juu” ni mahali palipoinuka ambapo watu walikwenda kutengeneza madhabahu na kutoa dhabihu zao.. Mahali hapo panaweza kuwa ni mlimani au mahali penye mwinuko. Ilikuwa ni heshima kwa Mungu kutengeneza madhabahu mahali palipoinuka, kuonyesha kuwa yeye ni juu ya yote.
Ibrahimu ni moja ya watu wa kwanza kutenengeneza madhabahu mahali pa juu.. Wakati anamtoa Isaka mwanawe, alipanda juu ya mlima Moria, na kutengeneza madhabahu pale, sasa mahali pale alipojenga madhabahu ile ndio mfano wa “mahali pa juu”..
Ifuatayo ni baadhi ya mifano michache juu ya mahali pa juu…
1Samweli 9:11 “Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?
12 Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu WATU WANA DHABIHU LEO KATIKA MAHALI PA JUU”
Na pia tunaona kabla Mfalme Sulemani kujenga hekalu lile juu ya mlima Moria, naye pia alikuwa anatoa dhabihuu katika mahali pa juu..
1Wafalme 3:2 “Ila watu walikuwa wakichinja dhabihu katika MAHALI PA JUU, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la Bwana, hata siku zile.
3 Sulemani naye akampenda Bwana, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika MAHALI PA JUU”
Mistari mingine inayozungumzia mahali pa juu ni pamoja 1Nyakati 16:39, 1Nyakati 21:29.
Kwahiyo mahali pa juu ilikuwa ina maana kubwa sana, na hata sasa ni muhimu sana kuwa makini na mahali pa juu, kwani kuna kitu katika mahali pa juu palipoinuka, Ndio maana watu wa Mungu walikuwa wakienda huko juu sehemu zilizoinuka kama mlimani kumuabudu Mungu aliye hai na kumjengea madhabahu..na hata Bwana wetu Yesu alikuwa anapanda mlimani mahali pa juu kuomba, kwahiyo ni muhimu sana kuwa makini na mahali pa juu maana huko tukiweka madhabahu nyingine tofauti na madhabahu ya Mungu aliye hai tunajitafutia laana badala ya baraka.
Lakini tukirudi katika historia ya wana wa Israeli, kama we ni msomaji wa biblia utakuwa unafahamu kuwa kuna kipindi wana wa Israeli walikuwa wanamuacha Mungu na kufuata miungu ya mataifa, na moja ya kosa ambalo walikuwa wanafanya ni kujenga madhabahu ya miungu katika mahali pa juu. Jambo ambalo ilikuwa inamchukiza sana Mungu, na hivyo kipindi walipokuwa wakifanya hayo machukizo, Mungu alikuwa anawadhibu kwa kuwatia mikononi mwa hao mataifa watumikishwe, na wanaporejea na kutubu kwa kumaanisha, Mungu alikuwa anawahurumia, lakini kosa moja ambalo walikuwa wanafanya pasipo wao kujua kuwa linamchukiza sana Mungu ni kutoondoa mahali pa juu. Maana yake walikuwa wanamrudia Mungu na wanaacha mambo mengine mabaya lakini wanaendelea kutoa sadaka zao na kuvukiza uvumba katika mahali pa juu.
Sasa tutazame Wafalme kama wanne wa Yuda ambao walikuwa wanakuja na kufanya mazuri zaidi hata ya wengine waliotangulia .. lakini kosa ambalo walikuwa wanafanya ni kutoondoa mahali pa juu, kwasababu wao waliona ni jambo dogo tu, kumbe ilikuwa inamchukiza sana Mungu.
2 Wafalme 12:1 Katika mwaka wa saba wa Yehu, Yoashi alianza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Sibia wa Beer-sheba.
[2]Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA siku zake zote Yehoyada kuhani alizomfundisha.
[3]ILA MAHALI PA JUU HAPAKUONDOLEWA; watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
Tutazame mwingine..
2 Wafalme 14:1 Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.
[2]Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.
[3]Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi.
[4]WALAKINI MAHALI PA JUU HAPAKUONDOLEWA; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
Hao wote walikuwa wanafanya mema machoni pa BWANA lakini walikuwa hawaoni mahali pa juu. Hebu tuone na wengine wawili,
2 Wafalme 15:1 Katika mwaka wa ishirini na saba wa Yeroboamu mfalme wa Israeli Uzia
mwana wa Amazia mfalme wa Yuda akaanza kutawala.
[2]Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.
[3]Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia.
[4] ILA MAHALI PA JUU HAPAKUONDOLEWA, nao watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
[5]BWANA akampiga mfalme, akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee. Na Yothamu mwana wa mfalme alikuwa juu ya nyumba, akiwahukumu watu wa nchi.
Umeona hapo huyu alifanya mema sana lakini badala apokee dhawabu kinyume chake anapokea mapigo, tatizo nini? Ni kuacha kuondoa mahali pa juu.
Hebu tuone na huyu ambaye alifanya mazuri mno kiasi cha kumuondoa mama yake katika kiti cha umalkia kwasababu alikuwa anaabudu miungu.. lakini pamoja na hayo hakuondoa mahali pa juu.
2 Mambo ya Nyakati 15:8 Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaifanyiza tena madhabahu ya BWANA, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa BWANA.
[9]Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimwangukia wengi katika Israeli, walipoona kwamba BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.
[10]Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.
[11]Wakamchinjia BWANA siku ile, katika nyara walizozileta, dhabihu za ng’ombe mia saba, na kondoo elfu saba.
[12]Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta BWANA, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote;
[13]na ya kwamba ye yote asiyemtafuta BWANA, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, kwamba ni mwanamume au mwanamke.
[14]Wakamwapia BWANA kwa sauti kuu, na kwa kelele, na kwa mapanda, na kwa baragumu.
[15]Na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa moyo wao wote, na kumtafuta kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye BWANA akawastarehesha pande zote.
[16] HATA NA MAAKA MAMAYE ASA, MFALME AKAMWONDOLEA DARAJA YAKE ASIWE MALKIA, KWA KUWA AMEFANYA SANAMU YA KUCHUKIZA kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.
[17] LAKINI MAHALI PA JUU HAPAKUONDOLEWA katika Israeli; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu siku zake zote.
Unaona, wakati Asa anakaa na kuangalia kufuata sheria za Mungu katika torati na kuahakikisha wanazitenda sheria na hukumu zilizoandikwa huko, ni kweli alifanya vizuri sana, lakini kuna jambo ambalo alikuwa haoni, pengine aliona halina shida sana, wakati watu wanamtolea Mungu dhabihu Hekaluni..kumbe kuna watu wengine wanatoka wanaenda kutoa sadaka mahali pa juu kule.
Ndio maana hapa biblia inasema japokuwa alifanya mazuri yote na Mungu akamstarehesha.. hakukuwa na vita lakini mahali pa juu hapakuondolewa. Wakati Asa anaangalia tu sheria za Mungu na kushika torati na kwenda katika sheria za Musa na kuona inatosha, Kumbe Mungu anaangalia zaidi ya hapo, anaangalia ni sehemu gani iliyoinuka na nani anaenda kutolewa dhabihu huko. Mungu ana wivu sana na mahali pa juu. Na ukiendelea kusoma alikuja kutokea mfalme aliyeitwa Yosia, yeye peke yake ndiye aliyekuja kuondoa mahali pa juu na kuteketeza moto kabisa madhabahu zote za kigeni.
2 Wafalme 23:13 Na mahali pa juu palipokuwapo mbele ya Yerusalemu, palipokuwa upande wa kuume wa mlima wa uharibifu, alipopajenga Sulemani, mfalme wa Israeli, kwa Ashtorethi, chukizo la Wasidoni, na Kemoshi, chukizo la Moabu, na Milkomu, chukizo la wana wa Amoni, mfalme akapanajisi.
[14]Akazivunja-vunja nguzo, akayakata-kata maashera, akapajaza mahali pake mifupa ya watu.
15]Tena zaidi ya hayo, ile madhabahu iliyokuwako Betheli, na mahali pa juu alipopafanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli, madhabahu hiyo aliibomoa; na mahali pa juu alipateketeza, akapaponda-ponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera.
19]Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha BWANA, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli.
20]Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu.
Swali ni je! Mahali petu pa juu pa leo ni wapi?..mahali ambapo tunaweza kumtengenezea Mungu wetu madhahabu inayompa heshima yeye?.
Tusome
Yohana 4:19 “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!
20 Baba zetu waliabudu katika MLIMA HUU, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.
21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.
23 LAKINI SAA INAKUJA, NAYO SASA IPO, AMBAYO WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI. KWA MAANA BABA AWATAFUTA WATU KAMA HAO WAMWABUDU
24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”
Umeona mahali petu palipoinuka leo ni wapi?..Si milimani, wala si mahali penye miinuko, bali ni katika roho zetu. Huko ndiko madhabahu za Mungu aliye juu zinapotengenezwa.
Je ndani ya roho yako ipo madhabahu ya Mungu?..au ya miungu?..Haijalishi utakuwa unakwenda kanisani, au unatoa sadaka lakini kama mahali pa juu (yaani ndani ya roho yako), hakuna madhabahu ya Mungu, basi fahamu kuwa bado unaitumikia miungu migeni. Kama moyoni mwako kuna anasa, ulevi, wizi, uasherati, na mengineyo, bado wewe ni najisi mbele za Bwana.
Mathayo 15:19 “Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano”.
Vilevile kama Mungu si wakwanza katika maisha yako, fahamu kuwa mahali pako pa juu (ndani ya moyo wako) umeweka madhabahu nyingine. Utajuaje kuwa ndani ya moyo wako kuna madhabahu nyingine tofauti na madhabahu ya Mungu aliye hai.
Angalia kile kilichoinuka ndani yako, kile ambacho kinakupa kiburi, huwenda ni kazi, elimu, mke/mume, fedha, cheo n.k chochote kile ambacho kinachukua nafasi ya Mungu ndani ya moyo wako kiasi kwamba ukiwa nacho unabadilika kihisia, na ukikosa unabadilika kihisia..hicho ni sanamu (umejenga madhabahu ya kigeni ndani ya moyo wako).
Kama mkristo furaha yako sio kuwa na mali, na vitu vya dunia hii, sio kushabikia mambo ya kidunia, furaha yako hasa ni kuwa na Yesu ndani ya moyo wako basi.
Kama utafanya kazi masaa 12 kila siku halafu hata lisaa limoja kusali hauwezi kutoa, fahamu mahali pa juu umeweka madhabahu ya miungu, na halikadhalika kama unakesha kutazama tamthilia na kuperuzi mtandaoni lakini hata siku moja kwa mwezi huwezi kukesha katika maombi.. fahamu kuwa unamtia Mungu wivu ni heri usiwe mkristo kabisa. Kwahiyo ikiwa umeokoka kweli kweli.. kuwa makini sana na moyo wako kwa maana ndiko mahali pa juu palipoinuka..na ndiko Mungu anakoketi.
Na kama umeweka madhabahu nyingine, ondoa leo, huwenda ni mchumba, mali, elimu, n.k sio vibaya kuwa nayo lakini havipaswi kuchukua nafasi ya kwanza ndani ya moyo wako…ni Yesu tu ndiyo anastahili kuwa wa kwanza katika maisha yako, na ndani ya moyo wako. Hivyo ondoa madhabahu zote za kigeni ndani ya moyo wako…safisha mahali pa juu.
Bwana atusaidie tumjengee madhabahu bora katika roho zetu.
Maran atha!.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.