YESU KRISTO TUMAINI LA UTUKUFU
Wakolosai 1:24-24 “Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake;
[25]ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu;
[26]siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;
[27]ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, TUMAINI LA UTUKUFU.”
Je unalo tumaini la utukufu ndani yako?
Yesu Kristo ni tumaini la utukufu, na ukimkosa huna uzima ndani yako..kwani kupitia yeye tunapata msamaha wa dhambi na ondoleo la dhambi na kupewa tumaini la kuishi milele kupitia kifo chake msalabani.
1 Petro 1:3-4 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate TUMAINI LENYE UZIMA kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
[4]tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
Unaelewa maana ya kuwa na tumaini la uzima? Unaweza ukawa na matumaini lakini usiwe na tumaini la uzima!
Kuwa na tumaini la uzima ni kuwa uhakika wa uzima wa milele ambao Mungu aliuahidi tangu zamani na sasa unapatikana kupitia Yesu Kristo tumaini la utukufu.
Tito 1:1-2 Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa;
[2] KATIKA TUMAINI LA UZIMA WA MILELE, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;
Je! Unalo tumaini la uzima wa milele? Ikiwa mauti bado ina nguvu kwako, kiasi kwamba ukisikia habari ya kifo unakosa amani..hiyo ni udhibitisho kuwa bado hauna uzima na hivyo unahitaji msaada.
Lakini habari njema ni kwamba bado ile njia ya uzima ipo wazi, lakini haitakuwa wazi daima..wakati wote itafungwa na hakuna mtu atakayeza kuingia tena. Sasa hiyo njia ya uzima ni ipi?
Yohana 14:6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Ukimpata Yesu..basi unayo tumaini la uzima wa milele, na ishara mojawapo kuwa unao uzima ndani yako ni kutokuwa na hofu ya kifo na zaidi utakuwa na shauku ya kumuona Bwana.
Ufunuo wa Yohana 22:17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.
Je umempokea Yesu Kristo ipasavyo?
Kumbuka biblia inasema..
Yohana 3:16-18 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
[17]Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.
[18]Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
Kumwamini Yesu sio kusema kwa mdomo nimemwamini basi, Bali ni kuamini kile alichokileta duniani yaani ondoleo la dhambi na hivyo kila atakayesikia habari zake anapaswa kujinyenyekeza na kutubu dhambi zake kwa vitendo ili aondolewe kabisa ndani yake.. kumbuka kutubu sio kuomba msamaha, hapana kutubu ni kuacha dhambi.
Maana yake ule ulevi uasherati, uzinzi, uchawi n.k unaoufanya unaacha kufanya kwa vitendo kabisa. Unachoma mavazi yote ya ukahaba yaani zile suruali, vimini, na yale mapambo yote uliyoweka kwenye mwili wako unavua na kuvichoma zote, zile pakiti za sigara na ugoro unatupia mbali kwa mikono yako au unachoma kabisa, Kadhalika Ikiwa ni picha chafu na miziki ya kidunia ulizonazo kwenye simu yako unafuta zote, ikiwa ni vile vitabu vya uchawi na irizi zake unachoma kabisa, hivyo ndivyo walivyofanya wengine waliokubali kutubu dhambi zao kwa kumaanisha.
Matendo ya Mitume 19:18-19 Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.
[19]Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.
Hiyo ndiyo maana ya kutubu, na baada ya hiyo hatua, hatua inayofuata ni kubatizwa na kumbuka sio ubatizo tu ilimradi, ni ubatizo wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ..huo ndio ubatizo sahihi.
Matendo ya Mitume 2:37-38 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
[38]Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Umeona kanuni ya kupokea uzima wa milele, je! Upo tayari kupokea? Au unatazamia hukumu ya ziwa la moto. Maamuzi ni yako…lakini iwapo utachagua uzima na unahitaji msaada zaidi, basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.