NA WA KWANZA ATAKUWA WA MWISHO

Uncategorized No Comments

NA WA KWANZA ATAKUWA WA MWISHO

Shalom, nakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo. Karibu tujifunze biblia maneno ya uzima.

Biblia inatuambia “Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake,…” (Mhubiri 7:8), hii ni kweli kabisa, mara nyingi watu ambao wanaanza vizuri kufanya jambo Fulani hawamalizi vizuri bali ni wengine wanakuja kutokea mwishoni na kufanya vizuri, mfano tukiangalia hizi timu za mpira wa miguu..mara nyingi (sio mara zote) ile timu iliyoanza vizuri ndio baadaye inakuja kumaliza vibaya, ile ambayo hata ilikuwa haijatarajiwa kuwa ingekuja kupata ushindi..ndio inakuja kushangaza mwishoni kabisa. (Kusema hivyo haimanishi tufuatilie mipira) hiyo ni ili tuelewe mambo ya rohoni kwa urahisi, tuchukulie pia mfano wa wanariadha..mara nyingi wale walioanza vizuri kupiga mbio..mwanzoni ni rahisi kutabiri kuwa watakuwa wa kwanza, lakini cha ajabu ni kwamba wale ambao walikuwa nyuma kabisa ambao walionekana kuwa hawawezi kuwa miongoni mwa wale watakaoshika nafasi za kwanza kwanza..ndio kwanza wanakuja kuwa wa kwanza na wale wakwanza wanakuja kuwa wa mwisho japokuwa walianza vizuri.. hivyo tukirudi kwenye mambo ya rohoni…sisi tuliookoka kwa kumwamini Yesu Kristo na kuoshwa dhambi tunafananishwa na wanariadha (Wakorintho 9:24-25) hivyo Bwana wetu Yesu alisema…

Luka 13:29-30 “Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.

[30]Na tazama, WAKO WALIO WA MWISHO WATAKAOKUWA WA KWANZA, NA WA KWANZA WATAKAOKUWA WA MWISHO. “

Umeelewa maana ya hayo maneno..hayo maneno siyo ya kuchukulia kiwepesi wepesi kabisa ..ni kama tu yale ambayo alisema Siku ile wengi wataniambia Bwana, Bwana hatukufanya miujiza na kutoa pepo kwa jina lako, hatukufanya unabii kwa jina lako, na hata ukatufundisha katika njia zetu (Mathayo 7:21-22) lakini yeye atawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe. Na hapa anasema tena “WENGI walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na wa mwisho watakuwa wa kwanza” zingatia hilo neno “wengi” utasema ni wapi alisema ni wengi watakaokuwa wa mwisho ambao walikuwa wa kwanza, tuendelee kusoma katika injili ya Mathayo.

Mathayo 19:27-30 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

[28]Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.

[29]Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.

[30] LAKINI WENGI WALIO WA KWANZA WATAKUWA WA MWISHO, NA WALIO WA MWISHO WATAKUWA WA KWANZA.

Na hayo maneno ya Bwana kama yalivyo maneno yake yote yanakuja kutimia katika wakati huu wa mwisho, siku hizi kuna wakristo wengi ambao wanarudi nyuma, na wengi wa hao ni wale ambao mwanzoni walianza na moto na wakadumu kwa muda mrefu kwenye wokovu, lakini leo hii utaona wale ambao walikuwa wanasuasua…ambao hata hawakujua kweli yote, na wengine ambao walikuwa wapagani kabisa ndio leo wakisikia injili ya kweli utaona ndio wanageuka moja kwa moja na wanakuwa moto kweli kweli.

Hivyo ndugu uliyempokea wokovu wa kweli, ukabatizwa kwa maji na kwa Roho.. angalia sana jinsi mwisho wako unavyomalizia.. fahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa siku za mwisho..huu si wakati wa kutazama nyuma, sio wakati wa kuanza kupoa poa..ni wakati wa kuongeza bidii zaidi kwa maana mwisho umekaribia na Bwana alisema wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho atakuwa wa kwanza.. hivyo angalia usije ukawa wa mwisho ilihali ulianza vizuri.

Mwanzoni ulikuwa moto lakini leo umeanza kupoa, ulikuwa unafunga na kuomba kila week lakini leo kufunga na kuomba hata masaa 24 ni mzigo kwako, ulikuwa unaenda hata masaa manne hadi tano katika kuomba kila siku lakini siku hizi huoni hata shida kupitisha siku bila kuomba, ulikuwa unasoma biblia kila siku na kuitafakari lakini leo hii ni kama vile umeridhika, ulikuwa hukosi Ibadani lakini leo hata week mbili mpaka hata mwezi unapita na hauoni shida kabisa, ulikuwa unafanya kazi ya Mungu kwa bidii kwa karama aliyoiweka Mungu ndani yako lakini leo hukumbuki ni lini umetumia karama yako, hukumbuki ni lini umewashudia wengine habari njema, kwenye kutoa mkono umeanza kuwa mzito na ulikuwa mwepesi kama miguu ya kalungu, unatanguliza mambo yako kuliko kazi ya Mungu, ulikuwa unauchukia ulimwengu lakini taratibu taratibu umeanza kuupenda na kuelekeza moyo wako huko, ulikuwa unahubiri injili ya kweli na kuupenda lakini umeanza kuugeukia injili ya namna nyingine, ulikuwa unatazamia kurudi kwa Bwana muda wowote lakini leo hii ni kama umejisahau, hiyo yote ni ishara mbaya sana kwako…kwamba unataka kutimiza hayo maneno ya Bwana ambayo alisema “na wakwanza atakuwa wa mwisho na mwisho wakwanza”. Hivyo jiangalie sana jinsi unavyoenenda ndugu, na ukumbuke kuwa wokovu uliyopokea ni wa gharama sana… hivyo yatupasa kuidhamini sana na kuitetemekea kama tulivyoaswa katika..

Wafilipi 2:12 Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, UTIMIZENI WOKOVU WENU WENYEWE KWA KUOGOPA NA KUTETEMEKA.

Wokovu ni kitu cha kujali na kuidhamini sana kuliko kitu kingine chochote kile.

Luka 9:59-62 Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu.

[60]Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu.

[61]Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.

[62]Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.

Wakati mwingine uwe tayari kuhatarisha mahusiano yako na ndugu zako kwa ajili ya kutunza wokovu, kama hiyo kazi haikupi muda wa kumtafuta Mungu ipasavyo ni heri ukamwomba Bwana akupe kazi nyingine, ni heri uahirishe kufanya shughuli zako hata kama ni ya msingi sana ikiwa wokovu wako upo hatarini.

Wokovu ni wa kushikilia kwa nguvu zote, ni kupigana vita, ni kujikana nafsi kila siku, ni kushindania kwa bidii zote maana tumekabidhiwa mara moja na hivyo ukipoteza ndio basi, na adui yupo kazini kuakikisha unarudi nyuma na kuwa viguvugu, hivyo yatupasa kushindania kwa bidii sana bila kuchoka.

Yuda 1:3Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba MWISHINDANIE imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.

Je! upo kwenye ushindani kama hapo mwanzo au umerudi nyuma na kuacha kupiga mbio, hebu kumbuka ni wapi ulikoanguka ukatubu na kurudi kwenye mstari kabla mambo hayajawa mabaya sana. Biblia inasema”msipe ibilisi nafasi”.

Unyakuo wa Kanisa umekaribia sana kuliko watu wengi wanavyodhania..unaweza hata ukawa leo. Hivyo huu ni wakati wa kuongeza bidii katika mambo ya rohoni Zaidi ya yale ya mwilini kwasababu itakufaidia nini kupata furaha ya dunia na ukakosa kunyakuliwa.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *