
BIDII YA EZRA
Shalom Mwana wa Mungu, karibu tujifunze biblia.
Kumbuka biblia kwa sehemu kubwa inaelezea historia ya maisha ya watu kadha wa kadha waliowahi kutokea ili tujifunze kwao yale mazuri. Kwahiyo usomapo habari za akina Nuhu, Ibrahimu, Sara, Musa, Yusufu, Ruthu, Daudi, Ayubu, Danieli, Paulo, Yohana, Mariamu na wengineo usisome tu kama hadithi ya kujifurahisha..bali zitafakari maisha yao na uombe Bwana akufundishe kupitia maisha yao.
Leo tutajifunza kwa mtu anayeitwa Ezra.
Ezra ni nani?
Biblia inasema Ezra alikuwa ni mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa.
Ezra 7: 6 “.. huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa MWANDISHI MWEPESI KATIKA SHERIA YA MUSA, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye”
Maana ya mwandishi mwepesi ni mtu ambaye YUPO TAYARI kufanya jambo, yaani mwepesi katika kufanya jambo fulani, sio mzito..Ndio maana hapo biblia imemtaja Ezra kama Mwandishi mwepesi.
Mwandishi katika desturi za wayahudi alikuwa ni mtu anayefanya kazi kama za sasahivi za uwakili, alikuwa ni mtu anayeijua sheria ya Musa vizuri na hivyo ni rahisi kufahamu kipengele fulani cha sheria kinasema hivi au vile…Katika Agano jipya utaona Bwana Yesu amewataja waandishi sehemu kadha wa kadha..soma (Mathayo 17:10, Mathayo 20:18, Mathayo 21:15, Mathayo 23:2 n.k).
Pamoja na kwamba walikuwa na kazi ya kuhukumu kwa kupitia vipande vya sheria na kufundisha watu, lakini pia walikuwa na kazi nyingine wanayoifanya ya kunakili torati…Kumbuka zamani hizo hakukuwa na mashine za photocopy kama tulizonazo leo…Hivyo Nakala zote zilikuwa zinatengenezwa kwa kunakiliwa tena mahali pengine…
Kwahiyo kazi ilikuwepo kubwa ya kutengeneza nakala nyingi kila siku, waandishi hawa walikuwa wanaandika usiku na mchana, Katika kunakili walikuwa na vigezo vyao vya kufuata, kwanza mwandishi lazima ayatamke maneno Dhahiri ndipo ayaandike, na pia wakati wa kuandika anapokutana na jina la Mungu takatifu YEHOVA alikuwa anasimama kwanza ananawa mwili wote na kuisafisha kalamu yake ndipo aliandike. Na nakala ikishakamilika, itahakikiwa kwa siku 30 kabla ya kuruhusiwa itumike, na endapo zitaonekana kurasa mbili au tatu zitahitaji marekebisho basi nakala nzima inaachwa, kazi inaanza upya. Na kila aya na kila Neno lilikuwa linahesabiwa kuhakikisha na kitabu halisi. Kulikuwa na sheria nyingine nyingi tu katika uandishi…
Hivyo kazi ya uandishi ilikuwa inaheshimiwa sana katika Israeli, na huyu Ezra alikuwa mmoja wao wa hao waandishi, lakini biblia inamtaja alikuwa ni mwandishi mwepesi, yaani alikuwa anaifanya kazi yake kwa kupenda pasipo kusukumwa, na katika ufasaha, tofauti na wengine, Ndiye aliyekiandika kitabu cha Mambo ya nyakati.
Na katika kitabu hichi Roho ya Bwana ilimjia na kuanza kuandika hatua kwa hatua jinsi wana wa Israeli walivyotoka Babeli na kurudi Israeli, kuanzia Kundi la kwanza lililotoka Babeli na kurudi Nchi ya Ahadi mara baada tu ya Mfalme Koreshi kutoa amri ya uhuru wao. Na Kundi hilo ndio tunalolisoma katika Ezra Mlango wa 2.
Naye pia Ezra alikuwa ni miongoni mwa waliotoka Babeli na kurudi nchi ya Ahadi lakini yeye alikuwa katika lile kundi la pili ambalo tunalisoma katika mlango wa 7. Wakati Ezra anarudi kulikuwa tayari kuna lile kundi la kwanza lililotangulia miaka kadhaa nyuma, hivyo kuna mambo ambayo walikuwa wameyasahau yahusuyo sheria za Mungu, na kadhalika hata nyumba ya Mungu ambayo walikuwa wanaijenga upya ilisimama… hivyo Ezra alikusudia moyoni mwake atakaporudi awafundishe na kuwakumbusha wana wa Israeli sheria zote za Mungu wa Israeli na nini torati ya Musa inasema, na Bwana alimsaidia kupata kibali mbele ya Mfalme wa Uajemi, na kusapotiwa kwa kila kitu alichokihitaji ili tu akawafundishe sheria za Mungu.
Ezra 7: 6 “huyo Ezra akakwea kutoka Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye.
7 Nao wakakwea baadhi ya wana wa Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini, ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta.
8 Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme.
9 Maana alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake ulivyokuwa pamoja naye.
10 Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli”.
Utaona mbeleni baada ya Ezra kuingia nchi ya Ahadi, alikuta kasoro nyingi watu tayari walikuwa wameshaanza kufanya machukizo ya kuoa wanawake wageni, kama alivyofanya Sulemani jambo lililosababisha Israeli kugawanyika, na Ezra kama Mwandishi aliijua vizuri Torati hivyo akawaonya na kuwasaidia Wana wa Israeli na kuwarejesha tena kwa Mungu wao.
Na kwa ushujaa wote huo Mungu alimuheshimu, hakuwa Nabii, hakuwa anaona maono, hakuwa mtu mkubwa sana, lakini kwa Moyo wake wa kuwasaidia ndugu zake na kuwarejesha kwenye Torati Mungu alimheshimu, mpaka leo hii tunazisoma habari zake. Hiyo yote ni kwasababu alikuwa msaada kwa wengine kama jina lake lilivyo EZRA Maana yake MSAADA.
Nini tutajifunza kwa Ezra mtumishi wa Mungu.
Ezra alitumia nafasi yake ya uandishi kufanya kazi ya Mungu kwa bidii sana, na halikadhalika na sisi hatuna budi kufanya kazi ya Mungu kwa bidii kwa karama aliyoiweka Mungu ndani yetu. Biblia inasema..
Mithali 22:29 “Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo”.
Ili tupate kibali kwa aliye Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, zaidi ya wakuu wote duniani (yaani YESU KRISTO), hatuna budi kuwa na bidii katika kumtumikia yeye, na kuyafanya mapenzi yake kama Ezra, Nehemia na wengineo.
Anasema,..
Kumbukumbu 28:1 Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, KWA BIDII, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;
Umeona? Tusipokuwa walegevu, Bwana atatunyanyua juu sana tena sana kwasababu ni ahadi yake na haiwezi kutanguka..
Warumi 12:11 ‘kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;’
Hivyo, hakikisha, kile ulichopewa na Bwana unakitendea kazi, zaidi sana angalia ni kwa namna gani utakiweka ili kilete matokeo mazuri katika ufalme wa Bwana, usikifanye bila maarifa, hakikisha unatumia vyote yaani; nguvu zako zote, akili zako zote, roho yako yote, na moyo wako wote kwa pamoja bila kusahau kimoja wapo, ndani ya muda huu mchache uliopewa na Mungu hapa duniani. Na hakika kitakapochipuka kama Bwana alivyokusudia, Bwana atakutukuza sana na utasimama mbele yake kama mfalme siku ile.
Lakini ili hili liwezekanike ni lazima uwe umeokoka kwa kumaanisha kugeuka kabisa na kuacha dhambi. Kinyume na hapo huduma yako ni bure haijalishi utafanya kwa bidii kubwa kiasi gani.
Hivyo kama hujaokoka, ni heri ufanye maamuzi sasa ya kutubu dhambi zote na kumaanisha kuacha ulimwengu kabisa na kutafuta ubatizo sahihi ili upokee Roho wa Mungu ambaye atakupa kiu ya kumtumikia Mungu kwa bidii zote.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea Na..
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.