Shalom. Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi.
Huenda umekuwa mvivu na mzito katika kuomba mpaka ukumbushwe kila siku pasipo hivyo huwezi kuomba.. ni kwa sababu hujatambua maombi ni nini na haujafahamu nguvu iliyoko katika maombi.. ni maombi yangu kupitia makala hii Mungu akufungue macho tena ufahamu nguvu iliyopo katika maombi na kwa nini unapaswa kuwa muombaji..
Maombi nini? Ni njia ya mawasiliano kati ya Mungu na Mwanadamu. Ni kitendo cha Kiroho na cha Imani kinachomruhusu Mwanadamu kuzungumza na Mungu ana kwa ana kwa njia ya imani,kwa kumuomba Mungu msaada(kumuweka Mungu katika utendaji).
Maana nyingine maombi ni unyenyekevu mbele za Mungu.. unapoenda mbele za Mungu kuomba hiyo inaonyesha unahitaji msaada wake.. na unapokuwa na desturi ya kuomba kila siku inaonyesha unahitaji msaada wake kila wakati na kila saa. Usipokuwa muombaji maana yake unajitosheleza huhitaji msaada wake.
Na maombi anayoyahitaji Mungu ni maombi ya imani. Hivyo maombi yanayomfikia Mungu ni lazima yawe na msingi wa Imani pasi kuwa na shaka. Hata kama utaomba kwa kutilisha huruma sana na kulia usiku kucha ukiwa na shaka ndani yako na huna imani ni kazi bure.. Soma Yakobo 1: 6.
Fahamu pia Maombi ndio yanayokujengea imani siku baada ya siku unapokuwa muombaji kila siku wa masafa marefu mambi hayo yanazidi kujenga imani ndani yako.
Umewahi kufikilia kwa nini Shetani anazuia watu wasiombe? Na kwa nini mwili akili na Fikra vyote kwa pamoja viko kinyume na maombi? Wakati mwingine unapotaka kuomba unasikia uvivu,kuchoka,unajikuta unaomba juu juu tu na fikra pia zinahama!. Umewahi fikiria hili jambo?. Endelea kusoma utafahamu.
“Shetani anafanya juu chini ili usiombe kwa sababu maombi yanamuathiri yaani shetani anakushambulia usiombe kwa sababu maombi yanamshambulia na kumuharibu shetani”
Fahamu unapoomba hayo maombi hayakai kwa muda flani ndio yanajibiwa la!! Bali saa hiyo hiyo unapoomba maombi hayo yanajibiwa na inakuwa kama ulivyoomba.
Marko 11:24.“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
Ni kawaida ya Shetani kuzuia watu wasiombe maana anafahamu dhahiri kama ukiomba hatakuweza kwa namna yoyote ile utakuwa na nguvu nyingi.. na zaidi unapoomba unapata kukumbuka maagizo ya Mungu unakuwa si msahaurifu kwa sabahu kila mara unakuwa uweponi mwa Mungu na ni rahisi Roho Mtakatifu kukukumbusha.
Sasa tutajifunza kutoka kwa mtu mmoja ambae alikuwa mkamilifu na alipendwa sana na Mungu naye ni DANIELI.
Tunamsoma Danieli alikuwa ni mtu mkamilifu ambae aliadhimu kutokujitia unajisi kwa kitu chochote kile. Na ndio mtu aliepokea taarifa nyingi na kupewa kufahamu mpaka Habari za siku za mwisho na kumfahamu mpinga Kristo, na kujua hesabu ya muda uliokuwa umesalia wa wao kukaa Babeli nk.
Ukamilifu wa Danieli haukuwa katika kitu kingine zaidi ya MAOMBI. Na ndio maana Shetani aliweka zuio Danieli asiombe maana alifahamu akifanikiwa kumzuia Danieli na asiombe atakuwa amemmaliza Danieli. Hebu tusome kidogo…
Danieli 6:4 Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danielii kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.
5.Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danielii huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.
6. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.
Unaona hapo!? Katika mstari wa nne(4) walitafuta kumshataki Danieli lakini walikosa kosa lolote la kufanya wamshtaki.. yaani hakuwa na kasoro YOYOTE maandiko yanasema alikuwa mwaminifu (hutaweza kuwa mwaminifu kama si muombaji).
Wakaanza kutafuta namna ya kumuweza Danieli wakajua ni kuhusu mambo ya Mungu wake na walijua kabisa Danieli kila siku anamuomba Mungu haipiti siku hafanyi hivyo.. tena mara tatu kwa siku.
Sasa ukiendelea kusoma…
Danieli 6:7 “Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote ATAKAYEOMBA DUA kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.”
Unaona hapo? Wanazuia Danieli asiombe maana yake walifahamu ukamilifu wa Danieli upo katika maombi.. nguvu za Danieli ziko katika maombi kwa hiyo wakiweza kumzuia katika hilo watamuweza..
Hivyo shetani alifahamu hilo lakini Danieli alifahamu pia asipokuwa muombaji ni lazima ataanguka mahali fulani tu..
Unaona hapo tena zuio hilo halikuwa la mwaka mmoja bali ni SIKU THELATHINI tu yaani mwezi mmoja tu bila kufanya ibada na kuomba kazi itakuwa imeisha.. maana yake Shetani pia hataki tukae muda mrefu bila kuomba haweki vikwazo vya muda mrefu bali vya muda mfupi tu anajua katika muda huo wewe ni ngumu kufahamu tayari shetani kashakupandia magugu utakuja kuelewa baadae.
Hivyo shetani hakuwa anamuogopa Danieli ila analikuwa anaogopa kile alichokuwa anakifanya Danieli na matokeo yatakayotokea utaona pia Shetani alikuwa akizuia yale majibu ya maombi aliyokuwa anaomba Danieli ya siku 21..
Vivyo hivyo na mwili wako unakuwa mzito katika kuomba na fikra zako zinahama hata unapoingia kuomba kwa sababu mwili wako unafahamu unapokaa katika kuomba utasababisha kuzizima tamaa zake..
maana yake hautaweza kukutawala utaunyima haki ama kutimiza nia yake ambayo ni mauti.. maana nia ya mwilini ni kinyume na mapenzi ya Mungu.
Fikra nazo zinapingana na wewe na kuhama kuwaza mambo mengine kwa sababu zinafahamu zitashindwa kutimiliza mambo yake ambayo ni mawazo mabaya yanayokutia unajisi.
Fikra zinakuwa ni nyepesi kuwaza mambo mengine kwa sababu zinafahamu ukiendelea kukaa katika maombi kuna ile nia ya Kristo itakuja ndani yako nayo itakufanya upya katika kufikiri kwako na kuamua kwako..
Hivyo usipokuwa muombaji Shetani hakosi kukunasa. Na utakuwa ni mtu wa Mwilini utakuwa huna tofauti na watu wa kidunia shetani atakuburuza sana.
maana anakuwinda wewe wala hawawindi watu wa kidunia kwa sababu anajua hao tayari ni wake anachofanya juu chini ni kuhakikisha anakurudisha katika milki yake..
Kuwa macho maandiko yanasema yeye ni kama simba angurumaye akitafuta mtu ammeze na huyo mtu ni asiyeomba..
Usipokuwa muombaji sahau kuwa Mkamilifu na kutembea katika mapenzi ya Mungu na utakuwa msindikizaji katika safari ya wokovu na sahau Mungu kusema na wewe maana katika maombi Mungu anasema na sisi kupitia Roho wake..
Chukua hatua na kuwa siriazi na wokovu wako.
Uthamini,ujali kumbuka wokovu huo umepewa bure ila haujapatikana bure ni Yesu kaingia gharama usiuchukulie kawaida. Ukiwa kwenye wokovu na humuoni shetani akikutafuta ujue ameshakupata..
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.