TENA HABARI NJEMA YA UFALME ITAHUBIRIWA KUWA USHUHUDA KWA MATAIFA YOTE.

Siku za Mwisho No Comments

TENA HABARI NJEMA YA UFALME ITAHUBIRIWA KUWA USHUHUDA KWA MATAIFA YOTE.

Mathayo 24:14 “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja”.

Bwana Yesu asifiwe ndugu mpendwa..

Ukitaka kujua kuwa mambo yote sasa yameshakamilika, kinachongojewa ni UNYAKUO tu, angalia hali ya mwitikio wa Injili sasa hivi. Embu fananisha watu waliokuwa wanamjia Kristo kipindi cha mitume, na watu wanaookoka sasa katika kipindi chetu hichi.

Kipindi kile injili ilipokwenda kuhuburiwa mahali kwa mara ya kwanza, mwitikio wa watu wa kumgeukia Kristo ulikuwa ni wa kustaajabisha sana, utakumbuka baada ya Pentekoste tu, kanisa lilikuwa likijiongeza kwa idadi ya maelfu, kwa injili ndogo sana. Na ndio maana kwa kipindi kifupi sana, ukristo ulienea ulimwenguni kote, na sio kuenea tu, badi kuhubiriwa (Wakolosai 1:6, 1Wathesalonike 1:8).

Lakini angalia sasa, mambo ni tofauti hakuna mtu asiyeifahamu injili, au kuzijua habari za Kristo, wote tunazifahamu, lakini jiulize kwanini, watu hawataki kuokoka, kinyume chake ndio wanakwenda mbali kabisa na Ukristo..Hiyo ni kuonyesha kuwa mavuno yameshakwisha shambani, kilichobaki ni magugu tu.

Na hiyo imepelekea sasa injili kubadilika sio tena ya kuwavuta watu, bali ni ya ushuhuda. Unapoona, injili imekufikia hapo ulipo kitandani kwako ukiwa umeishika simu yako na kusoma, ujue hiyo sio ya kukuvuta wewe, hiyo ni ya ushuhuda tu, ukiona injili imekufikia hapo sebuleni kwako unapotazama tv na familia yako, injili inakufikia kwenye hivyo vipeperushi unavyovisoma huko mitaani. Unapewa biblia bure ya kwenye simu yako, mambo ambayo hata zamani hayakuwepo. Basi ujue hiyo sio injili ya kukuvuta tena kwa Kristo ndugu. Ni injili ya USHUHUDA Tu. Ili utakapokufa katika dhambi zako, usiwe na sababu ya kusema sikuwahi kusikia, au kuona, au kuambiwa..usiwe na udhuru.

Mtu mmoja aliniambia wakati namshudia habari njema aokoke, akanijibu mbona huyo Yesu nimemsikia hata kabla wewe hujazaliwa, akaendelea kuniambia kila mtu amesikia habari za Yesu kwahiyo nisipoteze muda niende kuendelea na mambo mengine.

Sasa ni kweli kila mtu amesikia habari za Yesu Kristo, lakini injili tunayohubiri sasa hivi ni injili ya ushuhuda…kwasababu hiyo, ule mwisho umekaribia.

Moja ya siku hizi ambazo zinahesabika, tutashuhudia mabadiliko makubwa sana duniani. Tutashuhudia tendo kuu la Unyakuo wa kanisa.

Ndio yale maneno ambayo Bwana Yesu alisema, .(Mathayo 24:40-42) yatatimia hapo. Usiku huo wawili watakuwa wamelala mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wanasaga(ikimaanisha watakuwa katika biashara zao), mmoja atatwaliwa mmoja ataachwa. Wale watakaoachwa, huku duniani kitakachokuwa kinaendelea ni vilio na kusaga meno. Wakijuta kwanini kipindi kile hawakuitii sauti ya Mungu, ilipokuwa inawavuta kwake kwa upole. Watalia na kuomboleza, kweli kweli, ndugu usiwe mmojawapo.

Lakini watakaokuwa wamenyakuliwa, moja kwa moja wataelekea mbinguni wakiwa na miili yao ya utukufu, katika ile karamu ya mwana-kondoo. Kwenye raha isiyokuwa na kifani. Wakifutwa machozi kwa taabu zao walizokuwa wanapitia huku duniani kwa ajili ya Kristo.

Ndugu mambo haya unaweza kuona kama ni hadithi, au mambo yatakayotokea miaka elfu 1 mbeleni, usijidanganye. Yesu aliposema TUBUNI, kwa maana ufalme wa mbinguni UMEKARIBIA. Alikuwa hasemi uongo. Ni kweli ufalme wa mbinguni ulikuwa umekaribia, jiulize sisi wa sasa hivi tusemeje?.

Maanisha kugeuka, unaposikia injili hii ya ushuhuda kwa wakati huu.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *