Fanya bidii kuwa mnyenyekevu ndani yako.

Biblia kwa kina No Comments

Fanya bidii kuwa mnyenyekevu ndani yako

Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele na milele karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Unyenyekevu ndani ya mtu hautokei tu Kama bahati mbaya au hautokei kama ajali tu la! 

Bali ili unyenyekevu uweze kuumbika ndani ya mtu aliemwamini Yesu Kristo ni lazima afanye bidii yaani akubali kuingia katika madarasa ya Mungu na kufundishwa yaani akubali kuingia gharama ili mchakato huo ukamilike.

Sasa tutaangalia kwa ufupi nini maana ya unyenyekevu?, Pia tutaangalia watu ambao walikuwa ni wanyenyekevu na thawabu gani walipata nasi tunajifunza kwao tutaawaangalia wanadamu kabisa sawa na sisi.

Unyenyekevu, ni Hali ya kujishusha chini. Ni Hali ya kutokujiona kuwa wewe ni bora au unastahili kuliko wengine. Kutokutafuta sifa kwa kujisifu kuhusu mafanikio yako au uwezo wako, kuthamini maoni ya wengine na kuwaheshimu watu wote nk.

Kumbuka ni uwezo wa kujishusha chini sio kushushwa chini!!.

Zaidi sana unyenyekevu unakufanya kukubali udhaifu,makosa pamoja na kuwategemea watu wengine katika maeneo fulani bila kiburi au majivuno.

Wakati mwingine kukubali kushuka chini au kutokutumia uwezo ulionao ilihali unauwezo wa kufanya lolote.

Sasa katika maelezo hayo naimani kuna jambo umelifahamu kwa kina kuhusiana na unyenyekevu ni nini hasa.. ni zaidi ya hilo neno lenyewe na inahitaji kujifunza kila siku na kutegemea neema ya Mungu katika kuwa mtu wa namna hiyo.

Katika hali ya asili kwa kila mtu hakuna mtu anaependa kujishusha,kila mtu wa tabia ya mwilini/asili anataka kuwa juu na kuonekana kuwa yeye ni bora zaidi ya wengine anataka thamani yake itambulike watu wamuone na kumsifu..

 

Tutawaangalia baadhi ya  watu  waliokuwa ni wanyenyekevu sana na Mungu aliwapa neema kubwa sana.

1.Petro.

Mtume Petro ukisoma kwa haraka haraka bila kutafakari kwa kina zaidi(juu juu tu) utaona alikuwa ni mtume ambae alikuwa ni kama msumbufu kwa Bwana Yesu alikuwa ni mtu wa kudadisi sana na kutaka kujifunza zaidi…

Bwana Yesu yeye alimpa mamlaka ya kuwa kiongozi au mwangalizi wa kanisa kifupi Bwana Yesu alimtazama Petro na akamfahamu vyema na ndio maana alikubali kumuweka awe kiongozi wa Kanisa (mwili wa Kristo) sio jambo la kawaida.. tuangalie maeneo machache tu ili tuone Petro alikuwa mtu wa namna gani?

__Petro kukemewa na Paulo. 

Wagalatia 2:11“Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu.”

Kama ukisoma juu hapo nilisema”…..unyenyekevu unakufanya kukubali udhaifu,makosa…”

Mtume Petro alikosea kweli katika kile alichokuwa anafanya na Paulo alimwambia hiyo tabia sio nzuri.. lakini Petro hakujiinua na kuanza kubishana na Paulo alitambua kweli si sahihi na akajirekebisha.. kwa namna ya kawaida hapo Petro angesema..”mimi nimekaa na Yesu Miaka mitatu wewe ambae hata hujakaa na Yesu utanifundisha nini au unajua nini?? Mimi umenikuta kwenye imani muda mrefu wewe ndio umeokoka siku si nyingi utaniambia nini? Huwezi ukaniambia kitu wewe nk”

Maneno hayo au na zaidi angeliweza kuyasema lakini Petro hakujiinua na kutaka mashindano alikubali amekosea na akarekebika..

Je wewe na mimi leo hii tunaweza kukubali kurekebishwa na mtu alietukuta kwenye imani kwa muda mrefu na mtu huyo kaokoka hana hata miaka 2 au 1? Akatuambia hivi si sawa na tulikuwa tunamjua ni mwizi,nk? Na tukakubali kutii na kurekebika bila kujiinua? Tafakari ndugu.

Na kumbuka Paulo anamkemea Petro kiongozi wa kanisa yaani Mchungaji anaejulikana mahali na mahali si jambo dogo hebu litafakari kwa kina..

Tena hakumchukua pembeni kumwambia vile bali katikati ya kusanyiko watu wapo wanasikia.

___Bwana Yesu anamkemea Petro. 

Petro kutokana na upendo wa dhati aliokuwa nao kwa Yesu Kristo hakutaka hata Yesu afe(hakufahamu kufa kwa Yesu Kunaenda kuleta kitu gani kwa watu wote duniani)kabisa lakini mbele ya watu anamwambia Petro maneno haya…

Mathayo 16:23“Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

Fikiria ni wewe unaambiwa maneno haya je? Ungeweza kuendelea kufatana na Bwana Yesu? Tena mbele ya watu wengi?? Kifupi Mtume Petro alikuwa ni mtu mnyenyekevu sana sana..

Na ndio maana katika nyaraka zake zote  kasisitiza sana unyenyekevu, Bwana Yesu hakukosea kumuweka kuwa kiongozi wa Kanisa (mwili wake). Katika nyaraka zake zote kagusia sana unyenyekevu.

2.Musa.

Musa aliudhiwa na kusemwa vibaya na wakina na Dathani,Kora, Abiram na pamoja na timu nzima yakina na Dathani jumla ya watu 250 walikuwa kinyume naye…  wakati mwingine watu (Israeli)wote wanataka k Mpiga kwa mawe kwa sababu ya kukosa kitu fulani lakini Musa alikuwa na uwezo wa kusema chochote pale lakini alijishusha akazidi Kumuomba Mungu na kuwaombea rehema kwake na Bwana akawarehemu..

Lakini Musa hata aliposikia maneno ya kina Dathani hakujiinua lakini alishuka chini kabisa alikuwa na uwezo wa kujisifu lakini yote anasema Bwana ndio atakeyeonyesha yeye ni nani aliemtakatifu na anaestahili kusogea kwake angeweza kujihesabia haki kuwa yeye ndio pekee anaongea na Mungu lakini hakufanya hivyo.

Hesabu 16

3 nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n’nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana?

4 Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi;

5 kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake.

Si kawaida ya mwanadamu wa tabia ya asili kuwa mtu wa namna hii mtu asiyeomba,asiyesoma neno nk hawezi hata kama anasema ameokoka..

Musa alikuwa anaweza kabisa kujiona kuwa ni spesho zaidi yao alikuwa anaongew na Bwana uso kwa uso nk Mungu alimtumia yeye kuwavusha Israeli kwenda kanani angeweza kujiona kuwa yeye ndio kila kitu na angeweza kuwapuuza watu na asiwakilize lakini haikuwa hivyo..

 

Utakumbuka hata wale wana wa Selofehadi(Hesabu 27:1-11)baada ya kwenda kudai haki yao Musa hakuwapuuza na kuendelea na mambo yake lakini haikuwa hivyo aliwasikiliza na kuwapatia haki yao.. hakuwadharau.

Alikubali kushauriwa na baba mkwe wake Yethro nk

Sasa unawezaje kuwa mnyeyekevu?

Hakuna njia mpya zaidi ya kuwa mtu wa kusoma neno na kulitendea kazi,kuwa mtu wa kuomba Mungu akusaidie katika hilo eneo unapokuwa msomaji wa neno na kutafakari neno la Kristo litakaa ndani yako na litakapokaa ndani yako vizuri ukajaa Roho basi hata wakati unapotaka Kujiinua neno lililoko ndani yako litakwambia/Roho Mtakatifu atakukumbusha kuwa hii sio asili yako hutakiwi kuenenda hivyo..

Mkristo ukiwa mzito katika eneo la kusoma neno na kuomba na kufanyia kazi kile unachojifunza kutaka kujizoesha kuwa mtu wa namna hiyo. Mkristo asiyekuwa na vitu hivi huyo ni Mkristo msumbufu kanisani na usiekuwa na msaada wowote katika kuujenga mwili wa Kristo.

1 Petro 5

5 Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.

6 Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.

Naimani na nimekuombea Bwana akuongezee neema ya kuwa mnyenyekevu zaidi na Bwana atakukweza kwa wakati wake..

Ubarikiwe sana.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *