NEEMA YA YESU HAITADUMU MILELE

Biblia kwa kina No Comments

NEEMA YA YESU HAITADUMU MILELE

Shalom

Ulishawahi kutafakari haya maneno ambayo Yesu aliwaambia wanafunzi wake?

Yohana 11:9 “Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu.

[10]Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake”.

Utajiuliza ni kwanini Bwana Yesu alijifananisha na Nuru ya ulimwengu? Ambayo ni JUA linalofanya kazi saa kumi na mbili tu, Ukilitafakari hilo kwa ukaribu ndipo utakapofahamu kuwa hii neema tuliyopewa sio ya kuichezea hata kidogo.

Alitumia mfano wa asili kabisa wa kitu kinachoitwa JUA”, jinsi linavyotembea, ili kutupa picha halisi ya neema yake jinsi inavyokuwa.

Kwa kawaida jua linapozama upande mmoja, huwa linachomoza upande wa pili wa dunia. Wakati hawa wamelala, wengine wanaamka, na wakati wengine wanaamka, hawa wanalala.

Ndivyo Yesu alivyojifananisha yeye ni kama Nuru ya ulimwengu huu (yaani JUA).

Yohana 12:46 “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.

Akiwa na maana kuwa, hana tabia ya kudumu milele sehemu moja, au kwa mtu mmoja, anatembea kama jua, Anachomoza kwa mtu mmoja, na wakati huo huo anazama kwa mwingine.

Leo akikujia na kuugua moyoni mwako uache dhambi, ujue kuwa hatafanya hivyo kwa kila mtu, Kuna mwingine tayari ameshafunga mlango huo kwake, na ndio maana huwezi kuona leo hii watu wote wanaokoka au wanamwamini Yesu kwa mpigo.

Wapo ambao tayari neema ilishafungwa kwao, na hiyo yote ni kutokana na kwamba waliipuzia injili ya Kristo kwa muda mrefu walipokuwa wanahubiriwa. Ukiona moyoni mwako una hofu ya dhambi na hukumu ya jehanumu, ujue neema hiyo bado ipo kwako, hivyo chukua uamuzi wa haraka sana, kumpokea Yesu.

Utafika wakati, hiyo neema itaondoka na kwenda kwa mwingine ambao hawajawahi kusikia injili kabisa, na wewe ukabakia kuwa mtu wa kudhihaki na kuupuzia injili kama unavyoona kwa hao wengine, kwani nguvu ya kukuvuta tayari haipo ndani yako, usiku wako umeshaingia. Ukishafikia hatua hiyo ndio basi tena, hakuna tumaini ndani yako.

Hivyo ndugu ikiwa leo hii, unasikia msukumo fulani wa kumgeukia Kristo, ujue huyo ni Roho Mtakatifu ndani yako, ujue hiyo ni Nuru ya Kristo ndani yako inakumulikia, uone njia. Ni jukumu lako kuifuata, na kuitii bila kupoteza poteza muda, na kutenda yanayokupasa kufanya..

Hii neema sio ya kuchezea kabisa, ni kweli bado ipo duniani haijaondoka, lakini huwa haina tabia ya kuganda sehemu moja, inazunguka, , kama wakati wako umefika halafu unaipuuzia, ikiondoka hutaipata tena.

Hivyo ndugu yangu ni heri ukamaanisha kumpokea Yesu leo, angalia muda mchache bado unayo.

Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo, basi tafuta mahali pa utulivu, kisha piga magoti na sema sala hii kwa sauti na kwa imani, na leo leo Yesu atakusamehe na kuanza kukufanya mwanae.

Sema maneno haya;

“Ee Mungu wangu, nimetambua hakika ya kuwa mimi ni mwenye dhambi, Na nimestahili hukumu, nilistahili kupitwa na neema yako ya wokovu, kwa kuipuuzia injili yako uliyonihubiria kwa kipindi kirefu. Lakini sasa ninarudi kwako Kwa kumaanisha kabisa Ee Bwana Yesu.

Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote, nilizokutenda maisha yangu yote. Ninakiri kuwa wewe ndiye, Bwana na mwokozi wa maisha yangu. Na leo hii ninamkataa shetani na kazi zake zote, Nifanye kuwa kiumbe kipya kuanzia sasa, nikutumikie.

Amen.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ili ukamilishe hatua za wokovu.

Hivyo ikiwa utahitaji msaada huo Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *