Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Ni jambo la muhimu sana kulitambua hili na kujitathimini. Ipo tofauti kubwa sana kati ya kumcha Mungu na kumtumikia Mungu. Bahati mbaya sana watu wanasema wanamcha Mungu kumbe wanamtumikia Mungu tu wala hawamchi. Na siku ile Bwana Yesu hatawatambua kabisa. Tutaangalia mtu anamtumikia Mungu ni yupi na mtu anayemcha Mungu ni yupi/wa namna gani?.
Mkristo anaemtumikia Mungu ni wa namna gani?
Huyu ni Mkristo ambae anasema ameokolewa na anampenda Yesu Kristo. Lakini maisha yake yaani mwenendo wake ni tofauti kabisa na yule anaesema amemuokoa. Huyu ni Mkristo ambae kutenda dhambi kwake sio tishio kabisa ni kitu cha kawaida kwake. Anazini,anaiba,mtukanaji,mlevi,anaangalia picha za uchi, anaendana na fashion za kidunia yaani hana kiasi hajizuii kwa lolote.
Lakini pia Mkristo huyu si kwamba si muombaji anaomba sana na ananena kwa lugha na pia anaweza kuwaombea wengine na wakapona kabisa na bado anatoa mapepo na kuona maono, na kuwatabiria watu vitu vya kweli kabisa na vikatokea.
Lakini ndani yake Hamchi Bwana yaani hana hofu ya Mungu kabisa ndani yake ijapokuwa anasema ameokoka. Lakini maisha anayoyaishi ni mbali na neno la Mungu kabisa linavyomtaka awe.
Ndio maana Bwana Yesu anasema..
Mathayo 7: “21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”
Unaona katika huo mstari wa 21? Anasema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”
Bwana Yesu anamalizia kwa kusema “…BALI NI YEYE AFANYAYE MAPENZI YA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI..”
hivyo kuita Bwana Yesu, Bwana Yesu sio shida lakini je? Unayafanya mapenzi ya Mungu?
Ukiendelea kusoma mstari wa 22 hapo anaendelea kusema wengi watakuja wakisema.. hatukufanya unabii,kutoa pepo, lakini si hivyo tu hata miujiza mingi ilifanyika si miujiza ya kichawi au kishetani la! Kweli kabisa ni miujiza inayotendeka kwa jina la Yesu Kristo. Hivyo utaona hapo hawa watu walikuwa wanamtumikia Mungu lakini hawakuwa wanamcha Mungu.
Ni Wakristo wanaimba kanisani,wanatoa fungu la kumi,nk hivyo lakini Mungu hatawatambua kabisa. Ni jambo la kuogopesha sana siku ile Yesu anakwambia “SIKUJUI ONDOKA..” ndugu ogopa sana.
Mkristo anaemcha Mungu ni wa namna gani?
Mtu anaemcha Mungu kama maandiko yanavyosema..
Ayubu 1:1“Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.”
Unaona hapo mwisho kabisa anasema”…ni mmoja aliyemcha Mungu na KUEPUKANA NA UOVU”
Hivyo kumcha Mungu ni kuepukana na uovu na kumtii Mungu,kumuogopa Mungu,kumpenda,kuchukia uovu wa kila namna, kufanya ibada, nk hii ni jumla ya mambo anayokuwa nayo mtu anayemcha Mungu.
MKristo wa namna hii huyu hata anapotaka kufanya uasi haanzi kufikiria wanadamu wakijua itakuwaje lakini hofu yake yote inakuwa kwa Mungu. Kwamba akifanya hivyo atasimamaje mbele za Mungu?,atamwambia nini Mungu? Kama vile Yusufu alivyosena “nitamtendaje Bwana uovu mkuu namna hii?” Hivyo na maandiko yanasema..
2 Timotheo 2:19“Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.”
Unaona hapo Mtume Paulo anamwandikia waraka huu Timotheo anasema mwisho wa sentensi “..KILA ALITAJAYE JINA LA BWANA NA AUACHE UOVU..”
Kila anaelitaja jina la Bwana yaani aliemuamini Yesu Kristo ni lazima atakuwa ni mtu anaechukia uovu kabisa hata anapoanguka anafanya juu chini kutokurudia tena na anakaa hana amani ndani yake. Ni mtu ambae kila siku atakuwa anapiga hatua kuacha mambo yote maovu.
Hivyo Mkristo wa namna hii atazidi kumkaribia sana Mungu na kuugusa moyo wa Mungu. Na siku ile Bwana atakukaribishwa katika karamu yake.
Je! Unaepukana na uovu? Uovu hatuepuliwi nao bali ni sisi kuepukana nao na tumepewa nguvu ya kuushinda kabisa.
Waefeso 5:
3 Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;
4 wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.
5 Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.
Mkristo wa namna hii anakuwa kinywa chake hakitaji maneno maovu kama hapo juu maandiko yanavyosema. Usiwe ni Mkristo unaemtumikia Mungu tu bali unaemcha Mungu yaani unaepukana na uovu.
Kumbuka Yesu Kristo anakuja je? Unauhakika wa kwenda nae atakaporudi? Usikubali kuwa ni msindikizaji tu bali kuwa Mkristo mwenye uhakika wa kwenda Mbinguni kila siku endelea kupiga hatua na kutamani kufanana na Yesu Kristo na inawezekana kabisa. Lengo la wewe kuokolewa ni ili ufanane na Kristo.
Warumi 8:29.“Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.”
Kuwa na kiu na shauku ya kufanana na Yesu Kristo na utafanana nae kabisa.
Ubarikiwe sanaa.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.