ADUI AKIONA AMESHINDWA ANAKUJA KWA HILA.

Biblia kwa kina No Comments

ADUI AKIONA AMESHINDWA ANAKUJA KWA HILA.

Si kila wakati ibilisi atakuja kama mpingamizi, au mharibifu, hapana, lengo lake litakuwa ni hilo ndio, lakini akijua hawezi tena kuja moja kwa moja, atakuja kwa ujanja wa kujionyesha ameshindwa wewe una nguvu nyingi, atajiweka chini yako, ajifanye kuwa yeye siku zote ni mnyonge tu.. lakini kumbe ameshakuweza. Ndicho kilichomtokea Yoshua alipovuka Jordani, sababu mojawapo ya yeye kushindwa kuwaondoa wenyeji  wote wa Kaanani ilikuwa ni hiyo, ya kumsikiliza shetani unyonge wake. Pale walipojifanya, wametokea nchi ya mbali, wanaomba sharti ya amani wasidhuriwe, kwasababu wamesikia ushujaa wao,  kumbe ni watu wa karibu tu.

Yoshua 9:1 Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng’ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo;

[2]ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja.

[3]Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai,

[4]wao WAKATENDA KWA HILA, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyoraruka-raruka, na kutiwa viraka;

[5]na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuingia koga.

[6]Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi.

[7]Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mwakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi?

[8]Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Nanyi mwatoka wapi?

[9]Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako twatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la BWANA, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri,

[10]na habari ya hayo yote aliyowatenda wale wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa huko ng’ambo ya pili ya Yordani, maana huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, aliyekuwa huko Ashtarothi.

[11]Kisha wazee wetu, na wenyeji wote wa nchi yetu, walinena nasi na kutuambia, Chukueni vyakula mkononi mwenu kwa ajili ya safari, mwende mkawalaki watu hao, na kuwaambia, Sisi tu watumishi wenu; basi sasa fanyeni agano nasi.

[12]Huu mkate wetu tuliutwaa ukali moto katika nyumba zetu, siku hiyo tuliyotoka kuja kwenu, uwe chakula chetu; lakini sasa, tazama, umekauka, na kuingia koga;

[13]na viriba vyetu hivi, tulivyovitia divai, vilikuwa ni vipya; sasa, tazama, vimeraruka-raruka; na haya mavazi yetu na viatu vyetu vimekuwa vikuukuu kwa vile tulivyokuja safari ya mbali sana.

[14]Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA.

[15]Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia.

[16]KISHA IKAWA, MWISHO WA SIKU YA TATU BAADA YA KUFANYA HILO AGANO NAO, WALISIKIA HABARI YA KUWA WATU HAO NI JIRANI ZAO, na ya kwamba waliketi kati yao.

Soma tena, habari ya washami walipoona wameshindwa mbele ya Israeli walitenda kwa hila, wakajifanya wanataka amani…kumbe ni maadui.

1Wafalme 20:26 Basi ikawa mwakani, Ben-hadadi akawahesabu Washami, akakwea mpaka Afeki ili apigane na Israeli.

[27]Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.

[28]Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, BWANA ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi BWANA.

[29]Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.

[30]Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani.

[31]Watumwa wake wakamwambia, Angalia sasa, tumesikia ya kuwa wafalme wa nyumba ya Israeli ni wafalme wenye rehema; tafadhali, TUVAE MAGUNIA VIUNONI, NA KAMBA VICHWANI, TUMTOKEE mfalme wa Israeli; labda atakuokoa roho yako.

[32]Basi wakajifungia magunia viunoni, na kamba vichwani, wakamjia mfalme wa Israeli, wakasema, Mtumwa wako Ben-hadadi asema Roho yangu, nakusihi, iishi. Akasema, Je! Yu hai bado? Ni ndugu yangu yeye.

[33]Wale watu wakaangalia sana, wakafanya haraka kulishika neno hilo kama ni nia yake, wakasema, Ndugu yako, Ben-hadadi. Akasema, Haya! Nendeni mkamlete. Ndipo Ben-hadadi akamtokea, naye akampandisha garini.

[34]Na Ben-hadadi akamwambia, Miji ile baba yangu aliyomnyang’anya baba yako nitairudisha; nawe utajifanyia njia huko Dameski, kama baba yangu aliyoifanya huko Samaria. Ahabu akasema, Nami nitakuacha kwa mapatano haya. Akafanya mapatano naye, akamwacha.

Leo hii mapepo yanaweza kukusifia sana, kujishusha, kusema wewe ni mkuu, unatisha,una upako, una nguvu, yakajifanya yanatetemeka mbele zako, ili tu uchukulie mambo rahisi rahisi, lakini kumbe tayari yanatenda kazi kwa nguvu ndani yenu bila kujua.. Usikisikilize kilio cha shetani. Ni mwongo.

Shetani akishaona una kitu ndani yako cha ki-Mungu atakuja kwa njia ya msaada au utetezi, na kwa unyenyekevu kuwa makini sana na misaada unayoipokea katika utumishi wako au unachokifanya. Hakikisha unaifahamu na unaelewa kwa undani nyuma yake kuna roho gani. Vinginevyo utaingia katika matatizo makubwa sana.

Halikadhalika usiwe mwepesi wa kufanya mapatano na mtu/watu usiowajua, wengine ni maajenti wa ibilisi. Hivyo unapaswa kutafuta kwanza amani ya Mungu kabla hajapokea chochote. amani ya Mungu unatafuta kwenye maombi. Laiti Yoshua angeuliza kwanza kwa Mungu asingeingia kwenye huo mtego… lakini biblia inasema hawakutaka shauri kwa Bwana.

Yoshua 9:14 Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA.

Shetani ana hila, ni muongo… hivyo hatukosi kuzijua hila zake kwa kuwa watu wa maombi sana.

Lakini kama hujaokoka fahamu kuwa huwezi kamwe kujua uongo wa shetani, utabaki kutumikishwa huku ukidhani uko salama kumbe umedanganywa siku nyingi.

Hivyo kumbuka hizi ni siku za mwisho kweli kweli, siku yoyote unyakuo utapita, na ibilisi analijua hilo, na ndio maana anafanya kazi kwa nguvu nyingi sana kutafuta watu wa kuwameza.

Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kumfuata Yesu. Ili akuweke huru.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *