Elimu ya dunia hii inafunua Elimu ya ufalme wa mbinguni.

Biblia kwa kina No Comments

Elimu ya dunia hii inafunua Elimu ya ufalme wa mbinguni.

Shalom! Mtu wa Mungu karibu tujifunze Neno la Mungu, ambalo ndio Taa yetu ituongozayo uzimani.

ELIMU ni UFUNGUO wa maisha, hiyo ni kweli, lakini ELIMU ILIYO SAHIHI sio tu ufunguo wa maisha, bali pia ni ufunguo wa kila kitu. Na kwa jinsi elimu ya mtu huyo itakavyozidi kuwa kubwa zaidi ndivyo uwezekano wa mtu huyo kufanya mambo yote unavyozidi kuwa mkubwa zaidi.

Kama tunavyofahamu karibu kila kitu tunachokiona hapa duniani kinahubiri hekima ya ufalme wa Mungu, ndio maana asilimia kubwa ya mafundisho ya Bwana wetu Yesu, alitumia mifano halisi ya vitu vya hapa duniani kuelezea siri za ufalme wa mbinguni.

Utaona anasema “Ufalme wa Mungu umefanana na mfanyabiashara, mvuvi, mpanzi/mkulima”, n.k soma Mathayo 13.

Sasa leo tutaangalia hekima iliyopo katika Elimu ya dunia ili tuweze kuelewa Elimu kuu ya ufalme wa mbinguni.

Utafutaji wa elimu ya ulimwengu huu unafanana na utafutaji wa elimu ya ufalme wa Mungu karibu kila kitu. Hii ni kweli kabisa na tutaona ni kwa namna gani, hii itatusaidia kuelewa kwa wepesi na kufahamu jinsi ya kupata elimu ya kimbinguni. Kumbuka biblia inaposema

“Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.(Mithali 4:13)”…

Mstari huo haukulenga Elimu ya darasani…hapana! Bali ulilenga Elimu ya Mungu (Elimu ya ufalme wa mbinguni) Mathayo 13:52..maana huo ndio uzima wetu…wengi wanaupeleka mstari huu moja kwa moja kwenye Elimu ya duniani, lakini hiyo si kweli.. “hiyo ni maana ya pili ya mstari huo lakini maana ya kwanza Kabisa Sulemani aliyomaanisha hapo ni ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI”. Hivyo hatuna budi kuutafuta sana na kushika hii Elimu kuu izidiyo elimu zote.

Sasa kama tunavyojua, tukizungumzia Elimu hutuachi kuzungumzia Shule, hutuwezi kuacha kuzungumzia Waalimu, hutuwezi kuacha kuzungumzia wanafunzi, wala hutuwezi kuacha kuzungumzia Mtaala (ambao upo ndani ya vitabu husika).

Na kadhalika Maisha mapya katika Kristo Yesu ndio shule yetu, Roho Mtakatifu ndio Mwalimu Mkuu wetu, Biblia ndio Mtaala wetu(Kitabu husika)..na wote waliomwamini Yesu Kristo kwa kuzaliwa mara ya pili, kwa kudhamiria kabisa kumfuata kwa kujikana nafsi zao ndio wanafunzi wake…Utasema hilo linapatikana wapi kwenye maandiko…soma

Luka 14:25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.

27 Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU”.

Sasa mwanafunzi kabla hajajiunga na shule yoyote ya kidunia, anakubali kuachana na wazazi wake, na ndugu zake, na hata marafiki zake, anakwenda kujiunga na shule ya Bweni…Huko shuleni hataishia tu kukaa mbali na wazazi wake kwa kipindi kirefu, bali atalazimika kuvikataa pia vile vitu vizuri alivyokuwa anavipenda akiwa nyumbani kama Tv, simu, uhuru, nk..anakwenda mahali ambapo hapana uhuru aliokuwa anautaka, mahali ambapo pengine atakutana na changamoto za chakula kibovu, na malazi mabaya.…

Na katika Ukristo ndio hivyo hivyo unapoamua kumfuata Kristo ni sawa na umejiunga na shule mpya, Maisha yako ya kale unayakataa, pamoja na mapenzi ya wazazi wako…kwasababu unakwenda kutafuta Uzima wako wa baadaye (future), na ndio maana Bwana alisema hapo juu mtu asiyemchukia baba yake, mama yake, mke wake, mume wake, watoto wake, ndugu zake na hata nafsi yake hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Kuchukia kunakozungumziwa hapo sio kuwachukia kwa chuki, bali kuchukia mawazo yao au mipango yao inayokinzana na mapenzi ya Mungu, kwamfano mzazi au ndugu anakuambia inakupasa urithi mikoba ya uchawi, au urithi chuki zake kwa mtu fulani, hapo Bwana anasema hatuna budi kuyachukia hayo mawazo na kuyakataa na kutoshirikiana nao hata kama watakutenga..hapo ni sawa na umewachukia ndugu zako, Kristo anakokuzungumzia..na ndio vigezo vya kuwa mwanafunzi wake.

Ukristo sio mteremko kama wengi wanavyofikiri, ukiamua kumfuata Kristo kupungukiwa wakati mwingine kunakuwepo na pia kuna kupitia dhiki nyingi..tofauti na wale watu wanaowahidia watu uongo kuwa watakafanikiwa siku zote.

Vivyo hivyo unapoingia shuleni, unakutana na sheria za shule na moja ya sheria hizo ni mavazi, na mwiko kutoka nje ya uzio wa shule.…shuleni huwezi kujivalia utakavyo, kunakuwa na UNIFORM maalumu…na wote mnafanana…na huwezi kuingia na kujitokea kama unavyotaka, ukitoka bila sababu maalumu ndio umejifukuzisha hivyo…..

Kadhalika unapozaliwa mara ya pili umekuwa mwanafunzi wa Kristo, na ni lazima uwe na UNIFORM za shule ambayo inafanana na wanafunzi wote. Na sare zetu ni matendo mema ya watakatifu ndiyo Uniform ya shule yetu.

Ufunuo wa Yohana 19:7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

[8]Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.

Hivyo unapojiunga na Elimu ya ufalme wa Mungu ni lazima mavazi yako na mwonekano wako ubadilike, vinginevyo huwezi kuwa mwanafunzi/Mkristo.

Ulikuwa unavaa vimini ni sharti uache, ulikuwa unavaa suruali wewe mwanamke ni sharti uache, ulikuwa unanyoa kiduku na kuvaa nguzo zinazobana na milegezo wewe mwanamume sharti uache, ulikuwa unapenda kusikiliza miziki ya kidunia, na movie zisizo na maana na fashion za ulimwengu, na kuzurura huku na huko vyote hivyo unaacha!…

Mwanafunzi anatambulika kwa uniform, asipokuwa nayo hawezi kutambulika, na Ukristo ni vivyo hivyo huwezi kutambuliwa kama huna vazi la utakatifu.. haijalishi utadai kuwa we ni mkristo, utajulikana tu kuwa raia wa kawaida. Na hata ukiingia kwenye kusanyiko la watakatifu watakushangaa umeingiaje ingiaje huna uniform.

Mathayo 22:11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja ASIYEVAA VAZI LA ARUSI.

[12]Akamwambia, RAFIKI, ULIINGIAJE HUMU NAWE HUNA VAZI LA ARUSI? Naye akatekewa.

[13]Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

[14]Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

Umeona hapo, mkristo ni lazima uwe na UNIFORM za ufalme wa mbinguni (utakatifu wa ndani na nje), la sivyo, utaonekana msamiaji tu na mwisho utakamatwa na kutupwa katika giza la nje.

Na pia Ukristo sio kuingia na kutoka…Ukiingia umeingia! Na ukitoka umetoka…Mwalimu Mkuu huwa hawi mkali kwa Watoto wa mitaani, huwa anakuwa mkali kwa Watoto walioko shuleni kwake, vivyo hivyo Roho Mtakatifu anavyowafundisha watu waliozaliwa mara ya pili ni tofauti na ambao wapo nje.

Kule katika shule za kidunia mwanafunzi hana uhuru wa kujiamuria tu kutoka nje ya shule ovyo ovyo, anatoka kwa kibali na kwa sababu ya msingi vinginevyo atajifukuzisha shule.

Halikadhalika katika ukristo kuna mipaka na sheria, huwezi kutoka na kwenda kusurura sura kule nje (ulimwenguni), halafu urudi baadaye, Roho Mtakatifu mwalimu mkuu hawezi kuruhusu jambo hilo litokee.

Hawezi kukubali mwanafunzi wake kuwepo kwenye mazingira yasiyoeleweka mfano vilabuni, kwenye matamasha ya mipira na wanamziki wa kidunia, au kwenye maparty ya sherehe za ulafi, au vijiweni ni marufuku mkristo kuwepo katika mazingira hayo.

Sasa baada ya kukubaliana navyo hivyo vigezo, ndipo unapewa MTAALA MAALUMU pamoja na Waalimu wa kukufundisha, na wewe mwenyewe unaongeza bidii zako binafsi kujisomea…Ukisubiri tu kila siku kufundishwa darasani na wewe mwenyewe hutaki kutafuta, utafeli mtihani wa Mwisho, na Katika Ukristo ni hivyo hivyo, umezaliwa mara ya pili, wewe kila siku unapenda tu kufundishwa Biblia, muda wa kujisomea mwenyewe huna, utafeli majaribu na hutaendelea mbele kila siku utakuwa unarudia darasa lile lile, miaka yote wakati wenzako wanaenda mbele..

Na jambo lingine baada ya kujiunga na shule za kidunia ni kwamba utakaa shuleni katika hayo mazingira ya kuteseka kwa muda mrefu kidogo inaweza kuchukua hata miaka kadhaa, lakini siku utakapokuja kufanya mtihani wa mwisho na kufaulu utapokea cheti, ambacho hicho kitaonyesha tofauti yako wewe uliyekwenda shule na yule ambaye hajakwenda…kulivumilia viboko vya shule na kula chakula kibovu na wakati mwingine kulala vitanda vyenye kunguni sio bure!…siku utakapohitimu na kupata cheti heshima yako ndio itakapoonekana kuwa hukuwa mjinga kujikana nafsi yako.

Kadhalika Roho Mtakatifu akishakupitisha katika madarasa yake na kuyahitimu vizuri faida zake utakuja kuziona hapa hapa duniani pamoja na katika ulimwengu ujao…lakini sana utakuja kuziona katika ulimwengu ujao kwasababu vitu vya hapa duniani havidumu, vinapita lakini vya huko mbinguni ni vya milele…Siku zile wateule walioshinda watang’aa kama jua mbele za malaika wa mbinguni…

Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?.

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.

29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.

Umeona Umuhimu wa kuitafuta Elimu ya ufalme wa mbinguni sasa?..Elimu ya dunia hii inafunua elimu ya ufalme wa mbinguni, Kristo anapokuambia leo utubu na kuacha dhambi, na ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina lake na uache ulimwengu na mambo yake yote, na kisha umfuate sio kwamba anataka atutese, hapana ni kwasababu anataka atusajili kwenye shule yake ambayo baadaye itatupa cheti kilicho bora! Zaidi kuliko vyeti vyote.. Na heshima! Zaidi kuliko heshima zote….na kumbuka hakuna shule yoyote isiyokuwa na sheria ndio maana anakuambia ewe mwanamke jikane nafsi!! acha mavazi yako ya kikahaba, acha mawigi, acha kupaka wanja, acha mavipodozi baki katika hali yako ya asili…kama unapenda kujipamba subiri tukifika mbingu za mbingu utajipamba utakavyo kama kutakuwepo na kujipamba….lakini kwasasa upo shule!..fanya kile Mwalimu Mkuu anachokuagiza ukifanye kwa faida yako…

Onyesha kumfuata YESU, ikiwa wewe ni mwanafunzi wake kweli.

Ulipokuwa katika shule za kidunia ulipoambiwa uvae sketi za marinda ulitii na usisuke nywele ulitii bila shuruti lakini unapoitafuta elimu ya Roho Mtakatifu hutaki kutiii…nataka nikuambie ukweli bado hujaanza madarasa ya Roho Mtakatifu, bado upo nyumbani wala mtu asikudanganye kuwa upo sawa na Mungu bado haupo sawa, usidanganywe pia Mungu haangalii mavazi anaangalia Roho, ni kweli kabisa anaangalia roho lakini roho inamahusiano makubwa na mwili ndio maana ipo ndani ya mwili, kama vile elimu ya kidunia ilivyo na uvaaji wa wanafunzi wake..Elimu ni ufunguo wa Maisha, yaangalie Maisha yako ya baadaye yatakavyokuwa usijiangalie leo…dhambi za kitambo zisije kukuponza ukaja kujuta milele huko baadaye..Fanyika mwanafunzi wa Kristo leo.

Bwana akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *