Maombi yanayompendeza Mungu.

Maombi na sala No Comments

Maombi yanayompendeza Mungu.

(Omba Mungu akupe moyo wa hekima zaidi ya mali)

Kwanini tunapaswa kumuomba Mungu atupe hekima zaidi ya mali? Kwani! ni vibaya kuwa na mali?

Kuwa na mali sio vibaya na tunahitaji, lakini pia tukikosa hekima, hata hiyo mali pia hatuwezi kutumia vizuri.

Sulemani Mfalme wa Israeli mwana wa Daudi, Ni mtu aliyempendeza Mungu sana hata kufikia hatua ya kuambiwa aombe lolote naye atapewa…Tunaona Mfalme akachagua kuomba Hekima badala ya Mali, na Maarifa badala ya Ufahari na nguvu za kijeshi…sio kwamba alichagua hivyo kwasababu alikuwa hapendi utajiri au ufahari, hapana alikuwa anaupenda na kuutamani, lakini alipiga hesabu awe na utajiri na nguvu za kijeshi kuliko wafalme wote duniani, halafu akose akili ya namna ya kuwaongoza na kutatua matatizo ya watu wake itamfaidia nini?..Kwahiyo akaona jambo la kwanza la kuchagua ni akili na hekima kwanza , na hayo mengine yatafuata mbele ya safari kama yatakuwa na ulazima. Tunasoma ..

1 Wafalme 3:4 Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile.

[5]Na huko Gibeoni BWANA akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.

[6]Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo.

[7]Na sasa, Ee BWANA, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia.

[8]Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi.

[9]Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?

[10] NENO HILI LIKAWA JEMA MACHONI PA BWANA, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.

[11] MUNGU AKAMWAMBIA, KWA KUWA UMEOMBA NENO HILI, WALA HUKUJITAKIA MAISHA YA SIKU NYINGI; WALA HUKUTAKA UTAJIRI KWA NAFSI YAKO; WALA HUKUTAKA ROHO ZA ADUI ZAKO; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;

[12]basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.

[13] NA MAMBO YALE USIYOYAOMBA NIMEKUPA, MALI NA FAHARI, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.

[14]Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi.

Umeona maombi yanayompendeza Mungu. Hebu leo tupewe na sisi nafasi kama hiyo, Mungu atuambie tuombe lolote naye atatupa…Utaona wengi wetu mambo tutakayoyakimbilia kwanza, tupewe mali nyingi na utajiri ili tuishi maisha ya raha sisi na familia zetu, na ndugu zetu na ukoo mzima…Lakini ni wachache sana watachagua Mungu awape Hekima na akili za kuwapenda wenzi wao na ndugu zao, na akili na maarifa ya kuwalea watoto wao katika njia inayopasa kutokujali kiwango cha utajiri au umaskini walichonacho…Hilo ndio lingetakiwa liwe jambo la kwanza la kuomba kisha hayo mengine ndio yafuate.

Kwasababu itakufaidia nini, uwe na fedha nyingi na utajiri mwingi na kuwatimizia watoto wako mahitaji yote na Mwisho wa siku wanakuja kuwa mashoga au makahaba? Si ni afadhali wale chakula cha kawaida kila siku lakini ni matajiri wa akili na hekima, walizozipata kutoka kwako na mwisho wa siku watakapokuja kuwa wakubwa watakuwa msaada kwako na kwa wengine?..au itakufaidia nini uwe na mali nyingi na fedha nyingi lakini mke wako au mume wako haoni raha ya kuishi na wewe?..unapata mali lakini unakosa hekima ya jinsi ya kuishi na mume/mke. Hiyo ni hatari sana…

Ndugu Hekima ni kitu kikubwa sana…Ndio maana utaona ni kwanini mtu mmoja anakaa na mke wake au mume wake mwenzi mmoja au mwaka mmoja wameachana, na mwingine hana fedha wala si tajiri lakini wameishi na mwenzi wake miaka zaidi hata ya 40 na bado wanapendana na kuvumiliana, ni kwasababu ya hekima iliyopo ndani ya hao wawili..Sio kwamba hawajawaji kukosana kabisa, wanakosana lakini kila kukitokea kutokuelewana kidogo tu! Mmoja wao anatumia hekima ya kiMungu kutatua hilo tatizo kabla hawajafika mbali kabla hawajakwenda kumwambia mama mkwe au babamkwe au marafiki, hekima iliyo ndani yao inawapeleka kwenye unyenyekevu, upendo, uvumilivu, ustaarabu, kusitiriana, kuchunguza jambo kabla ya kuchukua hatua,kujadiliana, kusameheana nk.

Lakini hao wengine waliokosa hekima utaona kukitokea tatizo kidogo tu! Moja kwa moja mguu wa kwanza ni kwa marafiki na mashosti kuwaelezea kinachoendelea kati yao na wenzi wao..Na ndio huko huko shetani anapata nafasi wanapata ushauri wa kipepo wa kuachana na kuaibishana wakati mwingine, na mwisho wa siku ndoa inavunjika. Na sio tu katika Nyanja ya ndoa, bali katika Nyanja zote za maisha Hekima ni jambo la muhimu sana, ukikosa huwezi kuendesha maisha yako.

Hivyo Ndugu leo umefahamu jambo linalompendeza Mungu zaidi kuomba, hivyo achana na hayo maombi unayoomba au unayoombewa kila siku ya mafanikio ya biashara yako na kazi yako, anza kuomba hekima..Biblia inasema..

Mithali 16:16 “ SI AFADHALI KUPATA HEKIMA KULIKO DHAHABU? NAAM, YAFAA KUCHAGUA UFAHAMU KULIKO FEDHA.”

Ukiona matatizo kama hayo yamekutokea na unashindwa namna ya kuyatatua ni dhahiri kuwa umepungukiwa hekima na sio kingine..Na kupungukiwa hekima sio dhambi, ni udhaifu tu ambao kila mtu anazaliwa nao, na hivyo unaweza ukaondoka endapo mtu akitaka uondoke!..Kwahiyo unachotakiwa kufanya ni KUOMBA HEKIMA KWA MUNGU!.

➽Yakobo 1: 15 ‘’LAKINI MTU WA KWENU AKIPUNGUKIWA NA HEKIMA, NA AOMBE DUA KWA MUNGU, AWAPAYE WOTE, KWA UKARIMU, WALA HAKEMEI; NAYE ATAPEWA.

6 Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.

7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.

8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote”.

Neno limetushauri kama tumepungukiwa na Hekima na tuombe, Sulemani aliomba hekima kwasababu aliona amepungukiwa..na sisi vivyo hivyo, tunapaswa tuombe!

Lakini tunapaswa tuombe kwa imani na pasipo kusitasita.

Sasa Maana ya kuomba kwa imani ni nini?.

Maana yake unapaswa uombe, ukiwa ndani ya IMANI ya YESU KRISTO, na ukiwa na uhakika kwamba Mungu unayemwomba anakusikia na anawapa thawabu watu wajinyenyekezao kwake!..ukiwa nje ya Imani ya Yesu Kristo ni ngumu kupokea hiyo hekima, kwasababu hiyo Hekima ndio Yesu Kristo mwenyewe. Na pia hutakiwi kusita sita..Maana ya kusitasita ni kuwa na mawazo mawili… “mawazo ya ..aa sijui itawezekana, sijui nimesikiwa?”..na mawazo ya kushika hili na lile kwa wakati mmoja!! Kwasasa lenga jambo moja tu! Kumwomba Mungu hekima, usianze kuomba; Bwana naomba hekima, unipe na utajiri nipate hela,unipe na magari matatu, nyumba,unipe maisha marefu, unipe na biashara kubwa ya kimataifa n.k

HUKO NI KUSITA-SITA KWENYE MAWAZO MAWILI na hakumpendezi Mungu, ni sawa na mwanajeshi anayekwenda vitani na kumwomba kamanda wake ampe bunduki tatu za kubeba, mabomu sita, ampe na ndege ya vita na kifaru cha kisasa, ampe na mboksi matatu ya risasi, visu ishirini, ampe na kombora moja la nyuklia..Ni wazi kuwa huyo mwanajeshi hajiamini na hafai kwenda vitani..Na sisi hatupaswi kuwa hivyo.Kusita sita kwa kushika mambo mawili kwa wakati mmoja, Tunatumia silaha MOJA YA HEKIMA KWANZA, hizo nyingine zitakuja baadaye. Kama Sulemani alivyofanya hakuanza kumwambia Mungu naomba hekima, unipe na watoto sita waje kuwa wafalme, unipe na maisha marefu,unipe na utajiri, unipe na umaarufu na ufahari dunia nzima wanijue…hapana hakufanya hivyo hakusitasita kwenye mawazo mawili aliomba jambo moja kuu kwanza HEKIMA, na hayo mengine Mungu atayafungua mbele ya safari.

Tunasoma..

1 Wafalme 3; 9 “Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?

10 Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.

11 Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;

12 basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.

13 NA MAMBO YALE USIYOYAOMBA NIMEKUPA, MALI NA FAHARI, HATA HAPATAKUWA NA MTU KATIKA WAFALME KAMA WEWE, SIKU ZAKO ZOTE”.

Unaona Mungu anamwambia Sulemani nimekupa HATA YALE MAMBO USIYOYAOMBA! Tatizo kubwa lililopo katika Ukristo leo hii, ni kushindwa kuelewa kuwa Mungu anajua mahitaji yetu kabla hata ya sisi kumwomba, hata pasipo kumwambia anaweza kukutimizia mahitaji yako endapo utakuwa UMESHIKA JAMBO MOJA KUU NA LA MUHIMU.

Mungu si mwanadamu, au hana udhaifu wa kibinadamu wa kusahau kuwa hitaji moja linategemea lingine, umemwomba kiatu anajua kabisa utajitaji na soksi, kwasababu huwezi kuvaa kiatu bila soksi, kwahiyo siku atakapokujibu ombi la kiatu atakupa na soksi hapo hapo..atakutengenezea na mazingira ya kupata fedha ya kwenda kukisafisha na kukipiga rangi pia… Lakini tanguliza kwanza ombi la msingi la kuomba kiatu, ili hayo mengine Bwana akuongezee.

Na leo hii shika jambo hili moja kuu na la Muhimu “HEKIMA” Itafute hiyo na hayo mengine yote utazidishiwa, mali, maisha marefu, watoto, heshima, ukwasi n.k lakini la kwanza ni Hekima.

Mungu akubariki sana.

Tafadhali “share” Ujumbe huu kwa wengine.

Na Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *