Je umeona vema?

Biblia kwa kina No Comments

 

Yeremia 1:11 Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona UFITO WA MLOZI.

12 Ndipo BWANA akaniambia, UMEONA VEMA, Kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.

Shalom mtu wa Mungu. Karibu tujifunze biblia.

Kabla hatujaenda ndani kuangalia ujumbe wa leo, tuangalie kwanza maana ya huo mti wa mlozi alioonyweshwa nabii Yeremia kama tulivyosoma hapo juu.

Mlozi ni mti fulani, unaostawi sana sana huko mashariki ya kati (Lebanoni, Israeli, Palestina n.k), Jina lake kwa kiyahudi unaitwa “SHAKEI” na tafsiri yake ni KUTAZAMA/ KUANGALIA… Kwahiyo Yeremia kuonyeshwa pale Mti wa Mlozi ni lugha tu ya picha anayoonyeshwa kwamba Bwana ANATAZAMA, na je! anatazama nini?..

Anatazama NENO lake ili alitimize alilolinena juu ya Israeli liwe kwa ubaya au kwa wema atalitimiza tu. Na ukiendelea kusoma utagundua kuwa Bwana alikuwa akitazama neno la hukumu ambalo tayari alikuwa ameshatoa kwa vinywa vya watumishi wake kama wakina Isaya kwasababu ya maasi ya Israeli na machukizo waliyokuwa wanayafanya..na ndio maana anamwonyesha Yeremia UFITO (fimbo) tu! ya Mlozi, Ikimaanisha kuwa Mungu analitazama NENO lake, na kulitimiza juu yao kama ADHABU na sio BARAKA. Kwasababu FIMBO ni kwa ajili ya kuadhibu siku zote tunalijua hilo.

Sasa nini tunajifunza katika hilo andiko?

Mbali na mengi ambayo tunaweza tukajifunza hapo kuhusu huo Mti wa Mlozi, Kwamba Bwana analitazama Neno lake ili alitimize, ila pia Bwana anataka tujifunze KUTAZAMA/ KUONA VEMA! Kama Yeremia mtumishi wake,

Mara nyingi sana, Mungu anatuonesha mambo mengi ambayo anatamani tufumbue macho yetu na tutazame vema, ila imekuwa kinyume kwa watu wengi wanaishia kutazama vibaya,

Siku ya leo tutakwenda kutazama baadhi ya watu katika biblia ambayo waliona vema na wengine ambao waliona kinyume kisha tujifunze na sisi kuona vema. Namaanisha kuona kile Bwana alichokusudia tuone.

Na leo tuangalie mtu mmoja katika biblia ambaye anaitwa Petro, aliyekuwa mtume wa Bwana Yesu.. ,

Je! Petro alionyeshwa nini? Na akaona nini? Tusome..

Luka 4 “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.

8 Simoni Petro ALIPOONA HAYO, ALIANGUKA MAGOTINI PA YESU, AKISEMA, ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, Bwana.

9 Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwasababu ya wingi wa samaki walioupata;

10 na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.

11 Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, WAKAACHA VYOTE WAKAMFUATA.

Wapo watu wengi leo ambao wanaonyeshwa miujiza mingi, wana ushuhuda nyingi ya mambo makubwa waliyotendewa na Mungu katika maisha yao ila pamoja na hayo wanaishia tu kushangaa na kusema Mungu ni Mkuu, Ndiyo MUNGU ni Mkuu na atabaki kuwa hivyo milele ila sio kusudi la Mungu uishie tu hapo! Kuona tu huo muujiza na hauchukui hatua yoyote, utakuwa bado ujaona vema! bado hujaona kile Mungu alichokusudia uone,

Tazama Petro ALIPOONA tu huo muujiza mkuu…hakuishia tu kushangaa na kusema asante Bwana umenitendea, kama wengi wanavyofanya leo baada ya kuonyeshwa miujiza kadha wa kadha, Petro baada ya kuona hayo alianguka magotini pa Yesu, akasema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, maana yake hakustahili kufanyiwa hayo!

Na baada ya kufanya hicho kitendo cha kuanguka magotini pa Bwana (kutubu), Bwana hakumwambia Usiogope Petro wewe hauna dhambi, Bwana angeweza kumwambia nenda nimepokea shukurani zako, nitaendelea kukubariki!, ila Bwana alimwambia Usiogope Petro, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Na ndio ilikuwa kusudi la Mungu kumwonyesha Petro huo muujiza,

Kwahiyo baada ya Petro na wenzake kutendewa huo muujiza, Bwana alitegemea wote waone vema(wasione tu muujiza wa samaki wengi ila waone kilichopo nyuma ya huo muujiza), Na kweli Petro na wenzake wale wawili (Yakobo na Yohana) Ndio tu walioona vema, na Bwana akawaambia Petro UMEONA VEMA, kama tu alipomwambia Yeremia baada ya kumwonyesha ule Ufito wa Mlozi ambao ilikuwa ni lugha ya picha kama tulivyoona hapo mwanzo.

Hivyo baada ya akina Petro kuona kile ambacho walipaswa waone, waliweka MIZIGO yao kando WAKAMFUATA Bwana, na kuanzia huo wakati walianza kuwa wavuvi wa watu kama Bwana alivyokusudia toka awali, na hao watatu Petro, Yakobo na Yohana ndio waliokuja kuwa watu wa muhimu sana katika kanisa la Mungu mpaka wakaitwa NGUZO ya kanisa (Wagalatia 2:9)

ila wengine waliishia tu kuona na kushangaa ule muujiza wasione kile ambacho Bwana alikuwa anawaonyesha. Mfano halisi wa watu wa siku hizi za mwisho ambao Bwana anawaita kupitia muujiza wanayowatendea kila siku ila hawataki kufumbua macho yao waone, hawataki kuona kwamba huo muujiza waliyotendewa ni kwa ajili ya kuokoa nafsi zao na sio kufurahisha tu miili yao,

Ni ili watoke katika dhambi, waachane na uvuguuvugu, waache udunia, waache machukizo na dhambi wanazozifanya kwa siri, ila hawaoni wanaishia tu kushangaa na kutoa shukrani..

Wasijue kuwa Bwana anachotaka kwao sio wingi wa maneno ya shukurani au sio sadaka nyingi za shukurani bali ni mioyo yao kwanza watubu baada ya kuona uwepo wa Mungu.

Biblia inasema watu hawa wanafumba macho yao ili wasiokoke… hawataki kuona kabisa.

Mathayo 13:15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, NA MACHO YAO WAMEYAFUMBA; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, nikawaponya.

Je! ni mara ngapi Bwana amekuonyesha/amekutendea muujiza kwenye maisha yako, pengine alikuokoa na ajali mbaya, alikuponya na ugonywa hatari, alikuokoa na mauti, alikufanikisha mambo kadha wa kadha..ila uliishia tu kusema asante na kwenda kutoa shukurani kanisani, ndio ni vizuri kufanya hivyo,

ila unatakiwa ukae utafakari baada ya kutendewa/ kuonyeshwa huo muujiza, kisha uone kile ambacho Bwana anataka uone, Bwana anataka uache vyote umfuate, anataka uache dhambi unazotenda sirini, anataka uache uasherati/uzinzi unaoufanya kwa siri, anataka uache ulevi, uache usengenyaji, uache rushwa, uache uchawi, uache mambo yote mabaya ambayo dhamiri yako inakushudia, ndio maana ya huo muujiza,

hebu leo tafakari tena upya juu ya yale ambayo Bwana amekuonyesha/amekutendea kisha chukua hatua ya kumfuata kwa kujikana nafsi yako na kuacha machukizo yote unayoyafanya, wewe ni mwanamke kuvaa suruali ni machukizo (kumbukumbu22:5), kuvaa vimini, kusuka, kujipamba uso, kuchora mwili, kutazama picha chafu za ngono, we ni kijana unacheza kamari, una beti, unasikiliza miziki ya kidunia, n.k, hayo yote ni machukizo yanayomchukiza Mungu

Na biblia imesema WACHUKIZAO sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kibiriti Soma Ufunuo 21:8, hivyo leo fumbua macho yako uone vema, ona ishara Bwana anazotuonesha kuhusu siku za mwisho, ona dalili ambazo Bwana anatuonesha, usiwe miongoni mwa wale wanaodhihaki na kusema hakuna hukumu, Yesu harudi, maana wanafumba macho yao wasione yanayoendelea sasa na yaliyowahi kutokea sawa sawa na biblia ilivyotabiri kuwa watatokea watu kama hawa..

2Petro3:3 Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4 na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

5 MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, kwa neno la Mungu;

6 Kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

Umeona hapo! hukumu ipo, na ipo Karibu! Hizi ni siku za mwisho! Usidanyanyike!, fumbua macho yako uone vema; kisha chukua hatua ya kumfuata Bwana Yesu uwe salama, uokoke nafsi yako; kumbuka Bwana analitazama Neno lake ili alitimize.

Marko 8:34 Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataingamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

Salimisha maisha yako Kwa Kristo.. jikane nafsi yako na uchukue msalaba wako umfuate Bwana ili uokoke nafsi yako, Achana na raha za dunia hii, achana na furaha unayoipata kwenye dhambi maana mwisho wake ni uchungu usiyoelezeka.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *