SANAMU ZINAZOTEMBEA

Biblia kwa kina No Comments

SANAMU ZINAZOTEMBEA

Je! Unafahamu kuwa kuna sanamu zinazotembea? (Zizungumzii yale maroboti yanayoendeshwa kwa umeme).

Kwa kawaida sanamu yoyote haiwezi kutembea wala kufanya jambo lolote kwasababu haina uhai ndani yake, ni kama jiwe tu. Kweli inaweza kuwa na miguu mizuri lakini haitembei, inaweza kuwa na mikono lakini haishiki, inaweza kuwa na macho mazuri lakini hayaoni, na vile vile mdomo lakini haineni…hiyo ndiyo sanamu.

Na katika biblia kuna aina kuu tatu za sanamu.

1.Sanamu zenye mfano wa Mtu

2.Sanamu-watu

3.Sanamu-vitu

✓Sanamu zenye mfano wa mtu ni vitu vyote visivyo na uhai vyenye mfano wa mtu, ambavyo vinatengenezwa na watu kwa lengo la kuabudiwa.

Tabia ya hizi sanamu kulingana na biblia ni kwamba zina midomo lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazinusi..na wanaoziabudu wanafanana na hizo kiroho.

Zaburi 115:4 “Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.

5 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,

6 Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,

7 Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.

8 WAZIFANYAO WATAFANANA NAZO, KILA MMOJA ANAYEZITUMAINIA”

Hizi ndio zile zote zinazoabudiwa na wapagani, pamoja na baadhi ya madhehebu yajiitayo ya kikristo. Utakuta sanamu imewekwa ndani ya nyumba ya ibada, na watu wanakwenda kuiangukia na kuisujudia, hata kuitolea sadaka na kuiomba, jambo ambalo ni machukizo makubwa..

Sanamu-watu (Sanamu zinazotembea)

Hii ni aina ya pili ya sanamu ambayo ni tofauti kidogo na ile ya kwanza… ile ya kwanza ina midomo lakini haisemi, ina macho lakini haioni, ina masikio lakini haisikii…. Hii ya pili nayo ni hivyo hivyo, ina macho lakini haioni, ina masikio lakini haisikii, ina macho lakini haioni..tofauti tu ni kwamba ile ya kwanza haitembei ila hii inatembea, ile ya kwanza haipumui ila hii ya pili inapumua, ile ya kwanza imetengenezwa kwa miti, udongo, chuma, fedha au dhahabu lakini hii ya pili ni Wanadamu. Kwa nje inaonekana zina miguu ya kutembea na zinatembea lakini kwa ndani imeganda haitembei, kwa nje inaonekana ina uhai, ina pumua, inakula, inaongea, n.k lakini katika roho ni Sanamu. Haina tofauti na ile ya miti. Hizi ndizo Sanamu zinazotembea, na leo ndio tunazungumzia.

Sasa tunaisoma wapi katika biblia…

Ezekieli 12: 1 “Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

2 Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, WATU AMBAO WANA MACHO YA KUONA, ILA HAWAONI, WANA MASIKIO YA KUSIKIA, ILA HAWASIKII; kwa maana ni nyumba iliyoasi”.

Umeona? Kumbe sanamu sio tu mawe na udongo vinavyoweza kuwa sanamu bali hata watu..

Kama hujamaanisha kumfuata YESU wewe ni SANAMU.. Kwasababu una macho lakini huoni mambo ya rohoni, una masikio lakini husikii sauti ya MUNGU, Una kinywa lakini hakineni mambo ya Mungu, Hivyo wewe ni sanamu pamoja na viungo vyako vyote.

Kwa ufupi mtu yoyote aliye nje ya wokovu ni sanamu inayotembea!!

Mtu ambaye hajali hatima ya roho yake, yeye masaa yote anasumbukia tu maisha ya mwilini, ukimletea habari za kutubu dhambi anaona kuwa unamharibia furaha yake, ukimletea habari zinazohusiana na hatima ya roho yake anaona unampotezea muda, mtu huyu kwa Mungu ni mfu, ni sanamu inayotembea.

Ndio maana Bwana alimwambia yule mtu aliyeomba ruhusa ya kwenda kumzika baba yake, alimwambia..

Mathayo 8:21 Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.

[22]Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; WAACHE WAFU WAZIKE WAFU WAO.”

Umeona hapo, hebu tafakari hiyo kauli “waache wafu wazike wafu wao” Maana yake kuna wafu wanaotembea na wafu wasiotembea ndiyo tafsiri yake. Maana ni ile ile Sanamu zinazotembea na sanamu zilizoganda.

Kuna watu ambao ni wafu wako hapa duniani wanatembea, wengine wapo makanisani, na wengine wapo mitaani. Wanachosubiria tu ni ile siku ya ufunuo, ambao wafu wote walioko makaburini wataisikia sauti ya Mwana wa Adamu, nao watafufuliwa kwa ajili ya hukumu.

Yohana 5:28-29 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.

[29]Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.

Je! wewe unayesoma ujumbe huu ni mkristo halisi au ni sanamu inayotembea? majibu unayo mwenyewe.

Kama unaisikia injili kila siku inayokuambia ulevi, uasherati, utukanaji, rushwa,uvaaji mbaya ni dhambi, mustarbation, usagaji, na pornography ni machukizo, kuvaa mavazi yampasayo jinsia nyingine ni machukizo, kusikiliza miziki za kidunia, filamu zenye maudhui ya uasherati, kunyoa mitindo ya kidunia/kiduku ni dhambi, kubeti, kucheza magemu, kujichua, kubadilisha rangi ya ngozi yako/mekaups, kubadilisha rangi ya kucha na nywele zako Mungu alizokuumbia ni dhambi…na bado unaendelea kufanya hayo machukizo, ni wazi kuwa wewe ni maiti/sanamu inayotembea kwasababu una masikio lakini husikii, una macho lakini huoni kuwa hiyo njia unayopita inakupeleka jehanamu.

Ni maombi yangu Bwana ayafufue leo hayo macho yako na masikio yako ya rohoni ili ubadilike na kuacha njia zako mbaya.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *