Shalom, Jina la Bwana Yesu lisifiwe milele
Kwa Neema za Bwana tutaangazia ni sifa gani alizonazo mtu ambaye amekombolewa kwenye mikono ya adui shetani, na kwa kujifunza hayo basi utaongeza maarifa zaidi..
Maandiko yanasema,
Marko 5:1-5,8-9,13-16
[1]Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.
[2]Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;
[3]makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;
[4]kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.
[5]Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.
[8]Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.
[9]Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni,
kwa kuwa tu wengi.
[13]Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini.
[14]Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea.
[15]Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa.
[16]Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe.
Kama ni msomaji wa biblia utafahamu hiyo habari, inayomzungumzia yule mtu aliyekuwa na mapepo mengi, waliojitambulisha kwa jina la jeshi yani, legioni, yalikuwa ni mapepo mengi takribani 2000 waliomvaa, wakimtesa, na kumfanya makazi yake yawe ni makaburini, lakini kuna jambo nataka tulione kwenye mstari wa 15,
Embu tusome..
[15]Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa
Baada ya huyu mtu kufunguliwa na kuekwa huru na Bwana Yesu, na mashuhuda kutoa habari zake, yapo mambo matatu natamani tujifunze au uyaone Katika hilo andiko, na tutachambua Jambo moja moja..
(1) Ameketi
(2) Amevaa nguo
(3) Anaakili zake
Na maandiko yanasema yaliyoandikwa yaliandikwa kwasababu yetu sisi, kutufundisha na kutuonya sisi ambao tumefikiwa na miisho ya siku za zamani, hivyo hatuna budi kutafakari kila wakati..
1) Ameketi
Baada ya kufunguliwa kwenye kifungo cha shetani, hakuondoka na kukimbia kwa furaha, hakusema sasa nimekuwa huru nikajichane sasa, bali maandiko yanasema aliketi,maana yake alikaa kwenye utulivu ule wa Yesu Kristo akilisikiliza neno la Bwana,anamwambia nini, akiyasikiliza maagizo ya Bwana juu baada ya kufunguliwa kwake, ni sawa na yule mtu kwenye maandiko ambaye naye alipata uponyaji, hakukubali kuishia kuponywa tu bali alimtafuta Bwana mpka akamkuta kwenye hekalu ndipo akasikiliza Maneno ya Bwana akimwambia..
Yohana 5:13-14
[13]Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale.
[14]Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.
Na sisi hatuna budi baada ya kuona muujiza wa Bwana Yesu aliotutendea, si wakati wa kusema nimeshaponywa sasa basi, ulikuwa kwenye kifungo cha magonjwa lakini Bwana akakufungua unachotakiwa ni kuendelea kukaa chini yake na kumsikiliza anataka nini baada ya kukufungua,
Na tunaketi kuyasikia Maneno ya Mungu si kwenye vigoda au chini ya miguu yake bali tunaketi kwenye kusoma Neno lake yani BIBLIA TAKATIFU, ili umsikie Mungu, uyasikie maagizo yake,keti kwenye kusoma maandiko, kama alivyofanya Mariamu ndugu yake na Martha na Bwana akamuona amechagua fungu lililo jema..
Luka 10
39 Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.40 Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.
41 Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi;
42 lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
2) Amevaa nguo
Jambo lingine alilokuwa kuwa nalo huyu mtu aliyefunguliwa, maandiko yanasema alikuwa amevaa nguo, jiulize kipindi akiwa na yale mapepo kwanini alikuwa uchi/ mtupu, hiyo inatuonyesha tabia ya shetani siku zote ni kukuabisha, kukufanya udharaulike uonekane kituko, uwe uchi,aibu yako ionekane, ndo mana alipofunguliwa alifichwa aibu yake na Bwana Yesu..
watu wengi leo baada ya Bwana kuwaweka huru wanasahau kuficha aibu zao, ni mdada anasema ameokoka lakini kavaa kimini, anavaa suruali za kubana, vinguo vifupi vya kuonyesha mapaja wazi, anajipodoa ili aonekane na watu, huwezi kumtambua kijana aliyesema amefunguliwa, kijana wa kiume,unasuka rasta, unakunywa pombe,unavuta sigara, kutwa unachati na wadada, fahamu kabisa wewe upo uchi…
Ndugu fahamu maandiko yanasema ukishakombolewa mwili wako ni wathamani mbele zake, na yeye haangalii roho tu bali roho na mwili vyote anavikomboa, anza kuvaa mavazi ya kujisitiri kwa wewe dada, magauni marefu ya heshima yenye kumtukuza Mungu, sketi ndefu, funika kichwa chako,ulinde mwili wako kwa adabu njema,
1 Timotheo 2:9
[9]Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
Kijana wa kiume vaa mavazi yanayokupasa kama kijana, achana na ufasheni na mitindo ya kidunia haitakusaidia kitu kumkaribia Mungu wako,
Kumbukumbu la Torati 22:5
[5]Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako.
3) Ana akili zake,
Na jambo la tatu maandiko yametupa kuona huyu mtu akarudi kwenye akili zake, kumbe inatuonyesha hapo mwanzo alikuwa hana akili zake ndio mana ikapelekea awe anapiga makelele, anajichana na kujikata kata, jambo ambalo hawezi kulifanya mtu mwenye akili zake timamu, kwasababu ukiona tu anafanya vituko kama hivyo ufahamu wa haraka utakaokuja ni kuwa hana akili yule, ndivyo alivyokuwa huyu mtu kabla ajawekwa huru.. lakini maandiko yamemtaja baada ya kufunguliwa akili zake zilirudi akawa hafanyi tena yale aliyokuwa akijitendea, kujikata kata, akawa anauelewa mzuri tu,
Hivyo yakupasa baada ya kutolewa kwenye vifungo vya giza na kuwekwa huru, ni sawa ulikuwa huna akili kwa mambo uliyokuwa ukiyatenda lakini sasa Yesu Kristo amekupa ufahamu,amekupa akili ya kutembea kwenye neno lake, ili uwe nuruni na sio kwenye giza tena,
Mtume Paulo kwa kulifahamu hilo aliandika hivi,
Tito 3:3
[3]Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana,
Ukiyatenda hayo utamuona Mungu akitembea na wewe kwa viwango vingine kabisa tofauti na ulivyokuwepo hapo kabla, anza kuliishi Neno la Mungu,
Njia pekee ya kukubalika mbele za Mungu si kwa metendo yako au kusema nimeokoka nampenda Yesu, bali ni kutubu kwa kumaanisha kabisa na kubatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo,ili upokee Roho Mtakatifu,sawa na neno lake, matendo 2:37-39,
Unasubiri nini, saa ya wokovu ni sasa..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.