Anasa ni nini? Na kwanini ni dhambi kwa mkristo kuishi maisha ya anasa.
Anasa linatotoka na neno la Kiarabu lenye maana ya raha au starehe tele katika maisha ya binadamu.
Anasa mara nyingi hujumuisha kumiliki vitu fulani vya thamani kubwa, au kuishi mazingira fulani, au kutumia vyakula fulani, au kitu chochote cha kufurahisha mwili ambacho mara nyingi ni cha gharama lakini si ya lazima.
Hivyo tunaweza kusema anasa ni tabia zote za kuistarehesha nafsi na mwili kupita kawaida.
Na mara nyingi watu ambao wanapenda maisha ya anasa wanaishia kuwa maskini, hili lipo wazi tumeshuhudia wenyewe, na pia biblia inathibitisha.
Mithali 21:17 ”Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.’
Ni ukweli watu wanaopenda maisha ya anasa, mwisho wao huwa ni kutofanikiwa. Kwasababu kile wanachokipata ambacho kingepaswa kiwekwe akiba kwa wakati wa baadaye au kiwekezwe kizalishe zaidi, wao hutumia chote katika starehe mfano wa pombe, uasherati, na kununua vitu vya gharama kubwa, lengo tu asionekane amepitwa na wakati, au aonekane wa kisasa.
Hapo anaposema apendaye mvinyo na mafuta, hayo mafuta yanayozungumziwa hapo ni marashi ya gharama ambayo zamani waliokuwa wananunua ni matajiri. Ni sawa na leo labda mwajiriwa analipwa mshahara wa laki tatu (3) kwa mwezi, halafu anakwenda kununua perfume (marashi), ya laki 2, ili tu aonekane wa kisasa, hiyo ni anasa, na mwisho wake ni umaskini.
Anasa ni tunda la majivuno, na kukosa adabu. Hivyo biblia inamfundisha mwanadamu yoyote kuwa, anasa ni kinyume cha mafanikio.
Lakini pia rohoni, anasa ni zao la ufukara wa ki-Mungu. Mtu wa anasa, hutumia muda wake vibaya, kwasababu nyakati zake za ziada huishia kwenye starehe za kimwili na sio kwenye mambo ki-Mungu.
Bwana alisema;
Luka 8:14 Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.
Umeona? Anasa husonga mbegu ya Mungu ndani yako.
Katika kizazi cha sasa anasa ni pamoja na kushinda kwenye tv kutazama muvi kila kukicha, ni pamoja na kushinda mitandaoni kufuatilia vipindi vinavyokupa raha za kimwili na kihisia lakini havikujengi rohoni, ni kuwekeza muda wako katika matanuzi ya mijini na kwenye sherehe-sherehe za kila mara ambazo hazina mpangalio. Muda wote akili yako ipo katika kile kitu wanachosema “ku-party weekend” na marafiki. Ushikapo simu yako, usiku wote ni kuchat, na wale wanaowaita ma-boyfriend na ma-girlfriend. Muda ambao ungepaswa kusoma Neno na kuomba.
Sasa ikiwa wewe umeokoka, na una mwenendo huo wa maisha, usitazamie hapo utazalisha kitu. Utabakia kuwa Yule Yule milele. Biblia inasema ni heri kuona kwa macho kuliko kutangatanga kwa tamaa(Mhubiri 6:9). Sio kila taarifa uifuatilie, sio kila kitu ukitende, viache vingine vikupite, ili upate nafasi ya kuwa karibu na Mungu wako, uwe mtu wa matunda. Komboa wakati.
Hizi ni zama za uovu. Na biblia imetufundisha tusiipende dunia. (1Yohana2:15).
Mtu yoyote anayesema ameokoka na ni mkristo na huku anaishi maisha ya anasa, maisha ya kuupenda ulimwengu na kufurahia tamaa zake kama mipira, miziki zake, magemu, mitindo ya uvaaji kama suruali kwa wanawake kama fashion, magauni ya mipasuko na ya kubana, nywele na kucha za bandia au kupaka rangi, lipusticks, mekaups, cheni, bangili, vipini, hereni, pete za urembo, kusuka rasta au mtindo yoyote, kuchonga nywele, kunyoa kiduku/denge, mwanaume kuvaa milegezo, suruali za kubana/modo, kuvalia mavazi ya thamani kwa lengo la kujionyesha, kucheza michezo kubashiri kama betting/kamari, pool table, na namna zote za kidunia, huko ndiko kuupenda ulimwengu/dunia na hiyo ndio maana kuishi maisha ya anasa ambayo ni najisi kwa mkristo, hivyo mtu akisema ameokoka na bado anaishi maisha hayo…mtu huyo anajidanganya nafsi yake mwenyewe na anahitaji msaada wa kuokoka.
Hivyo ikiwa ni wewe, na umeyafahamu leo haya.. usiendelee kuishi maisha hayo na kudanganywa au wewe mwenyewe kujidanganya kuwa umeokoka, fahamu kuwa hujaokoka na unahitaji kuokoka. Hivyo dhamiria leo kumpa Yesu maisha yako kweli kweli kwa kumaanisha kutubu na kuacha anasa zote na tamaa za ulimwengu.
Anasa yetu ni kupenda kuishi maisha ya utakatifu, kupenda maombi na ibada, kupenda kusoma biblia na kushudia kwa watu huko ndiko furaha yetu iliko, starehe yetu ni kukesha katika kuomba na wala sio kama wengine wakeshao bar, na kwenye vibanda vya sinema, starehe yetu hasa ni kulewa kwa kujazwa Roho Mtakatifu na sio kama wengine wanaolewa kwa pombe na mambo ya kidunia, utajiri wetu ni kuleta watu kwa Yesu na kuujenga ufalme wa Mungu wetu na sio kuwekeza kwenye utajiri wa hapa duniani kwani makao yetu ya milele sio hapa… hivyo utajiri wetu hasa upo kule juu, nyumba, magari na maisha ya lakishari yapo kule juu.
Je! Umempokea Yesu ipasavyo?
Ikiwa upo tayari kumpokea Yesu wa kweli na hujui ufanye nini, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii nasi tutakusaidia bure.
Usiache kushea na wengine habari hizi njema.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.